Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Saul Henry Amon

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rungwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. SAUL H. AMON: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Wizara ya Fedha. Kwanza nimshukuru Waziri wa Fedha kwa kuwasilisha bajeti yake, mimi nina mambo mawili makubwa. Wakati wa kukusanya kodi, kodi ni sawa na biashara nyingine yoyote lakini hapa kuna vikwazo ambavyo wafanyabiashara wengi tunavipata na kama Waziri hajalisikia hilo atume timu yake kwa wafanyabiashara, hasa wanaoingiza mizigo kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kuna huu mfumo wa TBS na tukiangalia kwamba nchi ya Tanzania sio nchi yenye viwanda kwa kiasi kikubwa na wafanyabiashara wa Tanzania sio wakubwa wa kila mmoja kwenda kutafuta kiwanda chake cha kuleta mizigo. TBS kuna tatizo, hasa la ile faini ya asilimia 15 ya invoice value ya mzigo anapoleta hapa Tanzania. Hilo ni tatizo kubwa sana ambalo naomba Serikali kwa kupitia Wizara ya Fedha iliangalie upya ni namna gani wanafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kuna Wizara mbili, kuna Wizara ya Afya kupitia TFDA kwa mambo ya vyakula na dawa na TBS ambayo inafanya sehemu zote. Hata hivyo, utaratibu wa TFDA ni mzuri, unaeleweka, pamoja na kwamba ni ghali, unakwenda unasajili bidhaa zako hapa Tanzania na wanakupa certificate. Ukishapewa mara moja huna usumbufu tena baada ya hapo, kwa hiyo TFDA hawana matatizo ukishasajili bidhaa zako, lakini TBS tatizo lake ambalo linawafanya Watanzania wengi wasiweze kuingiza mizigo, Watanzania wengi wapite porini ndiyo maana unasikia, Mheshimiwa Bashe ameongea hapa kwamba watu wanapita Kenya, wanapita Kenya kwa sababu ya kuikimbia TBS, wanaingizaje, haijulikani.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, TBS wangechukua mfumo wa TFDA nina uhakika kwamba ingepunguza usumbufu mkubwa sana, kwamba mimi nilete bidhaa zangu, TBS wazikague kwa sababu viwanda vinavyotengeneza mizigo inayopita TFDA ndiyo hivyohivyo vinavyotengeneza kupita TBS, lakini TBS kila unapoingiza mzigo unakuwa na certificate yake. TFDA wakikusajili utaisajili tena hiyo mizigo yako baada ya miaka miwili, unakuta usumbufu wa TFDA unakuwa haupo lakini TFDA anakwambia chakula ingiza, unaingiza TBS anakwambia hujasajili na kama hujasajili TBS ulipe asilimia 15 ya invoice value. Kwa kweli imewafanya wafanyabiashara wengi sana wawe na manung’uniko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri na timu yake awaulize wafanyabiashara nini kikwazo kikubwa cha biashara. Kama anavyojua tunavyoingiza mizigo ndivyo tunavyoweza kuuzia nchi nyingine za jirani, na ukiuzia nchi nyingine za jirani tutapata faida si moja tu kwa ajili ya kuingiza mizigo, kwanza wanakuja kuchukua mzigo, wanakuja wanalala, wanatumia usafiri wa nchi wa ndani wa kwetu na mambo mengine, akina mama lishe wanapata vyakula, wanapata hela. Kwa hiyo kupitia TBS kwa kweli hilo ni tatizo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba Serikali iliangalie hilo, kwa nini kazi za TFDA zisiwe za kwake. Tumepita nchi nyingi, ukiangalia Nigeria, Marekani na kwingineko, ukiambiwa kwamba hawa wanashughulika na mambo ya vyakula na dawa ni Wizara nyingine na ambao wanashughulika na mambo ya viwango ni Wizara nyingine na viwango