Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. George Mcheche Masaju

Sex

Male

Party

Ex-Officio

Constituent

None

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nashukuru kwa kunipa fursa hii niweze kuchangia katika hizi hoja mbili na niseme tu kwamba naunga mkono hoja zote mbili. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa hii pia kushiriki katika kuchangia hoja hizi mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nitoe ufafanuzi katika baadhi ya masuala ya kikatiba na kisheria ambayo yamezungumzwa hapa. Niseme tu kumekuwa na hoja zinazojirudia sijui kama ni mkakati wa makusudi au ni kutokuelewa kwamba mambo yanatolewa ushauri hapa wa kisheria na Kikatiba lakini yanarejewa wakati fulani kwa namna ya kupotosha. Kwa sababu mimi wajibu wangu ni kutoa ufafanuzi wa eneo hilo, sitachoka kulisaidia Bunge liweze kuelewa wajibu wake vizuri linapotekeleza majukumu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, moja, kumekuwa na hoja inayodai kwamba Serikali inapoka madaraka ya Serikali za Mitaa. Hii si kweli kwa sababu Serikali za Mitaa ziko kwa mujibu wa Katiba. Ukisoma Ibara ya 145 na 146 ya Katiba zimeeleza vizuri Serikali za Mitaa. Katiba hiyo imesema pia kwamba hizi Serikali za Mitaa zitafanya kazi mbali ya Katiba pia kuzingatia sheria zilizotungwa na Bunge hili. Kwa sababu hiyo, zimetungwa Sheria kwa mfano The Local Government District Authorities, The Local Government Urban Authorities, The Local Government Finance Act na sheria nyinginezo. Kwa mujibu wa Ibara ya 146(2), majukumu ya hizi Serikali za Mitaa ni kutekeleza kazi za Serikali za Mitaa katika eneo lake, kuhakikisha utekelezaji wa sheria na ulinzi wa wananchi, kuimarisha demokrasia katika eneo lake na kuitumia demokrasia kuharakisha maendeleo ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mambo haya yote ndiyo msingi wa Katiba na hata sheria hizo zinazoongoza Serikali za Mitaa katika kutekeleza majukumu yake zimeweka Mabaraza ambayo wajumbe wake wanateuliwa na wananchi wenyewe. Kwa mfano, Sehemu ya Tano ya Sheria ya The Local Government District Authorities, inaeleza majukumu ya Serikali za Mitaa kuwa ni:-
(a) To maintain and facilitate the maintainance of peace, order and good governance within its area of jurisdiction.
(b) To promote the social welfare and economic well-being of all persons within its jurisdiction.
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria hiyo imeeleza mambo mengine mengi. Pia Sheria ya Tawala za Mikoa imeweka mamlaka ya Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya. Hawa ni wawakilishi wa Serikali Kuu katika hizi Serikali za Mitaa kuhakikisha kwamba haya mambo yanatekelezeka. Sheria hizi za Serikali za Mitaa zote mbili pia zinaeleza mamlaka ya Wakuu wa Mikoa na mamlaka ya Wakuu wa Wilaya katika hizo Serikali za Mitaa. Wakuu wa Mikoa wametajwa katika Ibara ya 61 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na kazi zao zimetajwa pale. Kwa hiyo, Wakuu wa Mikoa au Wakuu wa Wilaya wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao ambayo wamepewa kwa mujibu wa Katiba na kwa mujibu wa Sheria za Serikali hizi Mitaa na Sheria ya Tawala za Mikoa wasichukuliwe kwamba wanaingilia mamlaka ya Serikali za Mitaa, hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba vyeo hivi viko kihalali. Ukisoma Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya kwanza imeeleza eneo la Jamhuri ya Muungano, baadaye ibara ndogo inaeleza kwamba hili eneo la Jamhuri ya Muungano litagawanywa katika maeneo mbalimbali ya kiutawala ambayo ni pamoja na mikoa na wilaya na wanawekwa huko viongozi wa kusimamia. Kama ilivyo kwenye Bunge ambapo unakuwa na Spika, unakuwa na Wabunge, unakuwa na Madiwani ndivyo ilivyo pia kwenye executive ambapo unakuwa na Rais, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya. Kwa hiyo, huwezi ukavunja ile sasa ukasema kwamba hivi vyeo vifutwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo napenda kulitolea ufafanuzi ni suala la kwamba Serikali ilete Muswada wa Sheria ili kumpatia mamlaka Mkurugenzi wa TAKUKURU kufungua kesi mahakamani bila hata kupata kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka. Naomba kulishauri Bunge lako Tukufu kwamba sheria iliyopo inatoa mamlaka kwa Mkurugenzi wa TAKUKURU kufungua mashtaka mahakamani kwa baadhi yake bila kulazimika kupata kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka. Ukisoma kifungu cha 57 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kinaeleza hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la msingi zaidi ni kwamba Ibara ya 59B ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inampa mamlaka Mkurugenzi wa Mashtaka kuwa na uwezo wa kufungua, kuendesha na kusimamia mashtaka yote nchini. Kwa mfano, katika kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, makosa ya kudai, kushawishi, kupokea au kutoa ahadi za kupokea au kutoa rushwa haya yanafunguliwa na Mkurugenzi wa TAKUKURU bila kulazimika kupata kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka. Huyu Mkurugenzi wa Mashtaka, kwa mujibu wa sheria yao yeye ni huru, haingiliwi. Isipokuwa anatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia mambo yafuatayo, Ibara ya 59B(4) inasema;
“Katika kutekeleza mamlaka yake, Mkurugenzi wa Mashtaka atakuwa huru, hataingiliwa na mtu yeyote au mamlaka yoyote na atazingatia mambo yafuatayo:-
(a) nia ya kutenda haki;
(b) kuzuia matumizi mabaya ya taratibu za utoaji haki; na (c) maslahi ya umma.”
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama kuna watu hawafikishwi mahakamani amezingatia tu haya. Vilevile kama kuna watu wanafikishwa mahakamani amezingatia tu haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kulishauri Bunge lako Tukufu, Waheshimiwa Wabunge tujiepushe kuzungumzia mambo yaliyoko mahakamani. Hatua hiyo inakuwa na nia ya kuvuruga mwenendo wa mashauri yaliyoko mahakamani. Hakuwezi kukawa na parallel processes, Bunge lishiriki halafu Mahakama iendelee, sijui ufungue kesi nyingine Uingereza, how can we? Hii ni kuharibu tu mashauri haya yanayoendelea. Lazima Wabunge sisi tutambue mipaka ya madaraka yetu. Hizi hoja nyingine Waheshimiwa Wabunge tutumie hekima tunapokuwa tunazifikiria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme moja, uchaguzi wa Zanzibar ni uchaguzi huru, ulifanyika kwa haki kwa sababu ulisimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi. Tume ambayo ilitekeleza jukumu lake la Kikatiba kwa ufanisi ipasavyo.
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa hakuna chombo kilichosema kwamba uchaguzi ule haukuwa huru na wa haki.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilisisitize hili kwa sababu Katiba yenyewe ya Zanzibar katika Ibara ya 21(1) inasema; “Kila Mzanzibari anayo haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, ama moja kwa moja…”
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa walipewa nafasi hiyo, wakakataa wao wenyewe kushiriki. Hawawezi kudai kwamba uchaguzi ule ulikuwa sio huru wala wa haki. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa AG, muda wako umekwisha.
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja.