Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

Hon. Naghenjwa Livingstone Kaboyoka

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii tena ya kuweza kufanya majumuisho ya taarifa ya PAC tuliyoileta asubuhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie fursa hii kukushukuru tena wewe binafsi kwa kuongoza mjadala huu tangu asubuhi mpaka sasa hivi. Naomba pia niwashukuru wachangiaji wote waliochangia hoja hii; kwa kuwa wengi wanaunga mkono taarifa ya Kamati katika kusimamia matumizi ya fedha za umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahili kwamba Waheshimiwa Wabunge wanachukizwa na matumizi mabaya ya fedha za umma. Wachangiaji waliochangia ni wengi akiwemo Mheshimiwa Allan Kiula ambaye amezungumzia mradi wa Mlimani City, Suma JKT, Polisi na TANESCO. Mheshimiwa Munde pia ameongea kwa undani mambo ya TANESCO na NSSF, Mradi wa Dege pamoja na Mlimani City, Mheshimiwa Catherine amezungumzia Mlimani city na NSSF. Wote hawa pamoja na wachangiaji wenzangu wengine ambao si rahisi kila mmoja kusema eneo lake.

Lakini Mheshimiwa Gekul amezungumzia mambo ya Pride, Mheshimiwa Mussa Mbarouk amezungumzia mambo yote yaliyoko kwenye taarifa yetu, Mheshimiwa Kigua mambo ya ALAT na Mheshimiwa Mabula umesisitiza ripoti ya Kamati Ndogo ambayo mwisho iliridhiwa na Kamati yote kwa Spika na pia akazungumzia mambo ya Mlimani City.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wenzetu wengine wamechangia kwa kuleta kwa maandishi ambao ni wengi na nafikiri majina yao ninayo. Walioleta ni pamoja na Mheshimiwa Rhoda Kunchela, Mheshimiwa Mary Muro ameleta pia, Mheshimiwa Ritta Kabati, Mheshimiwa Lucia Mlowe na wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipende kutoa masikitiko yangu kwamba Kamati, especially hii yetu ya PAC na LAAC tunapewa muda mfupi sana wa kushughulikia hesabu hizi za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma pamoja na Serikali za Mitaa. Kwa uzoefu wenzetu wa Mabunge mengine hata ukienda Bunge la Uingereza unakuta kazi ya PAC ni ya kudumu, wana ofisi wanayofanyia kazi kwa muda kwa hiyo wanajipanga vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi muda tunaopewa ni mdogo sana. Wiki mbili uwe field, wiki moja uandae taarifa ulete hapa. Kwa hiyo, unakuta tija ni ndogo mno. Hatuwezi kuitendea haki kazi inayofanywa na CAG ya mashirika zaidi ya 200 halafu tukakaa hapa kwa nusu siku tunaongea taarifa za CAG za mashirika yote hayo pamoja na Serikali Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na ripoti zote na ripoti yoyote ambayo tumeileta na reaction za Waheshimiwa Wabunge na Mawaziri, niseme kwa kiwango kikubwa ripoti yetu imekubaliwa. Niwashukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina machache tu ya kuongea. Mheshimiwa Waziri wa Fedha ame-cover mambo ya Benki ya Azania, Pride na amesema yanashughulikiwa. Nina maeneo mawili ambayo nataka kweli tuyazungumze kwa kina kuhusu hoja ya Mlimani City ambayo pia Waziri wa Elimu amejaribu kuyaeleza na kuelezea jinsi ambayo Chuo Kikuu kinafaidika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kusema kwamba tunakubali vitu vidogo vidogo sana. Ukipewa shilingi bilioni mbili mwenzio akichukua bilioni 20 unaona ni sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema tumedhulumiwa sana katika project hii ya Mlimani City. Hoteli ya nyota tatu yenye vyumba 100 ilitakiwa iwe imeisha tangu mwaka 2006. Hebu hesabu ni pesa ngapi tumepoteza tangu hapo mpaka leo,?

