Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa jitihada kubwa anazofanya kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali wa Wizara yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia hotuba hii nikiamini kabisa nchi yoyote duniani ambayo ina viwanda imara vinavyozalisha, uchumi wa nchi yake utakuwa imara. Nchi yetu ina fursa pengine kuliko nchi zilizo jirani nasi je, tutapataje fedha za kigeni bila kuuza nje? Tuna maeneo mengi ambayo yana fursa ya mali lakini tatizo ni usimamizi ambao siyo mzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo maeneo ya nchi yetu miaka ya nyuma yalikuwa na viwanda, mfano Mkoa wa Tanga lakini viwanda vimekufa, japo nimeona jitihada za kuvirejesha hali hiyo kwa kuona ujenzi wa viwanda vya sementi katika mkoa wetu. Tanga tuna reli inayoanzia Tanga kupitia Moshi, Arusha baadaye Musoma, tukijenga viwanda vingi Tanga na uwepo wa reli ya Tanga tutarejea mafanikio makubwa kwenye fikra ya nchi ya viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, nia ya nchi yetu kuelekea kuwa nchi ya viwanda, bado kuna tatizo la wawekezaji wetu kukosa mazingira au ushirikiano kutoka baadhi ya taasisi zilizo chini ya Wizara, hili litazamwe sana. Mfano yupo mwekezaji ambaye anataka kujenga kiwanda cha mabati, Wilaya ya Mkuranga ameshindwa kuanza uzalishaji kutokana na Baraza la Mazingira (NEMC) kutompa kibali, hili lifuatiliwe kwa karibu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lingine juu ya ugawaji wa fursa hizi katika maeneo ya nchi yetu, baadhi ya mikoa ya nchi yetu ina viwanda vingi kuliko mikoa mingine na si kwa sababu tu maeneo haya yana fursa zaidi kuliko mikoa mingine bali kuna tatizo la kutotoa fursa sawa. Nashauri sana tena sana tutoe fursa sawa kwa kila eneo muhimu, fursa ipatikane eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, Wilaya ya Kilindi ni eneo lenye shughuli kubwa za kilimo, pamoja na shughuli za mifugo. Naomba sana nasi tupewe fursa katika maeneo hayo. Mfano tunaweza kupewa kiwanda cha uchakataji wa siagi kwa sababu tuna mifugo mingi, aidha tunaweza kupatiwa kiwanda cha ngozi kwa sababu tunayo mifugo ya kutosha. Naomba Mheshimiwa Waziri achukue ushauri huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.