Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi. Kwa namna ya pekee naomba nianze kwa kuwatia shime na kuwapa hongera kubwa sana wewe Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wako, Makatibu Wakuu watatu maana ndiyo Wizara yenye Makatibu Wakuu watatu, hongereni sana kwa kazi pamoja na wataalam walio katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni Wizara kubwa na ningeshauri, Mheshimiwa Jenista wewe ni co-ordinator wa mambo ya Serikali Bungeni. Hii Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ni Wizara kubwa sana, mshauri Mheshimiwa Rais aangelie upya muundo wa Wizara hii. Ni Wizara yenye mambo makubwa na yanayogusa watu wetu kwa asilima zaidi ya
75. Ni Wizara yenye mifugo, kilimo, uvuvi pamoja na taasisi 130 chini yake, lakini ni Wizara moja na ina Waziri mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nafikiri kwamba wakati umefika kwa Bunge hili kupitia kwenu Baraza la Mawaziri mumshauri Mheshimiwa Rais wakati mnakunywa naye chai aangalie namna bora ya kui-restructure. Wizara hii ni kubwa mno na hata kwenye Kamati sisi tunapata shida kweli kwa sababu ina mambo mengi sana na mambo yote yanagusa maslahi ya wananchi wetu ambao ndio wapiga kura wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hilo pia nitoe pongezi nyingi kwa wataalam wetu, Waheshimiwa Wabunge sijui mmeangalia ukurasa wa 42, wataalam wetu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wamepata Tuzo ya African Union kwa kuandika mradi ambao umewezesha Wizara yetu kupata shilingi bilioni 44. Mheshimiwa Waziri hongera sana na wataalam wako, na mimi ningedhani sasa pengine hii ndiyo iwe trend.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Kilimo mna wataalam wengi sana, mna wasomi wengi sana, kuna Makatibu Wakuu wataalam wazuri kabisa, nilikuwa nafikiri hii ndiyo iwe trend sasa kwamba kwenye mashindano kama haya ambayo yanatolewa na AU, hizi nazo ni fursa nyingine za kutuongezea fedha kwenye sekta ya kilimo, hongereni sana kwa kupata shilingi bilioni 44 ambazo zimepatikana kwa kushinda Award ya Global Agriculture and Food Security; watalaam wa Wizara hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa niliseme, jana Mheshimiwa Waziri Mwijage amelisemeaa vizuri, kwamba Serikali hii ni moja maana kuna baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanafikiri Serikali hii ni Serikali ya vipande vipande, kwamba kuna Serikali Wizara ya Fedha, kuna Serikali Wizara ya Kilimo, kuna Serikali Wizara ya TAMISEMI. Serikali ni moja, na kwa ushahidi aliouonesha jana Waziri Mheshimiwa Mwijage na wewe ulioutoa leo umefanya vizuri sana kuondoa tozo zilizokuwa kero kwa wakulima wetu, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kahawa, mimi natoka katika zone ambayo pia tunalima kahawa; tumeshukuru sana hizi tozo 17 ambazo zilikuwa ni kero kwa wakulima wetu, na nina hakika zitasaidia sana kuongeza morally ya kuendeleza zao letu la kahawa. Sasa nina mambo mawili, matatu ya ushauri kwa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ni kuhusu upatikanaji wa mbolea. Mheshimiwa Waziri tumezungumza sana kwenye Kamati, bahati nzuri mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Kilimo. Hili tumelizungumza sana, juu ya umuhimu wa upatikanaji wa mbolea na Serikali mmekuja na mkakati wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja, sisi Wabunge wote tunawaunga mkono kwa asilimia 100. Zoezi hili ni zuri, mbolea hii itatusaidia sana. Jambo ambalo ningeomba tu kulisisitiza ni yale mambo ambayo Mheshimiwa Waziri tuliyazungumza kwenye Kamati ambayo ni muhimu kuyazingatia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, jana nimemsikia Waziri Muhongo anatuhamasisha kuhusu ujenzi wa Kiwanda chetu cha Mbolea kule Lindi na Mtwara, lakini uko ukweli Waheshimiwa Wabunge kwamba kiwanda hiki kimekuwa kinahujumiwa na taarifa hizi ni za uhakika. Sasa nikutie shime Mheshimiwa Waziri wewe na timu yako, wataalam wako wa Tanzania Fertilizers