Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Kamisheni ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Malawi

Hon. Salum Mwinyi Rehani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Kamisheni ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Malawi

MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na mimi kupata fursa hii adhimu. Kwanza niunge mkono hoja hii ya kuanzisha Commission hii ya Bonde la Mto Songwe ambayo kimsingi, the highly potential area kwa nchi yetu, kwa uchumi wa nchi hii, lakini vilevile kwa mustakabali wa wananchi wale wa Wilaya zile tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwamba mimi kwa bahati nzuri nimeusoma huu mkataba vizuri na nimeuelewa madhumuni yake. Ikiwa dhumuni kubwa ni kuhifadhi, kuendeleza na kuondoa athari za maji ambayo yanasababisha mto ule uweze kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine na tishio la athari ya wananchi ambao wanakaa pembezoni mwa mto ule.

Mheshimiwa Naibu Spika, fursa hasa za kuangalia kitu gani ambacho kitaweza kutusaidia kama nchi, eneo lile la Mto Songwe kwa Tanzania ni belt ya uzalishaji wa mazao mbalimbali. Kinachotakiwa baada ya kuridhiwa Kamisheni hii; Kamisheni itengeneze mpango mkakati ambao utaweza kuridhiwa na pande zote mbili kwa sababu yale yote yaliyoainishwa katika Kamisheni hii, kila mmoja yanamgusa hasa kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpango mkubwa pale wa kuanzisha mabwawa matatu yale ya Songwe Juu, Songwe Kati na Songwe Chini, kwa kweli kwa Tanzania ni fursa kubwa kwanza kwa upatikanaji wa maji hasa ya mvua. Ile dhana ya rainfall harvesting pale ndipo itakapotimia. Tutakapoweza kuyavuna yale maji, tutaweza kuu-shape ule mto uweze kwenda kwa mujibu wa mwelekeo tunaoutaka sisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile mto ule unafungua uwanja mpana wa kuanzisha maeneo ya umwagiliaji maji kwa eneo lile la Kyela. Tutaweza kuzalisha mpunga kwa kutumia yale mabwawa kama wanavyozalisha Moshi Chini na Moshi Juu. Tufanye uwekezaji wa maana ili nchi ionekane kwamba kuanzisha ile Kamisheni imeleta manufaa na isiwe Kamisheni tu kama nyingine ambazo baada ya miaka mitano, kumi tukija kutathmini, hakuna kilichofanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba Mawaziri watakaosimamia, pawe na uwekezaji ambao utaleta fursa kwa kila sekta. Tukizungumza Sekta ya Kilimo, zaidi ya hekta 15,000 pale tunaweza kuzifanya zote kuwa za umwagiliaji maji na zikaweza kutuzalishia zaidi ya tani laki tatu za mchele. Hilo linawezekana, suala ni kujipanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika eneo lile kuna mazao ya biashara, kuna ndizi ambalo ni zao kubwa katika maeneo yale ya Tukuyu na Kyela. Fursa ya uzalishaji kwa kutumia irrigation ipo, kutumia mabwawa yatakayoanzishwa kule. Tuhamasishe wananchi wajipange kwenye uzalishaji wa tija kuliko uzalishaji wa kutegemea mvua ambao hauna uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo yale, bado unaweza kuzalisha mahindi kwa mpango maalum na nchi ikaweza kunufaika na kuondokana na tishio la njaa linalotokana na ukosefu wa maji wa kila siku. Isitoshe, kazi kubwa inayotaka kufanywa pale ni kuhifadhi mazingira ya vyanzo vya mto ule toka vinavyotokea huko kwenye zile chemchemi za kutilia maji katika eneo lile, kwa sababu maji katika eneo lile ni mwaka mzima. Hiyo siyo kwamba yanavunwa yale ya