Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza nakushukuru wewe na namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima. Naunga mkono watu wote wanaosema pesa za maji ziongezwe kwa sababu ya umuhimu wenyewe. Mimi kwangu nina matatizo katika miradi kadhaa inayoendelea. Jimboni kwangu kuna miradi ya maji ya vijiji 10. Mradi wa Kawa umetumia zaidi ya shilingi bilioni mbili na nusu, lakini maji hayajaanza kwenda kwa wananchi. Hii ni hasara kubwa. Kwa hiyo, wananchi hawaoni tija wala thamani ya pesa ambayo imetengwa kwao. Naomba Wizara isukume jambo hili liwezekane. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kadhalika kuna Mradi wa King’ombe. Katika mradi huu tumetumia zaidi ya shilingi milioni 720, lakini mradi huu bado una shida katika maeneo mbalimbali, hasa katika maeneo ambayo bomba lake liko juu. Naomba Serikali ihakikishe kwamba maeneo ambayo bomba linaonekana linakatwakatwa ovyo ovyo, waweke sehemu ile chuma ili huduma ya maji iwafikie kwa uhakika. Wananchi wote wanaohujumu, mimi nalaani vitendo hivyo na hatuwezi kuviunga mkono hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, upo mradi wa siku nyingi sana wa maji kutoka Kate kwenda Isale, unapita Vijiji vya Ntemba, Kata, Ntuchi, Ifundwa na Msilihofu. Huu mradi ni muhimu sana, umekuwa ukiahidiwa na Maraisi wote wawili, akiwepo Jakaya Kikwete na huyu ambaye tupo naye kwenye madaraka sasa. Pesa zilitengwa zaidi ya sh.2,800,000,000/=. Naomba, sasa hivi Wilaya ya Nkasi mlitutengea pesa sasa hazionekani. Naomba mradi huu nao uanze kufanya kazi mara moja ili wananchi wa vijiji hivyo waweze kupata maji ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile upo mradi wa Kijiji cha Kisura. Mradi huu nao umekuwa ukisuasua, una zaidi ya shilingi milioni 400. Naomba Wizara itoe msukumo wa kutosha katika jambo hili ili maji yaweze kupatikana. Vijiji vyote kwa ujumla kwa Kata ya Nkandasi, Kata ya Kipande na vile vile Kata ya Nsintali bado maji ni taabu kubwa sana. Naomba pia utafiti ufanywe katika maeneo haya ili maji yaweze kupatikana katika vijiji vinavyohusika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika mradi wa umwagiliaji. Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi ina Majimbo mawili; Jimbo la Nkasi Kusini na Nkasi Kaskazini. Miradi inayotajwa hapa kwenye umwagiliaji, yote miwili imekaa kwenye Jimbo moja. Jambo hili nimekuwa nikilizungumza kila wakati. Sisi kwenye Jimbo la Nkasi Kusini tulishabainisha uwepo wa Miradi ya Bonde la Mto la Kate na Bonde la Mtisi lililopo Kijiji cha Namansi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumetoa mapendekezo, tunaomba tu pesa za kuanza kujenga miundombinu, lakini sijawahi kupata hata wakati mmoja. Naomba ufike wakati haki itendeke. Maana yake, ninapimwaje mimi? Tupo Jimbo moja lakini miradi ipo sehemu mbili, inapata pesa lakini iliyopendekezwa upande wa pili haipati pesa. Naomba na hilo mliangalie kwa umakini sana ili kutujengea pia siasa nzuri. Bila kufanya hivyo, maana yake tutakwama.

Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo yote yaliyokwishafanywa na Halmashauri, kinachotakiwa sasa ni kuomba pesa ili miundombinu ianze kujengwa hasa katika bonde hili la Kate ambalo kwa kweli ni kubwa la kutosha na linaweza kuzalisha chakula ambacho kitakuwa ni msaada mkubwa sana, mkijua kwamba mazingira yetu sisi Mkoa wa Rukwa ni wazalishaji wazuri sana wa chakula.

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante