Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

Hon. January Yusuf Makamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bumbuli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi uliyonipatia ya kuchangia hoja zilizowasilishwa leo. Nianze kwa kuwapongeza sana Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Viwanda, Biashara na Mazingira kwanza kwa taarifa yao nzuri kwenye eneo letu lakini pia kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya katika kipindi chote ambapo tumekuwa tunafanya nao kazi. Tunawapongeza na kuwashukuru sana wametupa ushauri, miongozo na tumeelekezana na tumefanya kazi nzuri. Kwa hiyo, Mwenyekiti aliyetangulia na Mheshimiwa Murad sasa na Wajumbe wote hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yamezungumzwa mambo mengi kwenye taarifa lakini nitazungumza mawili tu kutokana na uchache wa muda. Kwanza, ni suala zima la uwezo wa kifedha na fedha zinazotolewa kwa ajili ya usimamizi wa mazingira nchini. Nadhani wote tunakubali kwamba jambo hili tumelizungumza katika vikao mara nyingi kuhusu umuhimu wa hifadhi wa mazingira lakini uwezo mdogo wa rasilimali wa kufanya zile kazi zinazotakiwa kufanywa na Kamati ya Bunge imelieleza hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ambacho naweza kuliambia Bunge lako Tukufu ni kwamba tunaendelea kuzungumza ndani ya Serikali kati yetu sisi, Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara ya Fedha kuhusu namna ya kudumu ya kuweza kupata fedha za hifadhi ya mazingira kwa vyanzo mahsusi. Tulianza mwaka juzi kwa kupendekeza maeneo kadhaa ya mapato ambapo kufanyika kwa hizo shughuli moja kwa moja kunaathiri mazingira. Kwa mfano, mapato yanayotokana na magogo, mkaa na uingizaji wa bidhaa ambazo zinachafua mazingira, basi asilimia kadhaa ya mapato hayo iende kwenye Mfuko wa Mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo hayo yamewasilishwa kwenye Kamati ya Think Tank ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha, yametafakariwa na baadhi yametafakariwa na Kamati ya Bajeti ya Bunge katika Bunge lililopita. Imani yetu ni kwamba ndani ya Serikali tutamaliza mazungumzo ili mwaka ujao wa fedha sasa pale tutakapokuwa tumeelewana basi tutakuja na mapendekezo ya vyanzo vya kudumu na vya uhakika kwa ajili ya Mfuko wa Mazingira ili tuweze kuwa uwezo na nguvu kubwa ya kusimamia Sheria ya Mazingira lakini kurekebisha pale maeneo ambapo mazingira yatakuwa yameharibika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi dhamira yetu ni pale Wabunge katika Majimbo yao watakapokuwa wanaona changamoto ya mazingira, basi iwe rahisi kwao wanapotuambia sisi, sisi tuweze kujibu kwa uharaka tukiwa na uwezo wa fedha wa kusaidia kurekebisha mazingira yanayoharibika. Kwa hiyo, hii ni kazi yetu sote sisi ndani ya Serikali lakini pia Wabunge kama watu wenye sauti na wenye uwezo wa kupanga fedha tushirikiane ili tuweze kuhakikisha kwamba Mfuko huu unajaa fedha ili tuweze kufanya mambo ambayo Wabunge wanataka tuyafanye na mambo mengine ambayo tunaendelea kuyafanya ikiwemo kutafuta fedha kutoka kwenye vyanzo mbalimbali huko duniani na kwa washirika wetu wa maendeleo wa Kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ambalo ningependa kulizungumzia ni suala la mifuko ya plastiki, limezungumzwa hapa na limezunguzwa kitambo humu Bungeni na Kamati yetu ya Bunge imelitafakari na tumetafakari kwa pamoja sisi pamoja na wenzetu wa Wizara ya Viwanda