Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, lakini napenda pia kumshukuru Mwenyezi Mungu kuweza kunifikisha siku ya leo salama na kuchangia Wizara muhimu sana kwa wananchi wangu wa Mkoa wa Rukwa. Tunapozungumzia kilimo, tunazungumzia kitu muhimu sana ndani ya Taifa letu, tunazungumzia kitu muhimu sana kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa, lakini pia tunatazama hali ya uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika haya mazingira tunapozungumza kilimo kunajambo la msingi ambalo ni bajeti. Bajeti ni tatizo; na hata tutakapochangia mambo mengi hapa tunarudi pale pale kwenye bajeti, tutatoa maelezo mengi ushari mwingi suala linarudi pale pale kuhusu bajeti.

Naomba utakapokuja Mheshimiwa Waziri wa Kilimo utuambie mikakati uliyonayo tofauti na miaka iliyopita. Hali ya chakula umeiona, hali ilivyo mbaya unajua ingawa imefikia mahali sasa mnatoa kauli za kufurahishana tu unamfurahisha aliyekutua wakati wananchi wanaumia, tukizungumza hapa zinakuwa story tu kama story zingine za kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia kilimo; sasa hivi ukiwatazama watumishi wa Serikali hawategemei tu mshahara, wamejiingiza kwenye kilimo kwa sababu wanajua kilimo kinalipa; kilimo ndiyo kila kitu. Sasa kama tutashindwa kuwekeza kwenye kilimo tutaondokaje kwenye hii hali tuliyonayo? Pembejeo ni shida, kuna suala tunazungumzia kila kipindi cha bajeti; Benki ya kilimo. Kama maeneo ambayo yanazalisha hiyo Benki haipo, hata wakulima hawaijui tunamalizaje tatizo hili? Hawajui waanzie wapi wala waende wapi na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kila tunapozungumza majibu yanakuwa ni yale yale. Mimi naomba utakapokuja utuambie angalau mikakati mipya ambayo unayo ili kukitoa kilimo hapa kilipo na hatimaye tuinue uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi kuzungumzia kilimo kwamba wananchi wa Rukwa wananufaika wakati hujawaambia kwamba kwa kipindi hiki ambacho wanategemea kuvuna watauza wapi. Suala la masoko ni muhimu kuliko suala lingine. Sasa hivi tunaendeshwa kwa matamko tu, akipita Mheshimiwa Rais anasema hivi, halafu wewe Waziri wa Kilimo unakuja na matamko mengine, sasa hawa wakulima wamebaki dilemma, yaani hawajui wamsikilize nani? Wamsikilize Mheshimiwa Rais wakusikilize wewe Mheshimiwa Waziri wa Kilimo?

Mheshimiwa Naibu Spika, na haya mambo lazima yawekewe utaratibu. Tunajua itifaki zilivyo, lakini tunapozungumzia uchumi kuna watu ambao ni wataalamu panapokuwa na siasa pia tuwasikilize wataalamu hawa, wakulima tunawakatisha tamaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pembejeo tumekuwa tunalizungumza kila siku na hakuna majibu ambayo yanaonesha mwelekeo moja kwa moja wa kuondokana na haya matatizo ambayo wanayapata wakulima juu ya pembejeo. Tunaomba Serikali ipeleke pesa kwa wale wanaonunua pembejeo kwa wakati ili muda ukifika yale maduka yauze kwa bei ya ruzuku na wasaidie wale wakulima. Nilizungumza hapa, ukitazama Mkoa wa Rukwa mkiwapa pesa wale wakulima wanaopata shida, hawana hata pesa za pembejeo, mkiwapa kipindi cha mwenge hamjawatimizia malengo yao; wapeni kipindi cha kilimo ziwasaidie.

Mheshimiwa Naibu Spika, zitawasaidia wanawake zitawasaidia vijana pia. Kuhusiana na suala hilo utakaa tu wewe na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, mkatoa tu mwongozo ukafika kule. Sijajua Kiswahili ambacho kinaweza kikawasaidia ni kipi kwa sababu kama maneno tunasema mambo mengi tunazungumza lakini bado utekelezaji unakuwa mgumu. Kipindi nasema nakuja kuchangia Mbunge mmoja akaniambia unaenda kuchangia nini? Nikajiuliza maswali kwa nini ananiambia naenda kuchangia nini, nikamwambia naenda kuchangia kilimo; nini kwenye kilimo, bajeti yenyewe ndio hii! Nimetafakari sana, lakini tutasema tu kwa sababu ndiyo kazi yetu kusema, kama mtasikia sawa msipo sikia sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ajira Tanzania ni shida kwa vijana, vijana hawa wanategemea kilimo, kilimo chenyewe kina matatizo, tuambieni hawa vijana mnawapeleka wapi? Yaani kilimo hamjawasaidia, ajira hakuna mnataka waende wapi?

