Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

Hon. Livingstone Joseph Lusinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mungu kupata nafasi hii ya kuchangia hoja za Wenyeviti wa Kamati walizoziwasilisha mbele yetu. Nami nitoe pole kwa familia ya Ndugu Kingunge Ngombale-Mwiru, Mwanasiasa Mkongwe wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakati mwingine Bunge zinapokuja hoja za msingi kama hizi tatu kwa pamoja zinaletwa na Kamati halafu sisi wenyewe Wabunge tunajinyima tena nafasi ya kuzichangia, kidogo hapo Bunge tunakuwa ni kama vile hatujitendei haki. Ukiangalia hoja hizi ni za Kamati zetu na wachangiaji ni sisi Wabunge, kuna sababu gani ya kujipa dakika saba wakati uamuzi ni wa Bunge lenyewe? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo, nataka kwa haraka haraka nichambue baadhi ya mambo machache, nikijikita zaidi kwenye hoja ya Kamati ya Viwanda na Biashara. Kuna tofauti kubwa kati ya kujenga uchumi wa viwanda na kujenga viwanda vyenyewe. Unapotaka kujenga uchumi wa viwanda hasa kwa sisi Wabunge wa Vijijini ni vyema viwanda hivyo vikawa na chain. Kama vinahusu kilimo vikajipanga katika mpango ambao utawafanya wakulima wanufaike moja kwa moja na uwepo wa viwanda hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, unapokuwa na viwanda vya mazao ya mifugo, halafu kukawa na viwanda vya mbolea ambavyo vinagusa moja kwa moja wakulima, kutaifanya nchi yetu ipate kodi ya kutosha kwa wakulima na wakulima wenyewe wakajiletea maendeleo makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo kubwa sana la mwingiliano wa Taasisi za Serikali. Kwa mfano, ukiangalia kazi zinazofanywa na TFDA na TBS unaona ni kazi ileile moja, mfanyabiashara anaweza kupata certificate ya TFDA lakini TBS wakamkatalia. Kwa hiyo, unaweza kuona jinsi vyombo Serikali vinavyokuwa kikwazo cha kuhakikisha wanapata kodi ya kutosha na kupata maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati Kamati ya Viwanda na Biashara iliwahi kutembelewa na watu wa konyagi, wakaleta aina 32 za viroba na zikaonekana ni hatari Serikali ikazipiga marufuku, lakini leo viroba vinarudi tena kwa mlango wa uani, watu wanavipaki kwenye chupa, havina
stika za ubora za TBS, hazina stika za TRA wanakwepa kodi lakini vinauzwa. Wale wafanyabiashara ambao wanafuata utaratibu wanatozwa kodi kubwa wanajikuta wenzao wanauza kwa bei ya chini wao wanauza kwa bei ya juu, hawapati wateja, matokeo yake Serikali inashindwa kukusanya fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi mtu anayeuza kinywaji kikali kwenye chupa ya plastiki, haina nembo zozote za Serikali, nani atajua ubora wa kinywaji hicho? Matokeo yake bado tunaendelea kuwaangamiza vijana wetu kutokana na uwepo wa viroba kwa njia ya uani. Tunaomba leo Mheshimiwa Mwenyekiti utakapokuwa ukipitia tupate majibu ya kutosha kwenye jambo hili.

Mheshimiwa mwenyekiti, unajua Mungu akikupa kilema anakupa na mwendo wa kukitembelea, hawezi akakupa kilema akakunyima mwendo. Nataka niweke usahihi kidogo tu, ukitazama makusanyo ya kodi, walipokuwa wakikusanya Halmashauri, 2014/2015 walikusanya shilingi bilioni 18.9. Baada ya Serikali Kuu kuchukua na kuanza kukusanya wenyewe kupitia TRA kwa mara ya kwanza mwaka 2015/2016 walikusanya shilingi bilioni 28.2. Mwaka uliofuata, 2016/2017, Serikali walikusanya shilingi bilioni 34.9 maana yake kuna ongezeko hapo. Mwaka wa 2017/2018, kwa robo mwaka wamekusanya shilingi bilioni 16.6.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo langu mimi siyo kukusanya ila ni namna gani zinarudi kwenye Halmashauri ili ziweze kujitegemea. Ni kweli mmekusanya sana kuliko walipokuwa wanakusanya Halmashauri wenyewe lakini ni namna gani zinarudi ili ziweze kuleta maendeleo kwenye Halmashauri zenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine kubwa linaloleta mgongano kati ya Kamati ya Bajeti na Wizara ya Fedha. Kwenye Halmashauri kunakuwa na bajeti ndogo za Halmashauri, wanapitisha vyanzo vyao vya ndani, wanapitisha namna ya kukusanya, inapokuja kwenye bajeti

kuu, vile vyanzo vinafutwa halafu hakuna namna ya kuvifidia. Kwa hiyo, tunajikuta tunakuwa na bajeti za Halmashauri ambazo zimefelishwa na kutokuwepo na vikao vya mwanzoni kati ya Kamati ya Bajeti na Wizara ya Fedha. Mkiweza kukutana mapema mkaondoa mkanganyiko huu, maana yake Halmashauri haziwezi kupanga bajeti ambazo huko mbele ya safari zitakuja kukataliwa na Serikali Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kuwe kuna vikao vya kutazama bajeti vya mapema, tunashindwa nini? Kwa sababu leo hata zile tozo za kero ambazo tulizifuta, bado hazirudishwi kwenye Halmashauri. Kwa hiyo, Halmashauri zinashindwa kujiendesha, zinakosa mapato ya kutosha kuweza kuwaletea maendeleo wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia kuwaomba sana, Wizara ya Viwanda na Biashara hebu tuleteeni orodha kati ya vile viwanda 130 na kitu vilivyobinafsishwa vingapi vinafanya kazi na vinafanya kazi kwa ufanisi gani? Leteni hapa orodha ili Waheshimiwa Wabunge tujue kumbe tangu tumeanza kuongelea viwanda kuna viwanda kadhaa vimeanza kufanya kazi na viwanda kadhaa bado vipo kwenye maandalizi ya kuhakikisha vinaendelea kufanya kazi. Vinginevyo tutakuwa tunapiga kelele hapa ya viwanda, viwanda kumbe hakuna kiwanda hata kimoja ambacho kinafanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie habari ya namna gani tunaweza kuzisaidia Halmashauri zetu. Halmashauri zinaweza kujiendesha zenyewe lakini pale ambapo vyanzo vyake vya makusanyo ya ndani vinaheshimiwa na Serikali Kuu. Tusiwe tunakuja tunafuta halafu baadaye tunazitaka zijiendeshe, hawataweza! Waheshimiwa Madiwani wamepitisha vizuri makusanyo yao ya ndani, wameyatungia sheria ndogo tunapokuja sisi kukataza huku juu maana yake tunawaweka katika mazingira magumu sana ya kuhakikisha wanapata mapato ya kuendelea kujiendesha wao wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, niombe sana Serikali na Wenyeviti wa Kamati watakapokuwa wanayapitia haya wayatilie maanani sana ili tuweze kusonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.