na Biashara. Nataka kusema kwamba katika taarifa ya Kamati ya Bunge mtaona imeeleza kwamba nchi yetu viwanda vyote vilivyopo nchini mwaka jana 2016 vilizalisha tani 73.6 za mifuko ya plastiki lakini pia taarifa hiyo hiyo inasema mifuko ya plastiki iliyoingizwa kutoka nje ni tani 1,354. Kwa hiyo, utaona kwamba asilimia zaidi ya 90 ya mifuko ya plastiki inatumika nchini ni ile iliyotoka nje ya nchi siyo inayozalishwa ndani ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna utata wa takwimu kuhusu idadi ya watu ambao wameajiriwa katika viwanda hivi kwa sababu kama viwanda viko 46 vinazalisha tani 73 kwa mwaka maana yake kila kiwanda kinazalisha chini ya tani moja na nusu kwa mwaka jambo ambalo kidogo ni gumu kulitafakari. Kwa hiyo, sisi kama Serikali tutaendelea kulishughulikia jambo hili na Kamati ya Bunge imeelekeza kwamba tupige marufuku uingizaji wa mifuko kutoka nje ya nchi ili hatimaye tuelekee katika kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba jambo hili lina implications kikodi, kiajira na kadhalika lakini sisi kama Serikali au sisi kama Ofisi ya Makamu wa Rais tumeona kwamba madhara ya matumizi ya mifuko ya plastiki ni makubwa katika mazingira na afya ya watu wetu. Kwa hivyo basi, tutashirikiana na wenzetu wa Wizara ya Fedha, bahati nzuri Sheria ya Mazingira, kifungu cha 80 kinampa mamlaka Waziri mwenye dhamana ya mazingira kwa kushirikiana na kushauriana na Waziri mwenye mamlaka ya fedha kutengeneza nyenzo za kiuchumi zitakazoweza kushamirisha mbadala wa bidhaa zinazoharibu mazingira. Kwa hiyo, nitazungumza na mwenzangu wa Wizara ya Fedha tuone nyenzo zipi za kiuchumi zitakazotusaidia ili tutakapopiga marufuku mifuko ya plastiki basi kuwe na uchumi mpya wa mifuko mbadala na huko ndiko tunakoelekea na ndiko huko tunakotaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu jirani zetu karibu wote wamepiga marufuku mifuko ya plastiki lakini hawajapiga marufuku uzalishaji wa mifuko ya plastiki. Kwa hiyo, mifuko ya plastiki kwa mfano kwenye nchi moja ya jirani hawaitumii pale lakini wanaizalisha na hawajafunga viwanda kwa sababu sisi tunaruhusu. Kwa hiyo, sisi tumekuwa ni dampo la mifuko ya plastiki. Tunaamini kwamba tutakapozuia na sisi matumizi ya mifuko ya plastiki basi hata mianya inayotumika kuingiza mifuko hii nchini mwetu na yenyewe itazibwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni uamuzi mkubwa ambao utaathiri maisha ya watu na namna wanavyoishi lakini naomba tu niseme kwamba tukubali na tuwe tayari kuupokea uamuzi huu wakati wowote. Wale wenzetu wenye viwanda tulishatoa tahadhari tangu mwezi Mei mwaka jana kwamba uamuzi huu unakaribia na tutakapofika tu kwamba kufanya uamuzi huu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja nimalizie.

Wenzetu wanaozalisha na kuingiza mifuko ya plastiki itakapofika wakati Serikali itakapofanya uamuzi wa kupiga marufuku isije ikasemekana kwamba hatukuwa na taarifa ya kutosha. Hapa Bungeni katika Kiti hiki hiki mwezi Mei mwaka juzi 2016, tulitoa taarifa kuhusu dhamira hii ya Serikali. Kwa hiyo, tunaomba tu wajiandae kwamba tutafikia huko

lakini kama nilivyosema Serikali yetu kwa kujua kwamba lazima kupatikane mbadala basi itatengeneza mazingira ya kushamirisha uzalishaji wa mifuko mbadala ili watu wetu wasipate shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, naunga mkono mapendekezo ya Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii.