Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018

Hon. Philipo Augustino Mulugo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Songwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ili kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa hatua zote alizozichukua kuhusu masuala ya mchanga. Nakubaliana naye kabisa kwa asilimia 100 na tunasubiria hiyo Kamati nyingine ambayo inashughulika na masuala ya kiuchumi na sheria tuje tuone na yenyewe itasema nini, halafu baada ya hapo twende mbele. Hata hivyo, kwa hatua mpaka hivi sasa tunavyosema nakubali kwa asilimia 100 kwamba Mheshimiwa Rais ni mzalendo sana katika nchi hii na anavaa kabisa uzalendo katika nchi hii kwa ajili ya kulitumikia Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nirudi kwenye masuala ya Jimbo langu la Songwe. Daima nikiwa nachangia hapa huwa nasema miaka yote, kwamba; sasa sijui nitumie neno Serikali kwa ujumla ama niseme tu Wizara hii; Wizara ya Nishati na Madini Jimbo la Songwe naona kama vile inapendelea. Mheshimiwa Mwijage utakumbuka ulipokuwa Naibu Waziri wa Wizara hii alifika jimboni kwangu, Kata ya Kanga na aliniahidi kunipa umeme na hivi nimwambie Kata ya Kanga umeme unawake kwa initiatives zako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Jimbo la Songwe lina kata 18 na hivi ninavyosema kata sita angalau zina umeme na kata 12 hazina umeme. Hata hivyo, Waheshimiwa Mawaziri hawa wanasahau kwamba tulikuwa Mkoa wa Mbeya zamani, sasa tuko Mkoa wa Songwe. Kule kwa Mheshimiwa Mwambalaswa vijiji vingi vina umeme, kule Mbozi vijiji vingi vina umeme, kule Momba kwa Mheshimiwa Silinde vijiji vingi vina umeme, kasoro Jimbo la Songwe, kuna nini? Mheshimiwa Dkt. Kalemani, nimekwenda mara nyingi sana ofisini kwake, nimekwenda kwenye dawati lake kumlalamikia, kwa nini Jimbo la Songwe hawatuletei umeme? Tumekosa nini mbele za Mungu?