mvua, lakini maji yanatoka kwenye chemchemi ambazo ziko katika maeneo mbalimbali na ndiyo maana tunapata fursa na nguvu ya kuanzisha yale mabwawa ya kuzalisha umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pale panategemewa kuzalishwa umeme zaidi ya megawati 180, kitu ambacho tunafikiria tu kwamba mgawanyo uwe nusu kwa nusu. Nasema, bwana, kila mwamba ngoma huvutia kwake vilevile. Asilimia kubwa ya ule mto na eneo kubwa ni letu siye, lakini na zile infrastructure ambazo zinahitajika kujengwa katika eneo lile ziko kwetu. Nafikiri hao watakaoenda kukaa; Mawaziri na watu wengine, waangalie uwiano wa kugawana na siyo tu kwa kujenga mahusiano ya kusema kwamba tunaridhiana nusu kwa nusu, hapo tupaangalie kwa undani zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nitachangia katika hii Kamisheni ni uanzishwaji wa viwanda. Tuhamasishe maeneo yale ambayo yanazalisha kokoa katika maeneo mbalimbali ya Kyela, basi kuwepo na kiwanda ambacho kitaweza kuzalisha Chocolate na vitu vingine kuanzishia wananchi wetu ajira na fursa nyingine mbalimbali za kiuchumi zitakazokuwepo kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo vilevile inafungua corridor ile kuweza kuwa na mpango wa kujengwa reli kutoka huko Mchuchuma mpaka Lindi lakini ikaunganisha mpaka kwenye reli ya TAZARA. Itazidi kufungua fursa kubwa za kiuchumi na kulifanya eneo lile kuwa moja katika eneo, wanaita economic zone. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili kwa nchi yetu limekuwa likitumika isivyo na faida; yaani likitumika kikawaida. Hii sauti ya kuanzisha Kamisheni ilianza miaka mingi, lakini tushukuru Mungu sasa hivi Serikali imefika mahali pa uamuzi wa kuianzisha na kuanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba wataalam mbalimbali wa Wizara zote zinazohusika na Kamisheni hii kukaa na kuanzisha miradi ambayo itaweza kuwasaidia wananchi kushiriki nao hasa kwenye uhifadhi wa mazingira ya eneo lile, kwa sababu kila eneo mto unapopita mazingira yanakuwa ni mazuri, lakini kutokana na kazi na shughuli za kibinadamu, mazingira yale yanaharibiwa kwa njia moja au nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, wito wangu niombe hasa Wizara ya Kilimo kupitia mifugo, eneo hili lilindwe na lisiingizwe mifugo. Tutalimaliza! Tutauua ule mto na matokeo yake maji yale yatashindwa kutiririka kama yanavyotiririka hivi sasa. Haya ni mambo ya msingi. Tunaweza kuanzisha mambo mazuri, lakini kuna lingine tukalisahau ambalo linaathiri mazingira ya pale. Kwa hiyo, nawaomba sana wahusika wa Mikoa, Wilaya na maeneo mengine kuweza kuepuka uingizwaji wa ngombe wengi katika maeneo yale pale ambayo yanatumika kwa kilimo sasa hivi kikubwa. Kule Zanzibar wanasema mchele wote unaoletwa kutoka Mbeya ndio wenye soko kubwa. Kwa hiyo, nawaomba wazalishaji na viongozi walioko katika maeneo yale tuweze kutilia mkazo sana uzalishaji wa mazao mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nimeliona kwamba ni fursa kubwa, zile meli za bandari za Itui, Itumbi na sehemu nyingine, pale sitaweza kufanya kazi vizuri zaidi, kwa sababu ufungukaji wa ile Kamisheni itaanzisha fursa kubwa ya wafanyabiashara, lakini na wenzetu wa Malawi watapata fursa kubwa ya kuleta mizigo yao katika maeneo yale na hasa kwa kutumia ile meli mpya iliyoundwa hivi sasa iliyokuwa inaanza kazi kuwa na manufaa zaidi kuliko vile ambavyo tulivyokuwa tumetegemea.