Regulatory Authority wana uwezo mkubwa sana, wasimamie zoezi hili la ununuzi wa mbolea kwa pamoja ili hatimaye bei ya mbolea iweze kushuka na iweze kupatikana katika maeneo mengi ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niweke angalizo dogo tu, kwenye ununuzi wa pamoja kuna changamoto zake kama ambavyo zilikuwepo kwenye ununuzi wa pamoja wa mafuta. Ziko changamoto nyingi na moja ya changamoto kubwa ni hujuma, lazima kutakuwa na watu wenye Makampuni yao watakuwa wanataka kuhujumu effort hii ya kuanzisha bulk procurement. Nikuombe Mheshimiwa Waziri, mambo ya msingi ya kuzingatia iwe ni pamoja na ku-mitigate hizo hujuma, hiyo ni muhimu sana ili isitokee hata siku moja katika nchi yetu tukakosa mbolea eti kwa sababu utaratibu huu wa kununua mbolea kwa pamoja umekuwa na matatizo na umeshindwa kusambaza mbolea katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni matumaini yetu kwamba utaratibu huu wa kununua mbolea kwa pamoja utasaidia mbolea ipatikane kwa bei ya chini kama ilivyo ndoto yetu ya awali, kwamba tungependa mbolea hii ipatikane nchi nzima kama ilivyo Cocacola au vocha ya simu. Nina hakika, Mheshimiwa Waziri bahati nzuri tumeyazungumza kwa kirefu kwenye Kamati kwamba haya yote mtayazingatia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa kushauri na nimelisema sana Mheshimiwa Waziri ni kuangalia uwezekano wa kuwekeza katika Mikoa inayopata mvua ya kutosha na Mikoa hiyo siyo mingine ni Mkoa wa Katavi, Mkoa wa Kigoma na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Kagera. Haya ni maeneo ambayo yana fursa kubwa sana kwa sababu jiografia yake inaruhusu na tumeshazungumza sana, ni matumaini yangu kwamba jambo hili utalizingatia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ametufariji sana juu ya migogoro ya ardhi ya wakulima, wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi pamoja na Mamlaka, Hifadhi za Misitu na Hifadhi za Wanyamapori. Mimi niombe jambo moja, Mheshimiwa Waziri wewe katika jambo hili ni mdau mkuwa sana, jambo hili sasa limalizike. Yale maeneo ambayo yamekosa sifa ya uhifadhi yarejeshwe kwa wananchi ili wayatumie, msing’ang’anie maeneo ambayo hayana faida kwa wananchi wetu. Mheshimiwa Waziri wewe unajua pale kwetu Kasulu kuna hifadhi ya msitu wa Kagera Nkanda, msitu ulioko Makere Kusini, watu wanasumbuka, eneo lenyewe limeshakosa hadhi ya uhifadhi kwa kweli. Ni vizuri maeneo kama haya kama ambavyo tumekuwa tukishauri maeneo yarejeshwe kwa wananchi wayatumie kwa shughuli za kilimo ili waweze kujikimu kwa maisha yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusu upataikanaji wa mbegu. Mheshimiwa Waziri nikukumbushe kwamba kuna shamba kubwa la Bugaga, nitapata comfort sana kama utakapokuja ku-wind up utanieleza namna gani mnajipanga kutumia shamba la Bugaga lenye hekta zaidi ya 1,000. Shamba lile ni kubwa sana, limekaa tu, liko idle. Sisi Halmashauri tulilitoa kwa ajili ya kuzalisha mbegu, lakini shamba hili limekaa halitumiki na kama Wizara hamuwezi kulitumia basi nimeshakwambia siku zote mturejeshee kwenye Halmashauri sisi tulitumie kadiri tutakavyoona inafaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusu Mawakala wa Mbolea kwa masimu wa 2016/2017. Mheshimiwa Waziri umeshatueleza na wadau wamekuja wamezungumza na Waziri Mkuu pia, mmeahidi kuwalipa mawakala wale waliohakikiwa katika kipindi cha mwezi
mmoja, fanyeni zoezi limalizike. Wale mawakala wa mbolea ambao makaratasi yao yako vizuri, ambao hawana matatizo basi walipwe fedha zao, na wale wenye matatizo ndio wasubiri; lakini wale ambao mikataba yao iko vizuri, wamesambaza mbolea kwa wakulima wetu walipwe fedha zao ili kuweza kupunguza tatizo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo linguine, nimeshazungumza a wewe ni kuhusu Chuo cha Kilimo cha Mbondo, tafadhali sana angalia namna bora ya kuweza…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Basi nakushukuru Mheshimiwa Waziri naomba uzingatie Mbondo, ahsante sana.