Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Allan Joseph Kiula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwa mara ya kwanza katika kikao hiki cha Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Waziri na Naibu Waziri kwa kazi kubwa wanayoifanya, wanasema mwenye macho haambiwi tazama. Yapo mabadiliko makubwa ambayo Waziri aliahidi alivyoingia kwenye Wizara hii kwamba atafanya mabadiliko makubwa katika Wizara yake na tunayaona. Jambo kubwa zaidi ni kwamba wananchi wanachotarajia ni kuona matokeo chanya, kuona mabadiliko na kupata huduma ambazo zinatolewa na Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma kwa makini hotuba ya Waziri imeainisha mikakati mbalimbali na mipango mbalimbali ambayo wanakwenda kutekeleza katika mwaka ujao wa fedha tutakapopitisha bajeti hii. Nami kabla sijasonga mbele zaidi niseme kabisa naunga mkono hotuba ya Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuunga mkono hotuba ya Waziri, yapo mambo ambayo lazima tuyazungumze kwa sababu sisi ni Wawakilishi wa Wananchi. Japan wanayo management system ya Gemba Kaizen. Gemba Kaizen maana yake unatakiwa uende kwenye eneo la kazi/tukio. Sasa suala la migogoro Wabunge wote tunasimama hapa kuzungumza migogoro ya mipaka. Hilo ni jambo kubwa sana, tunatarajia kabisa kwamba watendaji wa Wizara wafike kwenye mipaka hiyo na wafike kwa haraka na migogoro iweze kutatuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana nilichangia na mwaka huu nimekuwa nikimsumbua Waziri, hata juzi nilikuwa ofisini kwa Waziri na Naibu Waziri nimefika, kumweleza matatizo tuliyonayo wananchi wa Mkalama. Imekuwa ni adha kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lililopita nilimwonesha Waziri picha ya mwananchi aliyekatwa panga kwa sababu ya mgogoro wa ardhi. Hii migogoro ya mipaka inatakiwa ipate mwarobaini wake. Nilimweleza Waziri kwamba tuna mgogoro kati ya Iramoto na Hydom, Eshgesh, Singa ‘A’ na Singa ‘B’, Kikonda na Singida Vijijini, Lukomonyeri na Singida Vijijini, Iguguno na Singida Vijijini, Mpambala na Bukundi ambako ni Simiyu. Sasa migogoro ya mipaka haiishii watu kupigana mapanga tu hata shughuli za maendeleo wananchi sasa wamekuwa wanakwepa kuzifanya maana mtu mwingine anasema yuko Mkalama, mara anasema yuko Hydom, mara anasema yuko Manyara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la mipaka ni muhimu likawekwa wazi na likatatuliwa. Naamini kabisa kwa kasi ya Waziri na Naibu Waziri, jambo hili halitakiwi kuchukua muda na linatakiwa lifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ofisi zetu hasa za Wakuu wa Wilaya tumezifanya kama Mahakama vile, kwa sababu kila siku watu wako pale wanazungumzia suala la migogoro ya mipaka kati ya Wilaya na Wilaya na kati ya Mkoa na Mkoa, jambo hili tunaomba lipewe kipaumbele. Pia namshukuru Waziri alishaahidi kwamba atalifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni upimaji wa Miji na Vijiji. Suala hili na lenyewe ni muhimu sana kwa sababu ziko Halmashauri mpya zimeanzishwa na zilivyoanzishwa kata kadhaa zilitolewa na vijiji vilianzishwa. Hata hivyo, sasa wahusika hawajaenda kuoneshwa mipaka yao. Kwa hiyo, imeanza kuleta migogoro kati ya vijiji na vijiji. Hilo ni tatizo, na lenyewe ni kubwa ambalo linaleta usumbufu mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba humu limezungumzwa suala la Hati za Kimila, maeneo mengine ambayo sisi hatujaanza kufika hatua ya juu kwa nini tusipate Hati za Kimila kama wanavyofanya wenzetu wa Kiteto na maeneo mengine, kwa sababu Hati za Kimila inaonekana zinaweza kusaidia kupunguza migogoro hii. Hilo ni jambo muhimu, nawakumbusha tena Wizara, naomba waweze kulisimamia kwa ukaribu kabisa ili tuweze kuishi kwa amani katika Tanzania yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni suala la Baraza la Ardhi. Kwenye hotuba ya Waziri nimeona suala la Baraza la Ardhi na tumeona Halmashauri zingine Mabaraza ya Ardhi yameanzishwa. Hata hivyo, ukiangalia hotuba ya Kamati nanukuu ukurasa wa 18:

“Kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kuanzisha Mabaraza ya Ardhi katika Wilaya zote nchini.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri wenzetu Kamati wameliangalia hili jambo na wameliona kwa uzito wake na sisi kama Wabunge tunalileta hapa kwa uzito wake. Nieleze masikitiko yangu makubwa. Miezi sita iliyopita Wataalam walikuja Mkalama, wakaja pale wakatuambia masharti yao, wakasema tuwaoneshe jengo, wakaoneshwa jengo wakalikubali lile jengo, lakini toka walivyoondoka hakuna feedback.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kunapokuwa hakuna feedback ndipo uhasama unaanza kati ya wananchi na Wizara pasipo sababu yoyote ile. Kama Rais anatumbua watu, kuna tatizo gani kutumbua hao watu waliokuja miezi sita halafu hawajarudisha feedback? Nafikiri Waziri atachukua hatua na nafikiri wakati wa kuhitimisha atanipa majibu ya kuniridhisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachukulia hiyo kwamba ni dharau, tumedharaulika. Kama mtu anakuja unampa jengo halafu hafanyi kitu chochote ina maana ametudharau na sisi hatuwezi kudharauliwa kwa sababu mimi ni Mbunge wa Jimbo, nawakilisha wananchi wa Mkalama hapa. Kwa hiyo, nasi tuna haki kama ambavyo majimbo mengine yana haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, si hivyo tu, sisi ni Watanzania. Wananchi wangu wanapata huduma Baraza la Ardhi Kiomboi ambako ni mbali, kwanza kwenda kule lazima ulipe nauli na ukifika kule labda kesi inaahirishwa au unalala kule. Pia humu ndani kuna akinamama wengi, akinamama wengi wamedhulumiwa ardhi, wajane wamedhulumiwa ardhi, hawapati haki yao. Sasa jambo hilo ni muhimu lazima liangaliwe, kama Baraza linaweza kuanzishwa, kwa nini lisianzishwe watu wapate huduma mahali ambapo ni karibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne, nimpongeze Waziri kwa kualika taasisi zake mbalimbali. Tumeona hapa ndani kuna Watumishi Housing, National Housing na mimi nilipata bahati ya kutembelea Watumishi Housing na niliweza kutembelea National Housing, wanafanya kazi kubwa sana. Kwa sababu na wenyewe wako hapa, Wilaya mpya zinazoanzishwa tayari kuna potential ya uwekezaji wa nyumba za wafanyakazi. Kwa hiyo, Wilaya mpya kama Mkalama inahitaji uwekezaji wa namna hiyo iwe National Housing au Watumishi Housing.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Mkalama Mjini chumba peke yake choo kwenda nje shilingi 50,000. Sasa kama ni shilingi 50,000 hiyo ni potential market, lakini watumishi wanakaa kwenye substandard house na mtumishi haendi mahali kwa sababu ya mshahara peke yake, mtumishi anakwenda kuangalia na mazingira ya kazi. Kwa hiyo, tunatumaini hizi taaisi zinaweza kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna Mfuko wa Mikopo ya Nyumba kwa watumishi wa Serikali. Mfuko huo ulianzishwa na Sheria ya mwaka 1992. Tunajua umefanya kazi kubwa, ukisoma kwenye bajeti ya Waziri tunauona kama ule Mfuko uko under funded, funding zinazokwenda pale hazitoshi. Tunaomba fund hizo ziweze kuongezwa ili watumishi wengi waweze kupata mikopo na waweze kujenga nyumba pia tuangalie marejesho waliokwishapata urejeshaji wake uko vipi? Ningependa kufahamu Mfuko huu tangu uanzishwe ni watumishi wangapi wamekwishapata hiyo mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine namba sita ni kuhodhi ardhi. Kama alivyosema Waziri hilo jambo ni la kusema hapana, watu wengi wamehodhi ardhi, wananchi wanaongezeka na mtu mwingine anakuwa na ardhi kubwa, kazi yake haitumiii yeye anakodisha watu kulima tu na hiyo iko sana kule Kidarafa, iko sana Mwanga, sasa huo ni unyonyaji, ardhi ya kwetu wewe kazi yako ni kukodisha watu. Nafikiri ni muda muafaka sasa Wizara kuchukua hatua na kuwachukulia hatua wale watu kwa kuwanyang’anya ardhi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la saba ni ardhi versus ongezeko la wananchi. Wizara hii ni Wizara nyeti, Taifa zima linategemea Wizara hii. Nafikiri Wizara inatakiwa ije na strategic plan ya kuonesha ukubwa wa ardhi na ongezeko la watu plus economic activities, mifugo, kilimo, madini, hilo ni jambo muhimu sana. Hata migogoro ambayo ilikuwa inazungumzwa jana kwenye Wizara ya Utalii yote hii inagusa rasilimali ardhi, watu hatujapangwa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni jukumu la Wizara hii kuweza kutupanga vizuri na uamuzi unatakiwa utolewe sasa hivi kwa sababu tunapochelewa kutoa uamuzi tunatengeneza bomu ambalo baada ya miaka mingi hatuwezi kulihimili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja nafikiri ujumbe utakuwa umefika mahali pake. Tuna imani na Wizara hii na tuna imani na Mheshimiwa Waziri na Naibu wake. Tunatumaini kwamba Tanzania itakuwa Tanzania mpya na watafanya kazi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.