Mheshimiwa Mwenyekiti, botanical garden ilitakiwa iishe mwaka 2006. Pesa kiasi gani tumepoteza ambazo kulikuwa kuwe na tourism pia mpaka leo bado tunasifu kwamba mwekezaji anatupa chochote, sisi tumekuwa watu wa chochote, inasikitisha sana. (Makofi)

Nipende kusema tuwe na uchungu wa nchi yetu. Huyu mwekezaji amesema kwamba wanamshinikiza aje akae waongee, hebu ona anashinikizwa! Mtu aliyekuja na dola 75 leo anashinikizwa ili aje aongee matatizo haya. Kama kweli ameweka pesa nyingi katika mradi huu kwa nini ashinikizwe? Tuna mambo mengi ya kujiuliza juu ya Mlimani City. Inawezekana hata huyo mwekezaji hayupo, ni watu wachache wamejichukulia jina akasema ni mzaliwa wa Botswana anaishi South Africa, lakini hata kwenye Kamati juzi hakuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mtu ameweka pesa yake nyingi hivi, structure zile asionekane kwa nini? Na bado tuichukulie juu juu. Mimi nasema kwa hili bado Kamati ilivyoshauri kwamba ufanyike ukaguzi wa kiuchunguzi, nasema Bunge lako liridhie ifanyike forensic and performance audit. Nasikitika na naona uchungu, naomba maji maana nasikitika jinsi ninavyoona Serikali inachukulia jambo hili kijuu juu, tunajaribu kuli-water down. Ardhi yote ile imechukuliwa, mikataba inaongezwa kidogo kidogo. Mkataba haujaisha umeongezwa, umesahihishwa na bado tunaongea, tunafurahi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri hata mtukufu Rais akisikia hili atasikitika sana na atasikitika jinsi ambavyo Watanzania tunatetea wawekezaji. Kamati tumejipinda bila overtime bila nini, tunafanya kazi. Hata tuliposema hatuna muda wa kutosha wa kufanyia kazi tukawaambia hapana leteni hivyo hivyo hiyo ripoti yenu. Bado tunakuja hapa Serikali inatetea kwamba mwekezaji anafanya vizuri katupa shilingi bilioni mbili, inatosha. Yeye akichukua hata shilingi bilioni 40, sisi tukipata shilingi bilioi mbili inatosha! Kweli katika awamu hii tunataka kwenda kwenye viwanja, tunataka kukusanya hela, tunaweza kutetea hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu angalia, nafikiri Waziri wa Viwanda na Biashara ataeleza jinsi ambavyo CBE imetoka mahali ambapo ilikuwa inapata ruzuku kutoka Serikalini sasa hivi inajitegemea na uangalie university mpaka sasa hivi inasaidiwa kujenga hostel, lakini tuna mradi ambao ungeweza ukajenga hostel hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu angalia wanafunzi wetu wanapelekwa Mabibo, wana-cross barabara wanaibiwa computer, wangetakiwa wafanye kazi mpaka usiku wakiwa kwenye lecture rooms’ lakini wanashindwa wanaondoka mapema maana hapo Ubungo kupita mpaka Mabibo wanaibiwa. Hostel inajengwa nje ya chuo wakati nafasi kubwa ilikuwa pale, eneo kule lile. Lile eneo ungetegemea ndiyo zijengwe hizi hostel tukaona tuwekeze, leo tunakuja na neno la kwamba tunapata bilioni mbili.

Waheshimiwa Wabunge, naomba nielezee hivi; hii hela tunayoambiwa Chuo Kikuu wanapata bilioni mbili, naombeni mnisikilize. Chuo Kikuu wameshindwa kufunga mahesabu yao tangu 2014. Kamati imehangaika nao, ilikuwa ifikie hatua mbaya sana, lakini sisemi mengi.

