Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye hii hoja muhimu ya maji. Namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitasema mawili tu kwa haraka haraka. Kwanza kikubwa ni kuishukuru Wizara kwa sababu Jimbo la Ushetu ni Jimbo ambalo liko katika Wilaya hii ya Kahama, lakini utaona kipindi kilipita tumekuwa na shida kubwa sana ya maji na kwenye bajeti hii ambayo tunaitekeleza niseme wananchi wa Ushetu wanashukuru kwamba tumekuwepo na miradi kwenye kata nane na katika kata tatu tayari wananchi wameanza kupata maji. Kwa hiyo, naishukuru sana na kuipongeza Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Kata hizi za Idahina, Ukune, Chambo, Bulungwa, Nyamilangano, Kinamapula Kata ya Ushetu yenyewe na Kata ya Ulowa, tulitenga fedha mwaka 2016/2017, kwa hiyo, naiomba Serikali iendelee kukamilisha hii miradi ambayo inaendelea ili wananchi waendelee kunufaika na kuachana na adha ya ukosefu wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nataka nizungumzie, wananchi wa Ushetu wanahitaji maji ya Ziwa Victoria. Kama nilivyosema kipindi kilichopita, Jimbo la Ushetu linachukua eneo la asilimia 57 ya Wilaya ya Kahama, lakini maji ya mradi wa Ziwa Victoria yamefika Kahama Mjini, lakini maji haya hayajasambazwa Ushetu. Wananchi wa Ushetu wanaomba maji ya Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa sababu wataalam wa Wizara wako hapa, nikumbushe, kulikuwa kuna maombi ya maji mwaka 2014, tuliahidiwa kwamba Mkandarasi Mshauri angeenda kwa ajili ya kusanifu ili maji yaende Ushetu. Sasa mradi uliishia njiani. Kwa hiyo, naomba sana Serikali iangalie ili tuweze kupata maji katika Kata za Ukune, Kisuke, Nyamilangano, Uyogo, Ushetu na Ulowa; na kuna vijiji vipatavyo 32. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri pia kwenye mradi wa maji ambao utakuwa ukipitia kwa majirani zetu katika Halmashauri ya Mbogwe, sehemu ya Masumbwe, tunaweza pia tukapeleka maji kwenye Kata za Idahina, Igwamanoni, Nyankende ambako kuna vijiji 40 vinaweza kunufaika. Kwa sababu lengo la Wizara au la Serikali ni kuhakikisha kwamba mwaka 2020 tunaweza kuwa na maji vijijini kwa asilimia 85. Kama hatupati maji ya Ziwa Victoria itakuwa ni ndoto. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali izingatie hili na nimefanya mazungumzo na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji namshukuru sana na naamini yale tuliyokubaliana kwa ajili ya kutusaidia Ushetu ataweza kutusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu nizungumze juu ya ubora wa report za miradi. Waheshimiwa Wabunge wengi hapa wamekuwa wakizungumza wanaona kwamba miradi inajirudia, lakini utagundua kwamba ile reporting system yetu tuiangalie vizuri, Wizara ya Fedha isaidie kwamba twende kwenye IPSAS accrual ili tuweze kupata report ambazo zitakuwa zinaleta maana. Kwa maana ya mchanganyiko wa cash basis na accruals inatuchanganya sana. Kwa mfano utaona kwa upande wa Halmashauri ya Ushetu tumepokea fedha shilingi bilioni 506 lakini haiwezi kueleweka mapema kwamba hizi fedha zilikuwa zimetengwa mwaka upi wa fedha. Kwa hiyo tukienda vizuri kwenye hizi report itaweza ku-report miradi yetu vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naishauri tu Wizara ya Fedha isaidie sana ili hizi report za miradi ziende kwenye ile reporting system ambayo nafikiri itakuwa ni nzuri zaidi ili kututoa katika mchanganyiko ambao tunaweza kukanganyikiwa zaidi. Kwa hiyo, nafikiria niseme hili, kwa sababu nimeona maeneo mengi sana yamekuwa yakituchanganya; tukienda kwenye accrual ziko faida nyingi. Hii itaweza pia kutusaidia kuoanisha bajeti na matumizi kwa kipindi husika. Kwa hali ilivyo sasa hivi mchanganyiko unakuwa ni mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda nishauri kwamba, tume-adopt accrual basis of accounting, kwa hiyo, nafikiri Serikali isukume sana ili zoezi likamilike, itatusaidia sana kuweza kupata report zenye ubora zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.