Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Silafu Jumbe Maufi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuweza kutoa mchango wangu kiasi katika suala zima la bajeti hii iliyowasilishwa asubuhi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kutoa shukurani za dhati na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya. Vile vile nitakuwa ni mnyimi wa fadhila kama nisipompongeza Waziri Mkuu na Baraza lake la Mawaziri kwa kazi wanayoifanya, nasema big up. Pia napenda kutoa shukrani za dhati kwa akinamama wa Mkoa wa Rukwa walioniwezesha kuingia katika jengo hili na kuweza kuwazungumzia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa shukrani za dhati za Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi katika kutambua na kujipanga na kuona kwamba wanahitaji kufanya nini katika kukinga na kuyaboresha mazingira ya nchi yetu ili iweze kuwa katika maendeleo ya wananchi kwa ujumla, nawapongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyeketi, napenda kuzungumzia suala la mazingira na hasa katika Mkoa wetu wa Rukwa. Mkoa wa Rukwa kwa maana ya jina la Mkoa wa Rukwa imetokana na Ziwa Rukwa tulilonalo. Ziwa hili linaanza kupoteza kina cha Ziwa lile kutokana na maporomoko ya mito inayotoka milimani kuanzia Mlima Liambaliamfipa mpaka milima inayozunguka ziwa lile; kuna mito mingi mno ambayo inatiririka kiasi cha kuchukua udongo na kujaza katika lile ziwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kufahamu Wizara imejipanga vipi katika kulinusuru ziwa hili lisiweze kupotea na Mkoa wetu wa Rukwa ukakosa kupata jina. Naomba Serikali ifikirie namna ya kuweza kuyakinga haya maji kwa namna moja au nyingine yakaweza kutusaidia katika suala zima la umwagiliaji au Serikali iweze kukinga maji haya wakayaweka mahali ambapo wanaweza wakafanya utaratibu wa kuyasambaza na kuya-treat, hatimaye kuyasambaza kwa wananchi wetu na kupata maji safi na salama. Kwa kufanya hivyo, itakuwa imewasaidia akinamama wangu wa sehemu ya Bonde la Rukwa kupata maji kwa ukaribu zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo linapelekea hili Ziwa letu kuwa na kina kifupi ni mifugo mingi iliyoko katika Bonde la Rukwa. Bonde la Rukwa lina mifugo mingi na mifugo mingine ni kwamba wakati wa mnada wa Namanyere kupeleka ng‟ombe Mbeya ni lazima watapita barabara ya bondeni na barabara ile ni barabara ya vumbi inayotoka Nyamanyere hadi Kibaoni, Kibaoni mpaka Mtowisa, Mtowisa –Ilemba, Ilemba - Kilyamatundu hadi kufikia Kipeta na hatimaye kuondoka kuingia Chunya - Mbeya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ng‟ombe wale wanaweka tifutifu, wakati wa mvua, lile tifutifu ambalo ni udongo unachukuliwa na maji na kupelekwa katika Ziwa Rukwa. Sasa Wizara ina mpango gani wa kushauriana na Wizara husika kuhakikisha barabara ile ya kutoka kibaoni hadi Kilyamatundu kuelekea Kamsamba iwe ni ya lami badala ya kuwa ya vumbi ili isiendelee kujaza udongo katika ziwa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uharibifu mzima wa mazingira sehemu yetu ile ya Rukwa ni kutokana na akinamama kuingia mle na kukata miti na kuitumia kama nishati. Sasa tunaomba nishati mbadala kwa lile Bonde la Rukwa kwa kuhakikisha kwamba umeme unapatikana. Umeme ukipatikana mama zangu watapata nishati mbadala na hatimaye ile miti itaweza kukua na kuhifadhi mazingira yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo naweza kuzungumza katika suala zima la mazingira ni suala zima la utafiti. Karibu Wizara zote ambazo nimewahi kuzisikia na ninazoendelea kuzisikia, daima huwa wanaweka utafiti, tathmini, katika sehemu ambazo kwamba zimekwisha piga hatua. Kwa nini wasifanye utafiti na wakafanya tathmini ya maendeleo ya jambo katika Nyanda za Juu Kusini ambapo tuko pembezoni tumechelewa kwa kila kitu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa utafiti uelekee upande wa Nyanda za Juu Kusini ili na sisi tuwe makini, tuweze kuelewa nini elimu ya mazingira, tunatakiwa kufanya nini kuhusiana na mazingira yetu na sisi tusije tukawa jangwa kama mikoa mingine ambayo imetajwa ndani ya taarifa hii ya Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makadirio yaliyokuwa yamekadiriwa katika Wizara hii hayatoshelezi mahitaji. Hayatoshelezi mahitaji kwa nini? Kwa sababu suala la mazingira ni suala pevu na ni suala pana ambalo kila Wizara ikitamkwa humu ndani, maendeleo yake huhitaji mazingira yake yawe ni bora zaidi. Sasa suala la mazingira ni suala pana ambalo linahitaji kuwa na bajeti kubwa ya kutosha. Mheshimiwa Waziri Januari sitaona ajabu kabla ya mwisho wa mwaka ukaomba tukuongezee bajeti ya utekelezaji wako. Sasa naomba, Serikali ione uwezekano wa kuiboresha hii bajeti ili iongezeke, tuweze kupata uhakika wa kuweza kuiendeleza vizuri Wizara yetu hii ya Mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Wizara hii ya Mazingira katika wilaya zetu na mikoa yetu hawa watu hawaonekani kutokana na kazi nzito iliyoko ya Mazingira. Nawaomba tuongezewe idadi ya watumishi ili watumishi hao waweze kujigawa kuweza kutoa elimu kwa wananchi wetu kuhusu suala zima la mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile na hawa wataalam, ni vema wakatengewa fungu la kutosha kupata elimu ndani na nje ya nchi ili waweze kwenda na nyakati zinavyoweza kusomeka katika suala zima la mabadiliko ya tabianchi katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitapenda kupewa taarifa rasmi na Mheshimiwa Waziri mhusika hasa kuhusu kuhakikisha kwamba Ziwa letu la Rukwa linakingwa na linaweza kuboreshwa na hatimaye kuwa ziwa zuri na kuweza kuimarika, kwa sababu Ziwa Rukwa lina mamba wengi mno. Suala la Mamba pia ni suala la Maliasili, kwa hiyo tunawaomba muwalinde mamba hawa wasiweze kupotea ndani ya Ziwa letu la Rukwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, namwomba Mheshimiwa Waziri mhusika aweze kuniambia ni mikakati ipi ambayo imewekwa au anayotarajia kuifanya kuboresha mazingira yanayoanza kupotea katika Nyanda ya Juu Kusini na hususani Mkoa wetu wa Rukwa ndani ya Ziwa letu la Rukwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.