Mwaka 2014 hawajafunga hesabu, 2015/2016 hawajafunga hesabu na ni Chuo Kikuu Kikuu kinachofundisha wahasibu, Chuo Kikuu cha nchi chenye hadhi hiyo. Sasa hata hii hela tunaambiwa inaingia huko kutoka Mlimani City, tuna uhakika nayo gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba, tuna muda mfupi wa kuzungumzia mambo haya lakini forensic audit inavumbua mambo mengi sana. Tutataka wote waliosaini huu mkataba waonekane, wazungumze, huu mkataba waliousaini hivi ulikuwa na maana gani? Halafu ukisoma ule mkataba ulikuwa haufungamanishi ujenzi wa Mlimani City na barabara ya Sam Nujoma. TIC wanawaongezea kwamba barabara kweli ilichelewa, wakati ujenzi haukuwa na mahusiano yoyote na barabara ya Sam Nujoma. Kwa hiyo TIC nao wanaingia hapo, Serikali, inaingia kati inamuongezea huyu mwekezaji muda kila leo. Mkataba haujaisha, umeongezwa mwingine, hivi tuieleweje nchi hii? Kwa hiyo TIC wanahusika pia katika kuhujumu nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikataba imeongezwa kiaina aina, tena correspondences tunazoziona ni kwa e- mails; hebu fikiria mtu mwenye hela yake nyingi hivi, hapo South Africa anafanya kwa e-mail. Juzi tulimuita kwenye Kamati tunataka tumuone mwekezaji, hakuonekana! Katuma Meneja wake, tukimuuliza swali anasema ngoja nikapige simu nimuulize mwekezaji. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge hili tunadharauliwa vya kutosha. Hii Kamati imeundwa na ninyi, ni sehemu ya Bunge, auditor anafanya kazi kubwa, anaeleza matatizo halafu tuliokosa uzalendo tunakuja hapa tuna water down, hivi unatetea nini? Hivi kweli Rais Magufuli akiona hili atafurahi kweli kwamba tunatetea kitu hapa. Kwa kweli nasema personal interest tuziache. (Makofi)

