Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua nafasi hii pia kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri ambayo anaifanya na anaendelea kuifanya. Pia nichukue nafasi hii kumpongeza sana Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa kwa kazi nzuri anayoifanya ya kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze pia Mawaziri wote kwa Wizara mbalimbali kwa jitihada zote ambazo mnaendelea nazo kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Hongereni sana, kazi mnayofanya inaonekana na Mungu awajaalie kila la kheri, awape wepesi ili muendelee kudunda kazi kama kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nimeona ni vizuri nikaenda moja kwa moja kwenye eneo la afya. Katika Manispaa yetu ya Songea, kituo cha afya cha Mjimwema ambacho hivi karibuni kinatarajia kupandishwa hadhi na kuwa Hospitali ya Wilaya pana shida kwani hakuna vifaa vya upasuaji. Leo hii tunakwenda kupitisha hii bajeti ya TAMISEMI, labda Mheshimiwa Waziri ataniambia katika eneo hili kuna pesa ambazo zimetengwa? Nimejaribu kuangalia hapa sijaona na kama nilichokiona bado ni kidogo na ndiyo maana kama vile sijaona. Kwa hiyo, niombe katika kituo hiki cha afya ambacho kinakwenda kupandishwa hadhi mwezi wa saba basi kuwe na umuhimu kuhakikisha kwamba vifaa vya upasuaji katika chumba cha upasuaji vikamilishwe ili inapopanda kuwa Hospitali ya Wilaya iwe pia imetekelezwa kwa kiasi hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende pia kwenye eneo hilo hilo la afya katika Wilaya ya Mbinga. Katika Hospitali ya Wilaya kuna tatizo kubwa la mortuary ambayo haijapewa vifaa vinavyostahili ikiwemo fridge. Sifa ya mortuary ni kuwa na fridge na kama haina fridge basi hiyo sio mortuary. Kwa hiyo, niombe kupitia Waziri wa TAMISEMI afanye kila linalowezekana kuhakikisha kwamba katika Hospitali ya Wilaya ya Mbinga kunakuwa na vifaa ambavyo ni fridge na vifaa vingine ambavyo vinastahili katika mortuary hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende pia kwenye eneo la kilimo. Juzi nilisema hapa lakini pia naomba leo niseme labda nikisema sana itaeleweka. Kwenye eneo hili la kilimo katika mkoa wetu nimeshasema sana na nadhani hata Waziri wa Kilimo anafahamu kwamba Mkoa wetu wa Ruvuma ni mkoa ambao unazalisha mazao kwa wingi sana hasa mazao ya chakula. Kwa hiyo, ni vizuri mkoa huu ukapewa kipaumbele kwa kupatiwa pembejeo za kilimo kwa maana ya vocha zikawa nyingi zaidi ya zile ambazo zinapelekwa huko kwa sababu zilizopo bodi hazikidhi. Pia nipongeze mpango huu wa Serikali wa kuhakikisha kwamba unatoa pembejeo za kilimo kwa mpango wa vocha ili kuwawezesha wananchi kujikimu katika shughuli hizi za kilimo ili waweze kuzalisha zaidi. Chagamoto zilizopo ni pamoja na ufinyu huo wa pembejeo lakini pia ni pamoja na kuchelewa kwa pembejeo ambazo zinapelekwa kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hilo hilo kuna changamoto kubwa ambayo imekuwa ni kero sana, wakulima wanakwenda kulima na wanalima vizuri kwa kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa maana ya kilimo kwanza na wamekuwa wakizalisha sana. Shida inakuja wamepata pembejeo na wengine wanajiwezesha wenyewe kwa kununua pembejeo kwa bei ghali hatimaye sasa inafika mwisho wa siku anaporudisha mazao yake kutoka shambani ni tatizo kubwa, ushuru umekuwa ni kero. Kumekuwa na kero kubwa sana ambayo inasababisha hata watu wanaona shida kulima. Mtu analima labda kata fulani, anapotoa mazao kutoka kata hiyo kwenda kwenye kata nyingine katika Wilaya hiyo hiyo kunakuwa na barrier lukuki. Kwa mfano, katika Wilaya ya Namtumbo, ukitoka Mputa kwenda Hanga pana barrier, ukitoka Hanga kwenda Msindo pana barrier, ukitoka Msindo kwenda Lumecha pana barrier, hii ni kero. Pia kuna barrier kati ya Mwanamonga na Mwengemshindo, ni kata hizo hizo tu kunakuwa na barrier karibu 30 katika Wilaya moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali na Waziri wa TAMISEMI ajaribu kuona namna ya kuweka mikakati ya utafutaji wa pesa kuziwezesha halmashauri zake siyo kuwakamua wananchi. Kwa sababu unapokwenda kumkamua mwananchi ambaye amehenya miezi sita ili aweze kupata mazao halafu mwisho wa siku anakuja anakamuliwa kwa kukatwakatwa huu ushuru nalo si jambo jema. Ni sawaswa na mtu una mgonjwa unamuongezea damu huku upande mwingine unampachika mrija wa kumnyonya damu, hii haina mashiko na wala haina afya.