Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Ally Mohamed Keissy

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa nichangie Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nachangia kuhusu mapato. Naomba Serikali irudishe kodi ya mifugo ili Halmashauri zetu zipate pesa za kujiendesha. Miaka ya nyuma kulikuwa na kodi ya mifugo, nashangaa Serikali ikafuta kodi ya mifugo wakati Serikali yetu ni maskini na Halmashauri zetu zinaharibiwa na mifugo lakini hatuna chochote tunachopata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo mifugo peke yake, hata mashamba ya kuku. Watu wanaofuga ng‟ombe mijini wanauza maziwa lazima walipe kodi. Ulaya wanajiendesha kwa kodi, Uingereza hawana chochote siku hizi ni kodi. Nilizungumza hapa hata tv, watu wana tv mpaka 20, 30, Uingereza wanalipa kodi ya tv lakini hapa hakuna mtu analipa kodi ya tv. Kama Serikali Kuu imeshindwa kulipia kodi ya tv, halmashauri zetu zikusanye kodi za tv maana wanajulikana wenye tv 10, 20, alipe kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, utendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi karibu watumishi wote wa Idara ni makaimu muda mrefu. Ujenzi kuna Kaimu, maji kuna Kaimu, utumishi kuna Kaimu, kilimo ni Kaimu karibu idara zote ni makaimu, ndiyo maana utendaji wa kazi unakuwa sio mzuri. Wengine hawana uwezo na kama wana uwezo wapandisheni washike hizo idara tumalizane. Siyo miaka 10, 20 mtu anakaimu, hakuna anayepeleka watumishi kule kwetu. Cha ajabu juzi juzi tu hapa Mkoa wa Rukwa RAS alikuwa amestaafu, wamemfanyia sherehe ya kustaafu, juzi wamesema amerudi tena Rukwa, ndugu zangu si hatari hii? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara. Nimezungumza muda mrefu Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi haina uwezo wa kujenga barabara katika mwambao wa Ziwa Tanganyika inataka nguvu ya Serikali. Akina mama wajawazito wanakufa wakifuata huduma ya afya kwenye vituo vya afya. Kuna kibarabara cha kilometa 35, wananchi wa kule tangu dunia kuumbwa hawajaona hata bajaji, kijiji cha Kazovu, Chongotete, Isaba, Bumanda, hawajaona lolote, wanapata taabu. Ziwa Tanganyika likichafuka hamna msalie Mtume wanazama. Tumekaa hapa viongozi tunajali mikoa mingine, unashangaa mkoa mmoja unapata shilingi bilioni 27, mingine shilingi bilioni sita wakati wana kila kitu. Watu wanaomba lami hata kwenye Wilaya zao sisi hatuna hata barabara za vumbi.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo ni miaka 40 Wilaya Nkasi pale Namanyere lakini hakuna Hospitali ya Wilaya. Wilaya ya Nkasi pale Namanyere leo miaka 40 wanapata maji kwa 16%. Kila siku tunapiga kelele habari ya maji Serikali haisikii. Sasa itakuwa namna gani, tunakuja kutetea wananchi au tunakuja kula posho za wananchi hapa? Kama tumekuja kula posho hakuna haja ya kuwa Mbunge maana hapa tunawakilisha watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haijali Mkoa wa Rukwa kwa sababu hii. Kuna mikoa wamegawa majimbo hata hayastahili kuwa majimbo. Tumelalamika kuhusu Jimbo la Kwela hapa, la Mheshimiwa Malocha lina kata 26, watu 400,000, jiografia yake ngumu ukubwa kama Burundi. Cha ajabu mwaka jana wamegawa majimbo hata hayastahili kuwa majimbo lakini Kwela wameiacha vilevile. Mimi nina kata kule kwangu, Kata ya Nkwamba na Kata ya Kolongwe ni kubwa kama majimbo mengine hata kugawa kata mnashindwa, kugawa tarafa mnashindwa? Mnapendeleana tu, kiongozi akitokea sehemu fulani anagawa anavyotaka, haiji. (Makofi)
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa TASAF. Wengi wamelalamika kuhusu TASAF, kusema kweli TASAF ni donda, ni jipu. Wamepeleka pesa kuwapa watu ambao hawastahili…
MHE. ALLY K. MOHAMED: Wanagawa kwa kupendelea, akiwa Mwenyekiti mjomba wake anampa hata ana miaka 18 anachukua hela ya TASAF. Kwa macho yangu na kwa ushahidi katika Jimbo langu wapo. Hili jambo mfuatilie hatukubali, hela zinakwenda kwa watu ambao wana uwezo. Watu ambao ni yatima, wasimbe sijui wanaitwa hawapati, wanakwenda kupewa watu wenye uwezo miaka 18, 20, watoto wa viongozi, hii haikubaliki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kituo cha afya cha Kirando nimelalamika miaka yote, kimezidiwa na wagonjwa mpaka wagonjwa wanatoka DRC Congo, kipandishwe hadhi kuwa hospitali lakini wapi masikio yamejaa pamba. Ndugu zangu nataka kituo cha afya cha Kirando kipandishwe hadhi kuwa hospitali. Mpaka wakimbizi kutoka DRC Congo wanakuja kutibiwa pale, vijiji vyote vya mwambao wa Ziwa Tanganyika wanakuja kutibiwa pale, hakitoshi, hali ni mbaya. Kimezidiwa sana kile kituo cha afya Kirando, hakifai. Wagonjwa wamekuwa wengi kuliko uwezo wa kituo cha afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Jimbo, ndugu zangu naomba majimbo yapitiwe upya kuhusu Mfuko wa Jimbo. Haiwezekani tupewe pesa zile zile. Mimi mfano jimbo langu kata nzima imeongezwa kutoka jimbo lingine naendelea kupata hela ile ile, itawezekana wapi? Majimbo mengine ndugu zangu tukiyapima humu hayana uwezo. Unakuta Mbunge anasema mimi nataka madawati, wewe una jimbo la kuomba madawati hapa, huna uwezo. Lazima hata haya madawati tunayogawiwa twende kwa vigezo. Jimbo gani ambalo watoto wanakaa chini sana na majimbo gani watoto wana madawati. Tusigawe tu madawati kila mtu sawa, haiwezekani, kuna majimbo mengine ndugu zangu yako taabani hayajiwezi.