Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. OMARY M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii jioni ya leo niweze kusema machache juu ya Hotuba ya Wizara ya Ardhi. Nami nitakuwa ni mnyimi wa fadhila kama sitamshukuru Waziri wa Ardhi, Naibu Waziri pamoja na timu nzima ya Wizara ya Ardhi kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba hii nitakuwa na maneno machache sana lakini yatalenga kwenye ushauri zaidi. Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Ardhi ikiwezekana alete sheria hapa ambayo itakayozuia maeneo ya kilimo yasitumike kwa ajili ya makazi. Jambo hili tumeliona, kila anayesimama hapa analalamika juu ya migogoro ya ardhi, hakuna kilimo bila mipango bora, kwa sababu tumeruhusu ardhi yenye rutuba tunaanza kujenga. Naona hili haliwezi kufanyiwa kazi bila kuleta sheria hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Ardhi kwamba Bunge litunge sheria ya namna ya kuzuia wananchi wetu wasiuze ardhi; isiwe mtu ana heka, kumi ishirini au zaidi anaamua kuuza tu kwa sababu ya shida yake. Ni kwa nini nasema haya? Hii ni kwa sababu migogoro mingi tunayoiona ya wakulima na wafugaji imesababishwa na wananchi kuuza maeneo yao. Nadhani Mheshimiwa Waziri analo jukumu hilo kuangalia, kupitia kuona ni namna gani tunaweza kupunguza migogoro kwa namna hii ya kuzuia wananchi kutouza ardhi ovyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeliona hili kwa sababu mimi natoka Jimbo la Kilindi ambako kuna migogoro mingi sana. Mtu mwenye pesa yake anatoka Arusha au Manyara huko anauza heka moja anakuja kununua heka 500 kule Kilindi. Sasa hawa wananchi ambao hawana uwezo, mafukara wanauza ardhi wanabakia kuwa vibarua katika ardhi hiyo. Kwa hiyo ili kulizuia hili naomba Mheshimiwa Waziri wa Ardhi alichukue hili aweze kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kuchangia ni juu ya migogoro ya wafugaji na wakulima. Kila aliyesimama hapa anazungumzia migogoro ya wafugaji na wakulima. Katika Jimbo langu la Kilindi nina wafugaji na wakulima wengi sana lakini najiuliza tatizo ni nini? Suluhisho
la kudumu, Mheshimiwa Waziri, ni kupima ardhi. Tupime ardhi hii ili wafugaji wajue maeneo yao ni yapi, wakulima maeneo yao ni yapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini najiuliza zaidi, hivi mimi Wilaya ya Kilindi ambayo ina vijiji 102 tutaweza kuvipima leo kwa muda mfupi hivi? Sasa kama mlianza Morogoro, nadhani muanze na maeneo ambayo yana migogoro ya ardhi Mheshimiwa Waziri anajua, Kilindi ni miongoni mwa maeneo ambayo yana migogoro mikubwa sana ya wafugaji na wakulima, nimwombe baada ya Morogoro aje Kilindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Ardhi juu ya mgogoro wa Wilaya za Kilindi na Kiteto ambao umedumu kwa takribani miaka 30. Mheshimiwa Waziri wa Ardhi alikuja mpakani pale, yeye na Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Waziri wa TAMISEMI. Nimshukuru kwa sababu aliweza kutupatanisha mikoa miwili ya Manyara na Tanga pamoja na wilaya hizi mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza, alifanya jitihada kubwa sana na akatenga shilingi milioni mia moja kwa ajili ya kupima. Kwa sababu kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa katika mkutano ule Mheshimiwa Waziri Mkuu aliagiza kwamba ili kutatua mgogoro ule ni lazima tutumie GN ya mwaka 1961, GN namba 65. Mheshimiwa Waziri wa Ardhi alituma wapimaji, wamefanya kazi nzuri sana na wameweza kuandika ripoti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tatizo hapa ni kwamba Mheshimiwa Waziri alielekeza ziwekwe beacons, leo takribani miezi miwili mitatu imeshapita wapimaji hawapo pale. Wananchi wa Jimbo la Kilindi wamenituma, wanajua kwamba yeye ni kiongozi mwadilifu, ameweza kutatua migogoro mingi, hivi tatizo liko wapi? Kwa nini wapimaji wale hawajaweza kuweka beacons kwenye mpaka huu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingependa kwenda mbele zaidi, lakini niamini kabisa, Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, wananchi wa Wilaya za Kiteto na Kilindi wana imani kubwa sana na Wizara yake, wana imani kubwa na utendaji wake Mheshimiwa Lukuvi. Mimi nimwombe, pale ambapo pamebaki sasa hivi ahakikishe kwamba wapimaji wanaweka mipaka ile ili shughuli za kilimo na ufugaji ziweze kwenda mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii nmkwambie, toka wamepita pale, toka Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuja pale wananchi wamekaa kimya wananiuliza Mbunge wao, Mheshimiwa Mbunge tatizo liko wapi, mbona hawa wapimaji wameondoka? Nimwombe Mheshimiwa Waziri, suluhu ya kudumu ni kuweka alama za beacons na kufuata maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya kwamba GN namba 65 ya mwaka 1961 inayogawa Mikoa ya Tanga na Arusha ndiyo alama sahihi, ndiyo GN sahihi na mimi nina imani kwamba na wewe utayasimamia hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo machache, nakushukuru na naunga mkono hoja.