vingekwenda kwa viwango na TFDA wangeendelea na kazi yao ya kukagua kwamba hivi vyakula na madawa viko salama kwa mlaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini mapato ya nchi yataongezeka, watu watapungua. Kwa sababu ukiangalia TRA hakuna usumbufu kabisa kama ilivyokuwa zamani, ukiangalia bandarini hakuna usumbufu kama ilivyokuwa zamani lakini ukifika unakwama, kwa sababu sisi wafanyabiashara wa Tanzania wengi ni wadogo, ni watu ambao hatuna mitaji mikubwa, tunavyoenda kununua mizigo iwe ni Ulaya, iwe ni Marekani, iwe ni China au Dubai, tunachanganya, hivyo huwezi kupata na usumbufu wake ni mkubwa mno. Wakati unanunua mzigo utachukua zaidi ya wiki sita ili kupata certificate ya TBS. Hilo naomba waliangalie walipe umuhimu wa hali ya juu, watu wanatoroka na mizigo kupita sehemu nyingine kwa sababu hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hapo Mheshimiwa Waziri amenielewa na kama nilivyomwambia, sehemu nyingine zake zote ziko sawasawa; TRA ambako watu walikuwa wanaogopa pako sawasawa, vitu vinakwenda sawasawa wala ndani hatuingii. Ukienda TFDA unakwenda na certificates zako nimeleta mzigo huu, hatusumbuliwi, unapewa invoice. Hata hivyo, ikifika sasa, kama ninavyomwambia, ni kweli nikikaguliwa nitakwenda kukaguliwa wiki sita, badala ya kuondoka siku tatu nitakwenda kukaa zaidi ya miezi miwili nikisubiria ukaguzi na mizigo, lakini kibaya zaidi, kwa nini hawa TBS ambao wana jukumu wasichukue kwamba wewe unachukua kiwanda gani, mimi nitasema nauza vipodozi nachukua Procter and Gamble, basi lete hivyo vitu tuvipime kama viko sawasawa, au nimechukua Unilever, tuvipime viko sawasawa, wanipe certificate.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatukatai kuvipima kama viko salama, lakini na wenyewe watupe certificate ili tusiwe tunasumbuka kila mara tunapoingiza mizigo. Huu usumbufu Mheshimiwa Waziri ataona sasa hivi umetengeneza monopoly, maana ukizungumza atakuwa analeta mtu mmoja, ukimwambia huyu ndio anayeleta chuma basi ataleta huyo huyo kwa sababu ndiye aliye na nafasi na access ya kwenda kwenye kiwanda hicho kinachohusika na kumpimia mizigo yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni hilo ambalo watu wengi wameliongelea, nadhani ni la kuongezea tu, kuhusu hizo milioni 50. Kwa kweli ni matatizo, Waziri akakae na timu yake, milioni 50 watu tuliwaahidi na zilikuwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na kila tukienda kwenye mikutano tunaulizwa kama vile tuliwakopa. Kwa hiyo, wakae wakijua kwamba ahadi ni deni, hilo waliangalie kwa uzuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo wameliongelea watu na mimi nasisitiza tu, kwamba Serikali iangalie kwamba kuzichukua zile hela waangalie namna ya kuzirudisha na namna ya kuzifuatilia lakini zirudi benki tuendelee kukopa. Mambo yetu yamekwama, benki wanakataa kutupa hela, benki kama CRDB ambayo walikuwa wanaweza kukupa mara moja, hawana hela. Tafuteni utaratibu, zirudisheni kule kama na ninyi mnataka riba basi chukueni riba kutoka benki ili tuendelee kukopeshwa na ndiyo uchumi wenyewe, hakuna uchumi mwingine, kama wananchi hawana hela utapata wapi hiyo kodi, maana hawanunui, utapata wapi hiyo kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli hayo ndiyo niliyokuwa nayo. Ahsante kwa kunipa nafasi hii kutoa mchango huu.