Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Zainabu Mussa Bakar

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. ZAINAB MUSSA BAKARI: Mheshimiwa Naibu Spika, Maji ni Uhai. Maji ni kila kitu katika maisha ya kila siku ya binadamu; ndiyo maana ukaja msimamo kuwa maji ni uhai. Tukizungumzia uhai tunazungumzia maisha ya kuweza kuishi na kuleta afya njema ambayo yatatengeneza uwezo wa mwanadamu na viumbe vingine viweze kuishi na kuleta tija na mwisho kutimiza kiu yetu ya maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maji na Umwagiliaji na Serikali ione sasa umuhimu wa kuvuna maji. Yaani iandae mkakati wa makusudi wa kuvuna maji hususani wakati wa mvua na hata maji yanayoporomoka katika milima yetu. Ni jambo la ajabu wakati wa mvua kuwa na mafuriko na baadaye mifugo na binadamu ikaanza kufa kutokana na ukame. Kuwe na utaratibu wa kujenga mabwawa ya kuhifadhia maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuwe na mfumo wa kuvuna maji kwa kuhakikisha nyumba zote zinazojengwa ziwe na mfumo wa kuvuna maji wakati wa mvua, hii itasaidia sana kero hili kuondoka. Pia suala la kuanzishwa kwa Wakala wa Maji Vijijini limejadiliwa, sana na leo hii niulize Wizara na Serikali, uanzishwaji wa Wakala wa Maji Vijijini utaanza lini?

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la maji ni suala nyeti na hasa kwa sababu Rais wetu anatamani kuwatua kina mama na watoto kuwatua ndoo ya maji kichwani, hivyo kuna haja ya kutimiza azma ya Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Hivyo Serikali ione sasa umuhimu wa kuokoa taifa hili kwa kuwanusuru kina mama na watoto vifo.

Mheshimiwa Naibu Spika, asilimia tisa ya vifo vya watoto vinatokana na kutumia maji yasiyo safi na salama. Kuna maradhi ya milipuko kama vile Typhod, Kipindupindu na kuharisha na kutapika. Ni wakati sasa wa kupunguza vifo hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali iongeze bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Mfuko tulioongeza tujue matumizi yake yakoje. Pia tunaomba kuwe na tozo, kila lita moja ya mafuta itozwe 100 kwa kila lita ziende kwenye maji au Mfuko wa Maji. Hali kadhalika asilimia 70 ipelekwe kwenuye miradi ya maji vijijini na asilimia 30 miradi ya mijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli sasa wakati wa kumtua mama ndoo kichwani umefika; nazungumza hivyo kwa msisitizo; ni wakati sasa kina mama na watoto kufanya kazi nyingine za kimaendeleo badala ya kufuata maji sehemu za mbali na kutumia saa moja kutafuta maji au wastani dakika 33 kufuata maji. Ni shida na ni kero sana kwa wananchi; wananchi wanakosa kushiriki mambo mengi ya kimaendeleo. Hata hivyo zile mita 400 za kupata maji si toshelezi, hivyo Serikali ikishirikiana na Wizara walione hili kuwa ni bughudha na kero kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali ione umuhimu wa hili na kuongeza bajeti ya maji ili tupate muda wa kufanya kazi za maendeleo. Pia lazima tuwe na msisitizo katika Kilimo cha Umwagiliaji kwani Kilimo ni Uti wa Mgongo hivyo tutumie mito yetu vizuri kwa kuweka mfumo mzuri wa kuweza kumwagilia ili kilimo hcetu badala ya kungojea mvua tu tutumie vyanzo hivi ili kuweza kukuumarisha kilimo chetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali izingatie suala hili kwa upana na huruma ili iweze kumuokoa Mtanzania katika shida hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.