Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Zaynab Matitu Vulu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niwe miongoni mwa wale wanaochangia hotuba hii ya bajeti ya awamu ya pili katika kipindi hiki cha Awamu ya Tano ya Mheshimiwa Rais Dokta John Pombe Magufuli, bajeti ambayo imeonesha dira na msisimko wa hali ya juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa juhudi anazozifanya kwa Watanzania kwa maendeleo ambayo anayaona yakiweza kufanikiwa basi Watanzania watakuwa wamegomboka na wamepiga hatua kuondokana na umaskini. Mheshimiwa Rais amelenga kuhakikisha pale palipokuwa na mianya ya mchwa anatia dawa wale mchwa wote waweze kufa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi sote ni mashahidi na sio tu humu ndani tu tunaompongeza Mheshimiwa Rais, Dokta John Pombe Magufuli hata Rais wa Awamu ya Pili, Mheshimiwa Alhaj Ali Hassan Mwinyi amesema hadharani kazi anayoifanya Rais Magufuli ni kazi ambayo imefanywa na wao kwa miaka 30 iliyopita. Kwa hiyo, sisi sote tuna kila sababu ya kuunga mkono juhudi zake.

Mheshimiwa Spika, nikupongeze na wewe, jana umetuwakilisha vizuri sana, sisi tuko na wewe bega kwa bega, mguu kwa mguu, mbele kwa mbele hadi tujue mwisho wa wale ambao wanataka kuharibu na kudhulumu uchumi wa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waziri wa Fedha na Mipango na Naibu wake wametuletea bajeti. Bajeti hii sisi tunaifurahia, wengine wanafurahia ndani ya mioyo lakini usoni hawataki kusema ukweli na huo ni ugonjwa. Kama wamekasirika waweke magari yao pembeni, kama wamekasirika yale yote ambayo yamependekezwa wayakatae hadharani kwa vitendo sio kwa maneno ya siasa ya humu ndani.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais amesema yeye tumpe ushirikiano na tumwombee dua, sisi wengine tuko kwenye Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, dua zetu, sala zetu, ibada zetu tumemwongezea yeye na tunamuombea na tunawaombea Watanzania wote kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukija kwenye kulipia mafuta nyongeza ile ya Sh.40/=, wataalam wa masuala ya uendeshaji wamesema hakuna hasara yoyote inayopatikana, ni faida tupu. Kwa hiyo, hii itasaidia pesa hizo zikipatikana si vibaya kama zitapelekwa zikatumike kwa wananchi kwa ajili ya maendeleo ya maji, umeme na mambo mengine. Pia hii imeondoa mzigo, si kwamba kutakuwa na nauli kubwa, mbona petroli inapopunguzwa wamesema hapa wanaofanya hizo biashara, hakuna hasara yoyote, tusitie maneno chumvi kabla mchuzi haujaiva. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende kwenye suala la utalii. Utalii ni sehemu ambayo ina nafasi kubwa sana. Kuna aina nyingi za utalii, niombe wanaohusika Kijiji cha Makumbusho kiboreshwe tuweze kupata pesa zaidi na tuangalie maeneo mengine ambayo yatatuletea tija kwa maana ya kuingiza pesa. Utalii utoke Kaskazini uweze kwenda Kusini, uje Pwani, Mafia tuna utalii wa kutosha, Kisarawe tuna utalii wa kutosha kuna mapango wanakaa popo mule ndani kinyesi cha popo kikichukuliwa kinaweza kikatoa nishati ya aina fulani, niombe hilo nalo lizingatiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukija kwenye kitabu cha bajeti, nimefarijika sana na si mimi tu nina jirani yangu Mbunge mmoja yeye pale Dar es Salaam maeneo yake mengi wanakaa watu wanaofuga kuku, sasa akiwa analipinga hili nitamshangaa sana tena nitakwenda hata kuwaambia hao watu wa huko. Sitaki kumtaja yeye mwenyewe ameshajijua. Ufugaji sasa hivi umepunguzwa tozo, kwenye mayai ya kutotolea vifaranga, kwenye vifaranga vyenyewe, kwenye bei ya vyakula, sasa unataka nini binadamu wewe zaidi ya hayo? Huoni kwamba hiyo ni tija kwa wapigakura wako? Jirani yangu, nikisema jirani yangu anajijua, hebu simama ulipongeze basi hata hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongeze lingine kwenye ushuru wa mazao, hili jambo limetusaidia sana hasa sisi ambao maeneo makubwa sana ya majimbo yetu ni sehemu za wakulima. Mkulima mdogo ndiye aliyekuwa anaumia sana, anatozwa ushuru wa mazao lakini leo akipakia gari lake halizidi tani moja, hadaiwi senti tano. Hii inatoa unafuu wa maisha, inampa nafasi mkulima aweze kuuza alichonacho, apate pesa ajiongezee katika kujiendeleza yeye, watoto wake, familia yake hali kadhalika na kujijenga katika mazingira ya kuondokana na umaskini. Sasa leo basi hata hilo ndugu zangu mnalikataa, mbona inakuwa mushkeli kidogo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi sitaki kusema hawana jipya, wanayo mapya lakini wajipange, wazungumze yale ya uhalisia wa maisha. Hakuna eneo katika jimbo ambalo halina wajasiriamali, leo wajasiriamali watapewa vitambulisho, watatafutiwa maeneo ya kufanyia biashara zao na sisi ndiyo wasemaji wao, leo hii wewe hata hilo ukilipinga, wewe mtu wa aina gani? Kilimo ukikatae, ushuru wa mazao uukatae, license ukatae!

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dokta Magufuli katuletea neema, anataka kumtua mzigo mwananchi wa kijijini. Hii Sh.40/= ikienda kijijini wanawake watapunguziwa mzigo wa kubeba maji kichwani, watapunguziwa muda wa kufanya kazi za kutafuta maji watarudi watafanya kazi zao za kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Waziri na niombe Wabunge tusimame kwa pamoja tuhakikishe kwamba bajeti hii inapita, mambo mazuri yanayoletwa na Mheshimiwa Rais yetu yanatimizwa, asilimia inayotakiwa kwa kila eneo ipelekwe lakini maendeleo yabaki palepale kwamba Watanzania tupate faraja, tuondokane na ukubwa wa matatizo ya kujiendesha kimaisha.

Mheshimiwa Spika, sisi tutaungana na wewe kwa yale yote ambayo umeyaahidi jana mbele ya Rais, Mheshimiwa Dokta John Pombe Magufuli kuhusu makinikia na mazagazaga mengine yote ambayo yamezungumzwa tutakuwa pamoja na wewe, tutashirikiana na wewe. Nina
uhakika kwenye suala la tozo ya maji, wewe na Wabunge wenzangu tutasimama pamoja kuhakikisha tunatua ndoo ya mwanamke kichwani, tunahakikisha kwamba mwanamke atakuwa na nafasi ya kutosha katika kufanya kazi zake badala ya kwenda kukaa saa sita, saba anasubiri maji ayafikishe nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja.