Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nisema kwamba kwanza nasikitika na ninawashauri tu Wabunge wapya na vijana, jukumu letu sisi ni kuisaidia Serikali na kuisaidia nchi. Anasimama Mbunge anatoa pongezi kwa Wizara ya Kilimo kwa sababu ya hoja moja ya tozo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake anatumia robo tatu ya muda kusema tozo mbalimbali alizozikata badala ya kutuambia pamoja na hiyo tozo kukatwa tuna mikakati gani mipana ya kusaidia 75% ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tungewekeza kwenye kilimo ipasavyo kama ambavyo mipango ya miaka mitano mitano kwa miaka zaidi ya 30 iliyopita, kama ambavyo Ilani ya Chama cha Mapinduzi imekuwa ikisema kwa miaka zaidi ya 30 iliyopita, ajenda isingekuwa tozo yaani tungeongeza kodi Serikali ingepata mapato kwa sababu tumewekeza vizuri. Ni muhimu Wabunge wapya wakajua Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi iliahidi kuongeza…

T A A R I F A . . .

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ananipotezea muda. Ninachotaka kumshauri, mimi unajua natoka Jimbo la mjini, alright! Asilimia 85 mnatoka majimbo ya vijijini. Tukichukulia mzaha bajeti ya kilimo, mimi kwangu naathirika kwa sababu tu ya mfumuko wa bei.

Kwa hiyo, ni lazima nizungumze hapa kwa sababu mwaka 2016 mfumuko wa bei ulikuwa 5.4% sasa hivi ni 6.4% kwa mujibu wa ripoti ya BOT iliyotoka juzi. Kwa sababu chakula, mahindi, sukari, mihogo imepanda bei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapozungumza hapa, tunataka wenzetu wasikie. Hivi unapongezaje bajeti ambayo mlituahidi kilimo kitakua kwa 10% mwaka 2010; kikashuka, sasa hivi kilimo kinakua kwa asilimia 1.7%? Mwaka 2016 kilimo kilikuwa kinakua kwa 2.7%; mwaka 2015 kilimo kilikuwa kinakua kwa 4%! Kwa hiyo, kwa kadiri ambavyo siku zinakwenda, kilimo kinazidi kushuka chini; na tafsiri yake 75%wa Watanzania wako hoi bin taabani! Hatuoni? Hivi tunapongeza nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya maendeleo inaniuma! Bajeti ya maendeleo, eti kati ya shilingi bilioni 101, zimepatikana shilingi bilioni 3.3, sawa na 3.31%. Hivi tunapongeza nini? Hivi Mheshimiwa Waziri huyu…

T A A R I F A . . .

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Chief Whip Kivuli! Aah, Mheshimiwa Chief Whip. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosema ni hivi, labda nirudie, niweke vizuri. Kwa sababu sisi ni rahisi ku-propagate mambo. Nasema hivi 75% ya Watanzania ambao wanafanya kazi ya kilimo, ambao 80% ndani yake ni wanawake, wamefukarishwa na Serikali ya CCM kwa sababu ya mipango ambayo hawana mikakati ya kuitekeleza. Ndiyo maana…

MWENYEKITI: Hapana Mheshimiwa Mdee. Unaikubali taarifa au unaikataa?

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeikataa kwa sababu haina issue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachosema ni nini Wabunge? Nasema kwa nia njema kwamba kama leo bajeti ya maendeleo ya kilimo tumetoa 3%; mwaka 2016 tukasema utekelezaji, ndugu yetu ni mpya 15% tena kwenye shilingi bilioni 32 ikatoka shilingi bilioni tano, asilimia 15.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umwagiliaji, wakati anasoma Waziri wa Maji imepatikana 8% tu. Tume ya Umwagiliaji ina wajibu wa kuhakikisha kwamba Sera ya Umwagiliaji inatekelezwa ili miundombinu ya umwagiliaji iwekwe kule kwenye mashamba, halafu eti mtu anakaa anapongeza, unapongeza nini? Hatuisaidii Serikali! Hatuisaidii nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea kwamba tutasimama hapa kwa sababu wengi tunawakilisha wakulima, tuweke mguu chini, tuiambie Serikali…

T A A R I F A . . .

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, siwezi kukubali, yaani haina mashiko. Siwezi kukubali hiyo taarifa, kwa sababu sisi tunasoma nyaraka ya Serikali. Tunasoma Taarifa za Kamati za Bunge. Sasa kama hizo taarifazinatuambia hivyo, hayo makandokando mengine ya kuombaomba huko, sisi hayatuhusu. Sisi tunazungumzia bajeti ya Serikali na tuko kwenye bajeti hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wasiniingilie.
Mheshimiwa mh! Jana…

T A A R I F A . . .

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Wabunge wa CCM, vijana na watu wazima ambao wameingia, wametukuta sisi tukiwemo, mkasome vizuri Ilani ya CCM. Mimi huwa naipitia, kwa manufaa tu ya kujenga, kwa sababu mwisho wa siku, mafanikio ya Ilani yenu, ni mafanikio yenu na ni mafanikio ya Taifa. Kwa hiyo, hapa hatutafuti mchawi. (Makofi)Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nawashauri wakasome Mipango ya Maendeleo mbalimbali. Yaani usije ukawa umekuja mwaka 2010, basi unachukua ule Mpango wa Maendeleo wa 2010 ama 2015; unakuja 15 kwenda mbele. Lazima tujue tumetoka wapi, tunakwenda wapi ili tuweze kushauri vizuri. Kwa hiyo, tusichukiane, dhamira ni njema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi kwa sababu watu wamezungumza suala la utafiti hapa, ni kweli! Tuliazimia na Serikali ikakubali kwamba 1% ya pato la Taifa itaenda kwenye utafiti kwa sababu dunia ya sasa hivi bila kufanya tafiti ili uweze kujua unataka nini, huwezi kupanga mipango yako. Isipokuwa mpaka sasa fedha zinazotolewa kwa tafiti zinatia aibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Mwijage amekuja hapa, kwa sababu tu ameandika kwenye hotuba yake viwanda ambavyo vimekuwa registered, yaani watu wameenda kusajili tu pale TIC! Kwa sababu ameandika kwenye hotuba yake viwanda
224. Kila Mbunge anapongeza anajua viwanda vimeshafanyaje? Vimeshajengwa! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nimepitia hivi viwanda 224, si tuko kwenye hotuba ya kilimo! Sasa wamezungumza watu, hakuna kilimo bila raw materials, viwanda gani hivyo? Nimeangalia hapa viwanda 224, robo tatu viko mjini Dar es Salaam. Halafu viwanda vyenyewe basi ukienda kuangalia deep into details unaweza ukacheka, ufe mbavu, uzimie na ufe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana wamezungumza watu hapa suala la pamba, nikasema hebu ngonja niangalie, kwenye hivi viwanda 224 hivi kwenye hiyo mikoa, kwenye robo hiyo chache basi, hivi viwanda vya kuiongezea hadhi Pamba vipo? Hakuna hata kimoja!

Sasa unajiuliza hivi wale ndugu zetu wa Kanda ya Ziwa hususan mikoa ambayo inalima pamba, pambaambayo ni zao muhimu, akiwemo Mheshimiwa Mtemi Chenge, hamko kwenye mipango ya Serikali, halafu anasimama mtu hapa anapongeza, eti tozo. Yaani tozo isingekuwa issue kama wakulima wetu hawa tungewapa mitaji; kama tungeweza kuweka miundombinu na tungetoa fursa za kilimo! Tozo siyo issue! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hiki kitabu, mlisema juzi hapa kwamba hii Serikali ni moja, siyo kwamba Wizara ni ya huyu, ni wa huku, Serikali ni moja! Hivi iweje leo ukisoma kitabu cha Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara, ukisoma kitabu cha Mheshimiwa Waziri wa Kilimo…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila mpangilio)

MHE. HALIMA J. MDEE: Vipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma hivi vitabu viwili, moja ni mbingu, nyingine ni dunia. Hivi vitabu havikutani. Kwa hiyo, sasa sisi tunaiomba Serikali jamani, tuache kutumia, sijui tuliwanyima Watanzania elimu! Tuna-take advantage ya kuwanyima elimu, maana tumeambiwa 31% ya watu ambao hawajui kusoma na kuandika. Sijui tunafanya makusudi ili ukienda na hoja nyepesi unaijengea maghorofa kama vile hiyo hoja ndiyo ulikuwa umeahidi, kumbe ulikuwa umeahidi kitabu kinene hivi!

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba kwa dhamira nzuri kabisa, tuisaidie nchi! Yaani naomba kwa nia njema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Kilimo alituambia mwaka 2013 kulikuwa kuna sera mpya ya kilimo. Hivi ni vitu gani ambavyo viko kwenye Sera ya Kilimo ya 2013 ambavyo vimekuwa reflected huku, yaani inauma! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunazungumzia masuala ya migogoro ya wakulima na wafugaji. Mwaka 2011 tulileta hoja binafsi hapa, miaka saba kama siyo sita iliyopita, tukaiambia Serikali tufanye land auditing nchi nzima ili tuweze kujua kila kipande cha ardhi cha nchi yetu anayo nani? Kama ni mwekezaji, kama ni mkulima, kama ni mfugaji ili tuweze kupanga matumizi bora ya ardhi, Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka sita iliyopita nilitoa hiyo hoja, Bunge likaunga mkono, likawa Azimio la Bunge na aliyekuwa Waziri wa Ardhi akafanya mabadiliko kidogo. Tukasema tukifanya hivi, tutaweza kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji, tutaweza kujua mashamba makubwa ambayo yako chini ya wawekezaji ni mangapi. Tutaweza kujua wakulima wetu wadogo na wafugaji wakoje, ili tuweze kupanga mipango kama nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka sita baadaye Azimio la Bunge ambalo nadhani lilikuwa ni la kihistoria kwa pande zote; Waheshimiwa Wabunge wa Chama Tawala na Upinzani tuliungana tukasema…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa. Muda wetu ndiyo huo. Ahsante sana.