Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru kwa kupata nafasi hii ya kuweza kuchangia katika hotuba hii ya Mheshimiwa Mpango. Vilevile nimpongeze sana Mheshimiwa Mpango kwa hotuba nzuri ambayo ameiwasilisha hususani kwa kuweza kugusia vipengele muhimu, kuainisha vipengele ambavyo ni vya kipaumbele kwa mwaka huu wa fedha 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimevutiwa sana na kipengele cha kuainisha kwamba moja ya vipengele vya msingi ni Mchuchuma pamoja na Liganga. Hii itakuwa ni mkombozi lakini nimwombe sana Mheshimiwa Mpango aweze kuangalia anavyoenda kushughulikia hivi vipengele vya msingi aangalie sana kwa yale maeneo ambayo yanazalisha makaa ya mawe (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia kwa Mkoa wangu wa Songwe, katika Wilaya ya Ileje kuna makaa ya mawe, vilevile ukienda kwenye Wilaya ya Mbozi Magamba kuna makaa ya mawe. Nichukue nafasi hii kumwomba sana Mheshimiwa Mpango aviunganishe pamoja haya maeneo katika mpango huu mkubwa wa mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuweza kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya kwa Taifa letu. Sote ni mashahidi tumeshuhudia namna ambavyo Rais anapambana kuhakikisha kwamba anasimamia rasilimali za Mtanzania likiwepo suala la madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashangaa sana watu ambao wanaibuka katika Bunge hili kuponda jitihada kubwa ambazo Mheshimiwa Rais anazifanya. Jana nimemsikiliza kwa umakini sana Mheshimiwa Msigwa, ameuliza kwamba eti Mheshimiwa Pombe Magufuli alikuwa wapi miaka yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea kama ambavyo Watanzania huko nje sasa hivi wameungana na Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba wanamtia moyo katika vita hii kubwa ambayo ameianzisha, nilijua kabisa kwamba hata humu ndani Bungeni tutaungana wote kwa pamoja kuhakikisha kwamba tunamtia moyo Mheshimiwa Rais, lakini wenzetu wanauliza kwamba alikuwa wapi. Sasa kwa sababu yeye ameamua kufukua makaburi na mimi naomba nimsaidie kufukua makaburi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, historia ya huko nyuma, ukifuatilia historia ya nchi hii, wakati Mwalimu Nyerere akiwa Rais, Mzee wangu Ndugu Mtei alikuwa ni Waziri wa Fedha na hilo wenzangu wanalijua vizuri sana na tutakumbuka kwamba ni Ndugu Mtei huyu ambaye alimshawishi Mwalimu Nyerere kwamba akubaliane na masharti magumu ambayo walitupa mabeberu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sharti mojawapo ikiwa ni kwamba kuweza kushusha thamani ya fedha yetu, lakini Mheshimiwa Nyerere alikataa na alipokataa tunaona kabisa Mzee wangu Mtei alijiuzulu na akahama nchi akaenda kufanya kazi World Bank kwa wale wale mabeberu ambao alikuwa anawatetea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo siyo jambo jipya kushuhudia hawa wenzetu wakiendelea kutetea mabeberu ndani ya Bunge hili, kwa sababu hata Muasisi wao ni kitu ambacho alishakianzisha tangia huko nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi wanavyouliza kwamba Mheshimiwa Magufuli alikuwa wapi? Wakati Mwinyi akiwa Rais Mheshimiwa Lowassa pamoja na Mheshimiwa Sumaye walikuwa ni Mawaziri, kweli siyo kweli? Sasa na kipindi hicho Magufuli hakuwa Waziri. Sasa unapouliza Mheshimiwa Magufuli alikuwa wapi, naomba waanze kuwauliza ambao wanao huko Mheshimiwa Lowassa pamoja na Mheshimiwa Sumaye walikuwa wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, Mheshimiwa Mkapa akiwa Rais wa nchi hii Sumaye alipanda cheo akawa Waziri Mkuu kwa maana ndiye Kiongozi wa shughuli zote za Serikali ikiwemo suala la mikataba ya madini. Sasa leo hii wanauliza kwamba eti Magufuli alikuwa wapi, kaka yangu Msigwa amenisikitisha sana. Hata