Mimi nasema, hilo naomba, kuna mambo mengi sana Waheshimiwa Wabunge ambayo hatuna muda wa kuyaelezea kwenye hizi documents zote. Muda tunaopewa, napewa nusu saa kuelezea mambo yote yaliyofanyiwa audit, kwa nusu saa tu! Kweli naweza kufanya justice katika Idara hii? Hapo hapo mjue hatuna ofisi, kila mmoja anakaa na documents zake nyumbani, ukitafuta hili unachambua siku nzima, hujapata unalitafuta! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba kusema kwamba naomba tuombe ufanyike uchunguzi wa kitaalam tangu uanzishwe mradi huu waliosaini akina Profesa Luhanga, nafikiri wako hai na TIC ilivyoingia hapo ndani mpaka hapa tulipofika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI ameeleza mambo kwa ufasaha najua ALAT unaifanyia kazi kwa hiyo tutangojea matokeo yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuingie kwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Waziri wa Mambo ya Ndani amekuja hapa ameeleza mambo ya magari haya na mikataba ya NIDA, mikataba ya immigration. Nikiongelea hili la magari tumehangaika nalo tangu mwaka wa jana tukiomba mikataba tunapigwa danadana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati tunaomba mkataba ambao unaruhusu pesa zitumike ambazo hata kama ni deni nchi italipa! Tunapigwa dana dana. Kwa hiyo tunafanya kazi bila vitendea kazi vilivyokamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais kwa kwenda hapo bandarini hailizuii Bunge kuunda kamati ya uchunguzi ikafanye kazi yake. Ijulikane wazi kwamba kama Mheshimiwa Rais asingekwenda juzi ina maana wenzetu Wizara wangekuwa bado wanalifumbia macho. Hili tatizo hatukulileta jana au juzi, lililetwa tangu mwaka jana. Tumempa Afisa Masuuli nafasi mara tatu, akija anatupiga danadana mara apite huku, apite huku. Vile vitu tunavyomwambia, atuletee, documents hizi na hizi, hataki kuleta! Sasa hayo mambo yalikuwa wazi kwanini hakuleta ile mikataba? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi hatuzungumzii kwamba risasi ngapi ama bunduki ngapi ziliingizwa, tunazungumzia fedha za umma inakuwaje iwe ngumu kuleta taarifa kamili ili tulione hilo na kuangalia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri anaposema eti, wameunda Kamati zinachunguza, hivi kweli mtu anaweza kujichunguza mwenyewe? Kwani hayo magari yameletwa mwaka huu? Kwanini huo uchunguzi angoje mpaka Mheshimiwa Rais aende ndipo aunde uchunguzi? Kwa hiyo ni wazi kwamba Wizara ilikuwa imelifumbia macho na wanajua kilichokuwa kinatendeka. Sasa haya yote yanayozungumziwa hapa mimi nasema Bunge lako Tukufu liazimie kwamba ukaguzi wa kiuchunguzi ufanyike. Hatuwazuii wao kufanya kazi yao wanayotaka, wakitaka kufanya kazi yao waendelee, lakini Bunge lijiridhishe kama makinikia ilivyofanyika na hii ifanyike hivyo hivyo, ieleweke kwamba kuna nini hapa. Kwa vile kuna mambo mengi inaelekeza yamejificha, sasa sisi tutafanya cosmetic, lakini tunataka tuingie ndani ya mzizi huu wa tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipokuwa tunataka kuongea mambo ya NIDA tukaambiwa kwamba kesi iko Mahakamani. Kwa hiyo, hata mkataba hamuwezi kuletewa, zaidi ya hapo tukaambiwa hii iliyowekwa sasa hivi ni addendum, hamuwezi kuongelea addendum kama hamkuingia kwenye mkataba wenyewe. Sasa ni kama PAC tumefungwa miguu na mikono. Kila ukitaka kuangalia hiki unaambiwa hapana. Mambo ya Ndani ukitaka kuangalia hiki unaambiwa hapana. Lakini mbona Jeshi la Wananchi wa Tanzania tukiwaambia leteni hiki wanaleta? Jeshi wanaleta, haya ya Mambo ya Ndani kwa nini yanakuwa mazito? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaomba Bunge lako Tukufu liridhie kwamba kuna mambo ambayo yamefichika ambayo kama tukiyachukua juu juu kwa maneno ya kisiasa tutakuwa hatumsaidii Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli. Tunataka uchunguzi ili Mheshimiwa Rais yawe mezani kwake! Bunge likishajua ajue kuna nini mbivu na mbichi zijulikane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya passport, immigration; Kamati imezungumzia kwa undani jinsi pesa za visa zinavyopotea, kwamba mtu akikata visa Marekani au Ufaransa au Dubai au wapi haijulikani na upotevu wa pesa nyingi uko katika visa. Sasa leo tukiongelea tu passport, hata zikarembwa kiasi gani, zikawa nzuri kiasi gani wakati hakuna jinsi ya kujua kwamba pesa ya visa imeingia kiasi gani, tunafanya kazi gani?

Mmh, mambo mazito haya lazima ninywe maji.

Kwa hiyo tunaomba kwamba tuyaangalie haya mambo kwa undani. Nia ya kwenda kwenye uchumi wa viwanda inataka tuwe na hela. Kama tunataka kuwa na hela lazima tuangalie kule kote ambako pesa yetu inapotea. Sasa kama hatuingii kuangalia visa zinalipwaje, je, wale wanaoingilia airport pale wanalipa kiasi gani, zinawekwa wapi na zinawekwaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna data ya kuonesha kwamba kuna kusomeka mtu akichukua visa akiwa South Africa au akiwa Uarabuni wakikaa ofisini pale wanaona watu wangapi leo wameingia Tanzania na wamelipa kiasi gani. kwa hiyo tusiremberembe mambo hapa kwamba passport nzuri sana, hata gauni yangu hii nzuri. (Makofi/kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama hatuzungumzii mambo ya msingi tukizungumzia vitu vidogo vidogo kwamba hiki kizuri, hii hata kama ingekuwa nzuri kiasi gani mbona hata Marekani wanaweza kukakatalia usiingie kule kwenye nchi yao, hata kama ingekuwa nzuri kiasi gani. (Makofi)

