Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Zainabu Mussa Bakar

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuongelea juu ya kuimarisha taasisi ya Utawala Bora. Kuhusu eneo hili la utawala bora Serikali ijipange vya kutosha kwani inaonekana kutosimamiwa kwa uadilifu ipasavyo bali Serikali inakwenda kwa hamasa za kisiasa zaidi kuliko kiuadilifu kwa kufuata misingi ya kidemokrasia. Demokrasia inamezwa kwa maslahi ya wachache na wengi kunyimwa haki zao. Wananchi wananyanyasika vibaya sana, hata vyombo vya dola vinaendeshwa kisiasa zaidi jambo ambalo si haki na halipendezi. Jambo hili linatufanya wananchi tukose imani na Vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia rushwa na ufisadi unaendelea kwa kasi nchini. Hivyo TAKUKURU imarishwe kwa kupatiwa rasilimali watu na bajeti ya kutosha ili waweze kujikimu na kutekeleza majukumu yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, mawasiliano ni jambo muhimu kwa binadamu hivyo ni lazima watu wajue taarifa mbalimbali za nchi yao. Hivyo, Serikali isiwanyime wananchi wake na walipa kodi walio wengi haki yao ya msingi ya kuliona Bunge lao na Wawakilishi wao wanavyowatetea. Hiyo ni haki yao ya msingi na ya Katiba wanataka wapate taarifa muhimu za bajeti zinazoendelea na taarifa za Majimbo yao walizozileta.
Mheshimiwa Naibu Spika, watumishi hewa Serikalini. Hili ni tatizo, Serikali ijipange na ifuatilie ufisadi huu ipasavyo kwani linaumiza kodi za wananchi, watumishi kujipandikizia mishahara miwili miwili si jambo jema. Hivyo, Serikali ifanye kazi ya ziada kuondoa watumishi hewa na wachukuliwe hatua za kisheria wanaohusika na hayo.
Kwanza, Makatibu Tawala, Wakurugenzi, watendaji waliosababisha uwepo wa watumishi hewa wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo. Pili, Serikali iunganishe mifumo ya rasilimali watu inayojitegemea. Mifumo ifuatayo iunganishwe, vizazi na vifo, malipo Serikalini, namba ya Kitambulisho cha Taifa, mfumo wa malipo ya kodi na malipo ya pensheni. Tatu, Tume ya Utumishi wapewe watumishi na vitendea kazi vya kutosha ili wafanye kazi kwa ufanisi na kutimiza majukumu yao kwa umakini zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF). TASAF ni jambo jema kwa wananchi kwa sababu inawasaidia sana. Ila pesa hizi ni nyingi sana; kwa kupewa wananchi pesa taslimu hakuwezi kuondoa umaskini na badala yake kwa kuanzishiwa miradi kunaweza kuondoa umaskini na kuweza kujikimu kimaisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba maoni yetu yazingatiwe ili kuendeleza Taifa letu kwa maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha maoni yangu.