kwenye Serikali ya Jakaya Mtendaji Mkuu wa Serikali Mkuu wa Serikali alikuwa ni Mheshimiwa Lowassa na mikataba yote ambayo ilikuwa ikisainiwa katika Bunge hili yeye alikuwa anahusika na sote tunafahamu alishirikiana na Karamagi kwenda nje wakaenda wakasaini mkataba ambao leo hii umeliingiza Taifa letu katika matatizo makubwa. Sasa mtu anapohoji kwamba eti Magufuli alikuwa wapi, naomba kabisa kwamba aanze kumuuliza Mheshimiwa Lowassa pamoja na Mheshimiwa Sumaye walikuwa wapi? Kwa sababu wao kipindi hicho ndio walikuwa Watendaji Wakuu wa shughuli zote za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme jambo moja, inapokuja vita kama hii ni vizuri kama Taifa tukaungana wote kwa pamoja kumsemea na kumshauri Rais wetu. Kaka yangu Mheshimiwa Lissu unapoanza kutaja watu kwamba Mheshimiwa Jakaya alihusika kusaini, unasahau kabisa kwamba Jakaya akiwa Waziri wa Maji Sumaye alikuwa Waziri Mkuu. Sasa nashangaa jana umemtaja Jakaya lakini Sumaye vipi ulimsahau? (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, inaonesha kabisa kwamba hawa watu ni watu ambao wanafanya vitu kwa double standard, ni watu ambao hawajielewi na sasa hivi Magufuli amewashika pabaya, walizoea kufanya siasa za matukio, siasa za matukio sasa hivi hamna. Walizoea mtoke humu Bungeni wakafanye maandamano, sasa hivi wananchi wanakipenda sana Chama cha Mapinduzi na ndio maana wanavyoona Rais anafanya kazi nzuri wanageuka wanasema Rais hatekelezi Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie masuala ya madini yapo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi na ukisoma ukurasa wa 28 imezungumzia kwamba Serikali hii itaenda kusimamia kuhakikisha kwamba suala la madini linawanufaisha Watanzania wote wakiwepo Watanzania ambao ni maskini. Sasa mtu anapokuja kusema kwamba haipo kwenye ilani anajitahidi baada kuona kwamba Serikali yetu inafanya kazi nzuri sasa hivi, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli anafanya kazi nzuri, anageuka kuanza kumtenga Rais pamoja na Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo rahisi kumtenga Rais wetu na Ilani ya Chama cha Mapinduzi, kazi anayoifanya anafanya kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Kumtenga Rais na Ilani ya Chama cha Mapinduzi haiwezekani ni kama kumtenga Lowasa na ufisadi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba nizungumzie jambo moja. Kuna suala ambalo limejadiliwa katika bajeti yetu kuhusiana na road license, wasijaribu kupotosha umma, Serikali imefuta na kuondoa kabisa tozo ya road license. Kwa hiyo, hili ni jambo ambalo limepunguza mzigo mkubwa sana, mzigo ambao ulikuwa ni lazima mwananchi aweze kwenda kulipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi hiyo tozo ambayo imeongezeka, tumshauri Waziri Mpango ahakikishe kwamba hiyo tozo Sh.40/= moja kwa moja anaipeleka katika kutatua changamoto za Mtanzania. Kwa sababu Mtanzania wa sasa anachoangalia je, hiyo Sh.40/= inaenda kufanya kazi gani? Shida hapa siyo tozo kuongezeka, shida ni kwamba hiyo tozo inayoongezeka inakwenda kufanya kazi gani? Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Mpango hiyo Sh.40 ambayo imeongezeka basi iende moja kwa moja kutatua matatizo ya Watanzania ikiwepo matatizo ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mpango katika Mkoa wangu wa Songwe akinamama wanapata shida kubwa sana ya maji na ni jambo ambalo nimekuwa nikilisema katika Bunge hili. Kwa hiyo, naomba sana namna pekee ya kuweza kuwapunguzia Watanzania machungu ni kuhakikisha kwamba tunatatua kero za Watanzania. Tunaomba sana hiyo pesa iende moja kwa moja kutatua kero za maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kesema hayo, nashukuru na naunga mkono hoja.