Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB – MWENYEKITI KAMATI YA MAMBO YA NJE, ULINZI NA USALAMA: Mheshimiwa Naibu
Spika, kwanza ningependa kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia na Waheshimiwa Mawaziri kwenye hoja yangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge 10 wamechangia kwenye hoja hii, watano kwa maandishi na watano kwa kuongea na Mawaziri, nawashukuru sana.

Waheshimiwa Wabunge waliochangia kwa maandishi ni Mheshimiwa Rhoda Kunchela, Mheshimiwa Lucia Mlowe, Mheshimiwa Zainabu Amiri, Mheshimiwa Mary Muro na Mheshimiwa Cosato Chumi. Mengi ambayo wameongea ni maoni ambayo tutayapeleka Wizarani kwa ajili ya kushughulikiwa na kwa mfano Mheshimiwa Rhoda amezungumzia mambo ya vitambulisho kwamba NIDA waweze kupewa uwezo waweze kutoa vitambulisho kwa haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri Waziri wa Mambo ya Ndani yupo hapa tutampa hiyo hoja na Mheshimiwa Lucia Mlowe amezungumzia mambo ya crime ambayo matukio ya kupotea watu ambayo nimeyazungumzia kwa kirefu sana na kuwataka polisi basi hao watu ambao wanapotea na kutekwa na watu wasiojulikana basi wajitahidi kuhakikisha kwamba hao watu wanaofanya vitendo hivyo wanajulikana na wanakamatwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kukamatwa Wabunge ndani ya Bunge limeshughulikiwa vizuri na sasa hivi nafikiri polisi wana hayo maagizo kwamba ni lazima waripoti kwa Katibu wa Bunge kabla ya kuendelea kutekeleza hiyo kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia suala la ucheleweshaji wa kesi ambayo limezungumzwa kwa kirefu na kwenye taarifa yangu/kwenye hoja yangu nimeeleza mbinu mbalimbali ambazo kamati imeona Jeshi la Polisi inatakiwa zichukue ili kuharakisha upelelezi wa makosa mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Zainabu amegusa mambo ya kuongezewa zimamoto nyenzo na kuweza kulipwa kupewa fedha kwa ajili ya maendeleo kama ambavyo tumezungumza kwenye hoja yangu. Mheshimiwa Mary Muro kazungumzia msongamano wa Mahabusu na Wafungwa ambao ameuzungumzia kwa uchungu lakini na kwenye taarifa yetu, kwenye hoja yetu tumeelezea na kuwataka Serikali kuhakikisha kwamba basi kesi ambazo ziko Mahakamani zinasikilizwa kwa haraka inavyowezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Cosato Chumi ameshauri ufunguzi wa Balozi mbalimbali kule Lubumbashi na Guangzhou, China ambapo kwa kweli kwenye Kamati tumelizungumzia suala hili kwa makini sana na kumshauri Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa aweze kulichukua suala hili, kwa sababu hizi sehemu ni sehemu za biashara. Lubumbashi Watanzania wengi sana wanakwenda kwa ajili ya kufanya biashara, pamoja na Guangzhou wanakwenda wengi sana ni lazima tuwe na Balozi ndogo kwenye hizo sehemu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge watano wamechangia kwa kuongea tukianza na Mheshimiwa Katani ambaye amezungumzia suala la ulinzi wa Wabunge ambaye ame-support issue hiyo akihusisha na kupigwa risasi kwa Mheshimiwa Tundu Lissu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwamba kwenye ile hoja yangu kwenye taarifa hiyo nimeongea kwa kinaga ubaga kwamba kuna suala la mlinzi na kuna suala la ulinzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesisitiza sana suala la ulinzi, Jeshi la Polisi ni lazima lihakikishe kwamba basi linatoa ulinzi kwa Waheshimiwa Wabunge kwenye makazi na kwenye maeneo ambayo wanaishi. Haina maana kwamba watoe mlinzi, kwa hiyo kuna mbinu mbalimbali ambazo wanazotakiwa kufanya kama kufanya doria na kadhalika, kama ambavyo ameelezea Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, isipokuwa suala la usajili wa gari nimelieleza kwa ufafanuzi mkubwa kama mamlaka inahusika itaridhia basi ingekuwa ni vizuri ili usajili wa magari ya Wabunge basi yaonekane kama ni MB so, so, so au Viti Maalum so, so! Kwa hiyo, suala hilo ni la muhimu isipokuwa hapo ni lazima Wabunge waangalie kwamba gari gani hiyo ambayo unataka kuiwekea inazunguka na bendera. Kwa hiyo ni lazima uangalie na nafikiri taratibu zingine zitafuatwa namna ya kushughulikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Ishengoma ametaja mambo ya amani na ulinzi ambayo kwa kweli ni Jeshi la Polisi linatakiwa liongezewe tu nyenzo na fedha ili liweze kukabiliana na uhalifu mbalimbali ambao unatokea hapa nchini.

Mheshimiwa Msigwa ametaja tukio la Mheshimiwa Tundu Lissu kwamba waliomba vyombo vya kimataifa vije kuchunguza tukio hilo, lakini ninavyofahamu ni kwamba ni lazima pana conditions zake kabla ya kuleta vyombo vya kimataifa. Ukianzia kwanza na tukio lenyewe, hilo kosa lenyewe linakuwa regarded kama nini, ni international crime, ni organize crime au ni domestic crime. Sasa na hawa wapelelezi ambao unataka kuwaleta je, tuna mahusiano nao kwa kinchi. Kwa hiyo, ni suala ambalo linatakiwa liangaliwe na sio kuwaleta wapelelezi kutoka nje kwa kienyeji.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la immigration mimi niliwakilisha kamati kwenye kupokea passport mpya hizi za e-immigration sasa na Mheshimiwa Rais pale alisema kabisa kwamba wamejaribu kuokoa kutoka kwenye wajanja walikuwa wameweka bilioni 400 pale lakini wametengeneza huo mradi wa hizi passport mpya kwa bilioni 50. Sasa hebu angalia hapo ni kiasi gani fedha ambazo zimeokolewa. Lakini nachosema hivyo ni kwamba sasa sidhani kama hizo taarifa ambazo anazo Mheshimiwa Msigwa zina ukweli kiasi gani kwa sababu mpaka Mheshimiwa Rais atangaze pale sidhani kama watu wanaweza wakampa taarifa ambazo ni za uongo.

Mheshimiwa Mwambalaswa ameelezea usalama wa Wabunge ambao nimeshaufafanua kwa kirefu lakini amesisitiza suala la ujenzi wa nyumba za Wabunge kwa sababu tuko Dodoma hapa Wabunge ni lazima watakuwepo kwa hiyo, ni muhimu sana Ofisi za Bunge zikafikiria namna ambazo zinaweza zikatengeneza Kijiji cha Wabunge ambacho kitakuwa na urahisi wa kuwalipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Mheshimiwa Nape Nnauye limefafanuliwa vizuri na Mheshimiwa Waziri wa Nchi na sijui kama kuna umuhimu wa kuileta Bungeni hiyo Sheria ya Usalama wa Taifa kwa sababu kazi za Usalama wa Taifa zinajulikana na ni intelligence informations na kushauri taasisi mbalimbali. Lakini nimeshindwa kuelewa hapa ilivyohusishwa na EPA pamoja na Diplomasia ya Uchumi ambayo kila watu na mikataba wako wataalam kwenye hizo sehemu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema, kutoa ufafanuzi huo naomba sasa kutoa hoja ili mapendekezo yote na maoni ambayo nimeyaeleza yaweze kukubaliwa na Bunge hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)