Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. JAPHET H. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipatia nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Ofisi ya Rais, Utumushi na Utawala Bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niwapongeze sana Waheshimiwa Mawaziri wote wawili kwa kazi kubwa ambayo wameifanya na ambayo wameendelea kuifanya. Kwa kweli nawapongeza sana tena sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba kuchukua nafasi hii kuipongeza Serikali kwa ujumla, Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imekuwa ikifanya kazi nzuri sana katika kuhakikisha kwamba maendeleo ya nchi hii yanasonga mbele. Kwa kweli hongera sana Serikali ya Awamu ya Tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kuchangia kwanza katika mapato ya halmashauri. Katika taarifa ya Mheshimiwa Waziri ameeleza kwa undani sana hatua ambazo Serikali inakusudia kuchukua ili kuhakikisha kwamba inaimarisha mapato na mimi naunga mkono hizo jitihada ambazo Serikali inategemea kuchukua. Hata hivyo, kuna haja ya kuwa na mfumo mzuri kabisa, mfumo madhubuti wa kuhakikisha vyanzo vyote vya mapato vya Halmashauri vinasimamiwa vizuri. Bila kuwa na mfumo mzuri wa kusimamia mapato, tutapata matatizo makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi Serikali inasema tutaachana na mawakala ambao walikuwa wanakusanya Halmashauri zitaanza kukusanya zenyewe kwa kutumia mfumo wa electronic. Nashauri kwamba wakati tunakwenda kwenye huu mfumo basi ni vizuri Halmashauri zitakapowapangia wale watendaji wanaokwenda kukusanya wahakikishe kwamba wanawapa malengo na malengo hayo yasimamiwe vizuri ili wale watakaoshindwa kufikia malengo wachukuliwe hatua za dhati kabisa. Kwa sababu bila kufanya hivyo usimamizi wa mapato bado utaendelea kuwa mgumu na maeneo mengi kutakuwa na matatizo mengi sana ambayo tulikuwa tunayapata huko nyuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, nimeshukuru suala la property tax kwamba sasa itakuwa inakusanywa na Halmashauri. Mimi nataka niongezee tu kusema kwamba property tax ilikuwa haikusanywi vizuri na ni eneo ambalo lina mapato mengi. Ukiangalia nyumba ambazo zipo katika maeneo ya mijini na maeneo mengine ni nyingi sana lakini nyingi zimekuwa hazilipi property tax. Kwa hiyo, ni vyema Halmashauri ziweke utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba majengo na maeneo yote yanalipa hiyo property tax ambayo itasaidia kuinua vyanzo vya mapato vya Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo napenda nichangie ni kuhusu malipo ya walimu ambao walisimamia mitihani ya kidato cha nne mwaka jana. Walimu hawa walifanya kazi nzuri sana, walisimamia kwa uadilifu, walisimamia kwa uaminifu mkubwa na kazi yetu ikawa imekamilika vizuri. Kwenye Wilaya yangu ya Mbozi wale walimu mpaka leo hawajalipwa, naambiwa walilipwa posho ya siku tatu tu. Hili ni tatizo kubwa kwani linawavunja moyo sana walimu hawa ambao bado wana kazi kubwa sana ya kufanya na kuchangia katika maendeleo ya nchi hii. Juzi Mheshimiwa Waziri alitoa tamko kwamba sasa wanafanya jitihada kuhakikisha kwamba haya malipo yanakamilika. Naiomba Serikali itutamkie ni lini hasa ambapo walimu hawa watalipwa hayo malimbikizo yao ya hela zao za kusimamia mtihani, itatusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine ambalo napenda kuchangia ni hili suala la fedha shilingi milioni 50 ambazo tumejiwekea kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambazo tutapeleka katika vijiji na vitongoji. Hizi fedha zikienda tutakuwa tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa sana, zitatusaidia sana. Hata hivyo tuwe na mfumo mzuri wa kuhakikisha kwamba hizi fedha zitakapokuwa zinatolewa basi wale wanaokopa utaratibu wa kurudisha ieleweke ni wapi watakuwa wanarudisha na wengine watakuwa wanakopa na wengine wanarudisha. Kwa hiyo lazima, tuwe na mfumo ambao unaeleweka vizuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo napenda kuchangia ni kuhusu afya. Kule Mbozi katika Jimbo langu la Vwawa, wananchi wameitikia wito sana wa kujenga zahanati na kushiriki katika ujenzi wa vituo vya afya. Zahanati nyingi zimejengwa ziko zaidi ya 40 na zimekamilika toka mwaka jana mpaka sasa hivi bado hazijafunguliwa. Naomba Serikali ije na mkakati ituambie ni lini hasa hizo zahanati zitafunguliwa ili zianze kufanya kazi kusudi wananchi waendelee kupata huduma zinazostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia napenda kuchangia kuhusu mafunzo ya awali kwa watumishi wa umma. Mafunzo ya awali kwa watumishi wa umma ambao wanaajiriwa kwa mara ya kwanza ni muhimu sana. Hivi sasa tumekuwa tukishuhudia kumomonyoka kwa maadili katika maeneo mengi. Watumishi wa umma wanapoajiriwa wakitoka mitaani wanakuwa bado hawajui miiko na utamaduni wa kufanya kazi kwenye utumishi wa umma. Sheria hii imeweka ni lazima ndani ya miezi sita wanatakiwa wapate mafunzo lakini hivi sasa waajiri wengi wamekuwa hawatekelezi agizo hilo. Naishauri Serikali ni vyema kuhakikisha kwamba ndani ya kipindi kile cha miezi sita wale watu wanapokuwa wameajiriwa kwenye utumishi wa umma wapatiwe mafunzo ili waweze kujua ni namna gani wanatakiwa kuendesha kazi zao na namna gani Serikali inatenda kazi zake. Hiyo itatusaidia sana katika kupunguza matatizo ambayo yamekuwa yaliyopo katika utumishi wa umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo la mafunzo ya awali lakini pia mafunzo elekezi. Mafunzo elekezi ni muhimu sana kwa watumishi wa umma hasa wale ambao wanakuwa wamefikia katika ngazi za kati na wanajiandaa kwenda kwenye ngazi za juu. Bila kupata mafunzo ya uongozi, mafunzo ya menejimenti hawa watu wanakuwa ni vigumu sana kuelewa. Kuna wengine wanakuwa ni wataalam wa fani zingine lakini unapokuwa umepata madaraka ya uongozi unatakiwa uongoze watu, kwa hiyo, ni lazima ujue masuala ya uongozi yanasemaje. Maana unatakiwa usimamie fedha, usimamie mali mbalimbali sasa lazima upate mafunzo ya kutosha kuhakikisha wanatenda kazi zao inavyotakiwa. Kwa kweli nashauri wote wapatiwe mafunzo haya elekezi hiyo itasaidia sana.
MHE. JAPHET H. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.