Kwa hiyo tuangalie mambo kwa undani, tunafanya kwa awamu, awamu ingeanzia basi kwenye immigration ili tujue pesa imeingia kiasi gani. Ili tujue basi tutengeneze passport nzuri maana tuna hela, tunaanza vice versa kwa nini? Ninaomba tuangalie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongea kwa juu juu sana mambo mengi maana tukisema tuingie ndani kwa muda ulionipa nitakuwa siwezi kumaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie tu utata ambao ulitokea kati ya Wajumbe wangu wa Kamati ambayo mmoja anasema heka moja ilinunuliwa milioni 800 mwingine anasema sio hivyo. Ni kwamba wanaweza hawa watu wakawa wanaongea kitu kimoja isipokuwa mmoja anaongea land for equity mwingine anaongelea cash money. Hili jambo ukitaka kulieleza sasa hivi sitaweza kulizungumzia maana la kihasibu zaidi, lakini itoshe kusema kwamba…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kaboyoka tafadhali kidogo naongeza dakika 30 kwa mujibu wa Kanuni ya 28(5) endelea.

MHE. NEGHENJWA L. KABOYOKA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE HESABU ZA SERIKALI:
Mheshimiwa Mwenyekiti,ahsante sana. Hapo awali huu mradi wa mradi wa dege ulikuwa mwekezaji alisema ana hekari 20,000 ambazo ndio alikuwa ameweka katika mradi. Baada ya auditor kufanya kazi akaonekana ana heka 300 tu. Kwa hiyo si hekari 20,000 ana heka 300; kwa hiyo pungufu ya hekari 19,700. Sasa hawa watu wawili ni wahasibu, mmoja kachukua hesabu za mwekezaji alisema nini mmoja akachukua land for equity kwamba ile land ilipewa thamani ya kiasi gani, lakini wote walikuwa wanaongelea jambo moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda tu itoshe tu kusema mradi huu umekuwa na utata, mradi huu ripoti yake Kamati Ndogo walienda kuungalia kwa undani, ukaletwa ripoti kwenye Kamati nzima ya PAC tukaupitia. Uliangaliwa kwa kina na ukatengenezwa mapendekezo yake na kama alivyosema Mheshimiwa Mhagama ripoti ikapelekwa kwa Mheshimiwa Spika. Ripoti ilipelekwa tangu Februari, 2017. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme kwamba hii ripoti imezungumzia mambo mengi ambayo siwezi kuyasema kwa muda huu mfupi na ndio maana Kamati ikasema, Mheshimiwa Spika ailete ile ripoti iangaliwe ili Bunge liweze kutoa maazimio. Kwa mantiki hiyo na tunajua kwamba Mheshimiwa Spika hayuko nchini, kwa hiyo tukashindwa kwamba turudie tena mapendekezo yale yale na ina maana tunge-rewrite ile ile ambayo tayari iko kule kwake tukaona kwamba Kamati tutakuwa tunajichanganya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nawaombeni Waheshimiwa Wabunge tuvute subira, Mheshimiwa Spika atarudi, hii ripoti itaangaliwa kwamba inasemaje. Kwa hiyo, tumeshindwa sasa hivi tusemeje isipokuwa tumesisitiza tu kwamba yale mapendekezo kamati iliyotoa kwenye ripoti ile yafanyiwe kazi na hapo yatakapoletwa Waheshimiwa Wabunge tutaweza wote kuiangalia na ku-debate.

Kwa hiyo niseme kwa kifupi kwamba kwa muda ulionipa niliogopa nisichanganyikiwe kama asubuhi ambayo nilikuwa na mengi ya kuongea na sikuweza kuhitimisha sasa nitajipeleka kwenye kidogo ili niweze kuzungumza yale machache ambayo ningeweza kuzungumza pamoja na kwamba kuna mengi ambayo ningeweza kuzungumza lakini itoshe na naona umeshanipigia kengele nikushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Wabunge wengine waliochangia ambao kwa kweli haikuwa rahisi kuwataja wote kwa sababu ya muda nashukuru kwamba mmenisikiliza Waheshimiwa Wabunge hivyo basi Kamati inashauri Bunge lako kukubaliana na mapendekezo ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kauwa maazimio ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnataka nirudie au?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hivyo basi Kamati inalishauri Bunge lako Tukufu kukubaliana na mapendekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuwa Maazimio ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.