Mheshimiwa Naibu Spika, wiki iliyopita nilichangia hapa kwenye Wizara ya Elimu, nikasema kwamba wenzetu kule, sisi wilaya mpya hatuna chochote, hatuna majengo ya wilaya, hatuna nyumba za watumishi, hatuna barabara ya lami, hatuna VETA, hatuna maji makao makuu ya wilaya, yaani kila kitu hatuna, hata umeme vijijini hatuna, yaani hata umeme tu tukose? Kwa kweli kesho nitakuwa mkali sana kwenye kushika shilingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sijawahi kuwa mkali kwenye hilo, lakini kesho, Mheshimiwa Mwijage, nitashika shilingi yake, kwa sababu yeye ameshawahi kufika kwenye jimbo langu, anawafahamu wananchi wangu na tulimpa na ng’ombe na mbuzi siku ile Mheshimiwa Mwijage, tukamweka akawa Mtemi kwa sababu alifanya jambo zuri sana na alichangia na maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo Kata za Gua, Udinde, Kapalala, Mbangala, Manda, Namkukwe na Mpona na vijiji zaidi ya 30, hatuna umeme. Nimekwenda pale REA Makao Makuu kulalamika lakini mpaka leo umeme hakuna, kuna nini Songwe na ni mkoa mpya na ni wilaya mpya? Jamani naomba na sisi watufikirie tuweze kula keki ya Taifa na sisi, wanatunyanyasa mno, hatuna chochote, nalalamika kila siku hapa. Mwenzenu sina barabara, nimesema hapa, sina chochote, basi hata umeme wa REA. Naomba, Mheshimiwa Dkt. Kalemani, nimemlalamikia sana kila siku nikija anasema atanipa mkandarasi, siwaoni hao wakandarasi wa Songwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mtu wamemweka kule Mbeya anayesimamia masuala ya nishati ya umeme Mkoa wa Songwe, hapatikani na Mheshimiwa Naibu Waziri, nimemlalamikia huyo mtu kwa nini wasimuwajibishe. Hataki kushirikiana na Wabunge wa Songwe masuala ya umeme na anamfahamu na nilimpa na namba zake za simu, please, naombeni umeme. Safari hii na mimi sasa nitakuwa mkali, nimekuwa mpole mno, nitakuwa mkali sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Shanta Gold Mining ambao kule kwetu wanajiita New Luika Gold Mining; kwa kweli watu wa madini hawa; ndiyo maana nimempongeza na Mheshimiwa Rais; watu hawa ni waongo sana. Mwaka wa jana amekuja Mheshimiwa Profesa Muhongo kwenye jimbo langu, tumekwenda kwenye Kijiji cha Saza, tumekubaliana na Mheshimiwa Dkt. Kalemani anajua, watu wa Kijiji cha Saza wamelalamika, kuna eneo la wachimbaji wadogo wadogo lakini watu wa Shanta wameliingilia eneo lile mpaka kwenye nyumba za wananchi, makaburi, miembe, miti, kila kitu kimekwenda Shanta, kwa nini.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kumlalamikia Mheshimiwa Profesa Muhongo, wamekuja na Mheshimiwa Kandoro aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya mwaka jana wamefika pale, tumekaa vikao siku sita, tumehukumu kesi na watu wa Shanta wakashindwa mbele ya wanakijiji, mbele ya mkutano wa hadhara na TBC walionesha na mimi nilikuwepo pale. Hata hivyo, Mheshimiwa Waziri alitoa ruling pale pale, kwamba eneo hili tuwape wananchi, lakini mpaka leo sina barua inayowaonesha wananchi kwamba wamepata lile eneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Kalemani na yeye nakumbuka nilimwambia, naomba kesho aniambie, baada ya Waziri kutamka kwamba lile eneo ni la wananchi na wamuulize Mheshimiwa Profesa Muhongo popote huko alipo aseme baada ya pale nini kilichoendelea, nakwenda ofisini kila siku anasema subiri. Hawa watu wa Shanta wana nini? Wametoa nini huko?

Mheshimiwa Naibu Spika, haya, juzi nilikuwa Jimboni, nimeuliza swali jana hapa kwa Mheshimiwa Waziri wa Maji, nasema hivi; hawa watu wa Shanta hawa tena wamefunga tayari mto. Mto unatoka Rwika unakwenda Mbangala mpaka Maleza wamefunga kwa ajili ya wananchi wasipate maji, kwa nini wanatuonea hivi jamani? Vijana wa Mbangala mpaka wakataka kufanya fujo lakini Polisi wakawaweka ndani, tunawaonea wananchi bure. Hawa watu wa madini ni waongo sana na mimi ndio maana sielewani nao kwa sababu ya hiyo toka mwaka jana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu nilipomwambia Mheshimiwa Profesa Muhongo amekuja pale sasa na hilo eneo tumewanyang’anya, basi leo ni chuki ya Mbunge na wananchi hatuelewani kule Songwe. Naomba tafadhali sana, maji yafunguliwe la sivyo mimi nitakwenda jimboni kuwachukua watu wa Saza na kuwachukua watu wa Mbangala tukashirikiane tuchukue majembe na shoka tukatoboe lile bwawa ili na mimi mje mnipige, mnifunge, haiwezekani kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikataba wameweka na kijiji lakini ni mikataba feki; na wamesema wao wenyewe kwamba; mikataba tumeweka, hamuwezi kutufanya chochote kwa sababu sisi Serikali inatulinda. Tafadhali sana Mheshimiwa Mwijage, Mheshimiwa Dkt. Kalemani, nawaomba suala hili walitamkie kesho watu wa Ashanti watoboe lile bwawa na wananchi wangu waweze kupata maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo wala siwezi kuchangia mambo mengi sana, naomba tupate...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzunguzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.