Mheshimiwa Waziri tunaomba mikakati ya kutosha, yaani hali ya kilimo haifurahishi ingawa unakuja hapa unatuambia hali ya chakula iko vizuri, siju iko vizuri wapi? Kwa sababu ukiangalia bei ya mahindi ya mwaka wa jana, bei ya mahindi kwa kipindi hiki sasa msimu huu wa kilimo bei yake unaiona halafu unasema hali ya chakula, Mheshimiwa Waziri unamfurahisha nani yaani?

Mheshimiwa Naibu Spika, yaani haya mambo unakuwa unamfurahisha nani kwa sababu hali halisi inaonekana. Ni bora ukasema ukweli tukusaidie kama suala ni bajeti hupewi pesa sema tukusaidie ndiyo kazi yetu. Lakini ukija hapa ukafanya mambo ya kufurahishana hatimaye tutaanza kuonana wabaya hapa, tunaweza tukakutuhumu kumbe kosa si wewe kosa ni bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la migogoro ya wakulima na wafugaji yaani umekuwa waimbo, hivi mnataka mtuambie kwamba mmeshindwa kabisa kuwa na mikakati ya kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji? Wataalamu wanafanya kazi gani? Yawezekana ninyi ni wanasiasa, wataalam wenu wameshindwa kuwasaidia jinsi ya kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji au mpaka leo hamjajua tatizo lililopo kati ya wakulima na wafugaji ni nini? na kuna migogoro mingine inachangiwa na ninyi wenyewe Serikali kwa kutokufanya maamuzi haraka ya kumaliza midogo kabla haijawa mikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali tena leo yawezekana ikawa mara ya mwisho. Suala la ardhi, ardhi tunajua ni ndogo na watu wanazidi kuongezeka tupeni sasa mikakati ya kumaliza migogoro hii yawezekana ndugu zenu hawajaumizwa, lakini kuna watu wamekufa .
Roho inakuwa inauma tunapokuja kuwaambia nyinyi hamsikii mnataka tuseme nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ningefurahi kama Mheshimiwa Waziri wangu vile ambavyo huwa anaonyesha anasikia tukizungumza leo tunapokuja kipindi kingine tunakuja na kauli nyingine lakini kauli ni hizi hizi na mambo haya haya hivi usikivu unafanyika wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nishauri tu, yale maamuzi ya kwenda kununua ndege yawezekana yalikuwa sahihi, lakini kama kilimo ni kipaumbele maamuzi yale yalikuwa batili. Huwezi kupanda ndege una njaa, huwezi kupanda ndege una utapiamlo, kama kilimo kilikuwa cha kwanza ni bora basi mngechukua nusu kwanza muingize kwenye kilimo na nyingine iende huko kununua hiyo ndege. Kwa sababu tunasema kilimo ndiyo kipaumbele. Sasa maji ni shida, kilimo cha umwagiliaji kinapatikanaje?

Pembejeo ni shida, bajeti yenyewe uliyopewa shida, haya kwenye masoko yenyewe mpaka leo hamjasema lakini toka acha wakulima wauze bei wanayotaka, sawa watauza halafu wakiuza hiyo bei kwa sababu shida sio bei shida ni pesa hakuna hata hiyo bei atakayopanga nani ataenda kununua hela hamna. Kwa hiyo, kunamazingira mengine matamko haya hayasaidii na yenyewe yanatengeneza migogoro tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mabadiliko ya hali ya hewa imekuwa ndiyo kisingizio, hawa watabiri wa hali ya hewa nao wanaweza wakatusaidia au wakatuathiri, kwa sababu wakulima wanapokuwa wanakwenda kulima wanataka kujua mwaka huu mvua ni nyingi au chache, wanatakiwa kuambiwa walime nini kulingana na hiyo hali ya hewa ya kipindi hicho. Sasa hayo mazingira yanapokuwa yanajitokeza na wakulima nao wanaanza kulima kwa mazoea. Ukitazama hii bajeti ina maana kwa kipindi hiki cha mwaka 2016/2017 wakulima walikuwa wanafanya kazi wao binafsi, ni kama Wizara haipo, kwa utekelezaji huu, Wizara haijawasaidia chochote.

Mheshimia Naibu Spika, suala hili sasa hivi mawakala kule Mkoa wa Rukwa hawajalipwa mpaka leo, kuna watu wameuziwa nyumba zao, kuna watu wamefilisiwa. Lakini kosa sio la kwao ni kosa la Serikali kwa nini inashindwa kuwalipa. Mheshimiwa Waziri ni vyema ukawa mkweli na muwazi tukusaidie. Tukiwa tunazungumza hapa masuala ya kilimo uti wa mgongo sijui kilimo kwanza yaani kauli nyingi ambazo haziendani kabisa na mazingira ya kilimo chenyewe kinavyokwenda. Ni vyema mkawa mnatoa matamko yanayoendana na mazingira mliyonayo. Lakini ukisema hamna pesa wala si dhambi kwa sababu utakuwa umesema ukweli… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)