Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba niipongeze Serikali ya awamu ya tano kwa jinsi inavyofanya kazi vizuri, na Serikali hiyo inayoongozwa na Mheshimiwa John Pombe Magufuli na kama anavyosema sisi Watanzania tuendelee kumuombea na kweli sisi tunamwombea Mwenyezi Mungu amjalie afya ili aweze kuendelea kuwatumikia Watanzania. Nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara ya Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kuendelea na hotuba yangu naomba niunge mkono hotuba hii kwa ajili ya wanawake wa Tanzania. Naomba niunge mkono hotuba hii kwa ajili ya wanawake wa Mkoa wa Kigoma na Wilaya zake zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini naunga mkono bajeti hii? Wakati naunga mkono bajeti hii, naomba bajeti hii iongezewe pesa ili iweze kumkomboa mwanamke wa Tanzania kwa kumpatia maji. Tusipojipanga kuongeza bajeti hii, tujipange kuja na bajeti ya dharura ya kutibu kipindupindu. Kwa maana hiyo, naomba pesa ziongezwe kwenye Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme yafuatayo:-

Naishukuru Serikali kwa sababu mwaka 2016/2017 ilitupangia pesa Mkoa wa Kigoma, nawashukuru kwa hilo. Naomba niseme, pamoja na pesa hizo zilizopangwa, bado lipo tatizo la maji. Kwa hiyo, naendelea kusisitiza kwamba pesa zikipangwa zipelekwe ili kuweza kukamilisha miradi iliyokwishaanzishwa katika Mkoa wa Kigoma. Nimeona wakati Waziri anatoa hotuba yake amesema tumepangiwa pesa nyingine, namwomba Mheshimiwa Waziri pesa hizo zipelekwe ili kuweza kukamilisha miradi iliyopo Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, maji ni uhai. Sisi wote tunafahamu maji ni uhai na maji ni kila kitu. Kwa hiyo, naomba bajeti hii iongezewe pesa kwa sababu wanawake wanapojifungua wanahitaji maji. Wanawake pamoja na watu wengine wanaotunza familia; zipo familia ambazo zina wagonjwa wanaohitaji kutumia maji na wanatumia muda mwingi kwenda kutafuta maji. Wakati mwingine wanatafuta maji na wanakosa muda wa kwenda kufanya shughuli za ujasiriamali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, maji ni kila kitu. Maji yanachangia wananchi kuweza kuongeza kipato chao. Kwa mfano, sasa hivi tunahamasisha vikundi, wanawake waanzishe vikundi. Wakitumia muda mwingi kwenda kutafuta maji, watashindwa kufanya shughuli za uzalishaji na watashindwa kujiunga kwenye vikundi na hata wakijiunga hawataweza kurejesha mikopo katika vikundi vyao kwa sababu muda mwingi watakuwa wanautumia kwenda kutafuta maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, upo mpango wa kutafuta maji kutoka Mto Malagarasi. Kwa sasa hivi, maji katika Mto Malagarasi yanapungua na vyanzo vingi vinaendelea kuharibika kwa sababu wafugaji wanapeleka mifugo kwenye vyanzo vya maji. Naomba basi tunapopanga bajeti kwa ajili ya kupeleka maji vijijini tupeleke na pesa kwa ajili ya kwenda kuhamasisha wananchi kutunza mazingira kwa ajili ya kuhifadhi misitu ili maji yasipotee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mipango mizuri ya kutoa maji Mto Malagarasi lakini tusisahau kufanya mipango ya kutumia Ziwa Tanganyika, kwa sababu Ziwa Tanganyika ni ziwa kubwa ambalo linaweza likasambaza maji maeneo mengi. Maji hayo yakisambazwa katika maeneo mbalimbali, tutafanikiwa katika kilimo cha umwagiliaji. Kwa maana hiyo, Tanzania yenye viwanda itawezekana kwa sababu wananchi watakuwa wanazalisha mazao yao na kupelekea viwanda kuanzishwa kwa sababu vitu ambavyo vitakuwa vimelimwa kutoka mashambani vitakuwa vinapatikana kutokana na kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali ipeleke pesa hizo ili kuweza kukamilisha miradi katika Mji wa Kasulu na viunga vyake ambako bado kuna maeneo yana matatizo ya maji. Mji wa Kibondo nao unahitaji pesa kwa ajili ya kukamilisha miradi ya maji. Vile vile Mji wa Kakonko unahitaji pesa. Kwa mfano, upo mradi mkubwa wa Mgembezi ambapo mradi huo ukikamilika utaweza kuhudumia Kata karibu tano. Kwa mfano Kata ya Kasuga, Kata ya Kakonko, Kata ya Kanyonza, Kata ya Kiziguzigu na Kata ya Kasanda. Kwa hiyo, tunaomba kabisa pesa hizo zikipatikana zielekezwe huko kwenda kukamilisha miradi ambayo tayari imeshaanzishwa. Ipo miradi mingine iliyoanza kutoka miaka takriban mitano hadi kumi, lakini bado haijaweza kukamilika. Tunaomba pesa zikipatikana zipelekwe zikakamilishe miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali iongeze bajeti kwa ajili ya Wizara ya Maji ili tuweze kupeleka maji katika maeneo mbalimbali kumsaidia mwanamke wa Tanzania aweze kupata maji na kumtua ndoo kichwani kama Mheshimiwa Rais wetu alivyoahidi. Nami naamini Rais wetu akiahidi, kwa sababu tumeona mambo mengi aliyoahidi, aliahidi ndege, tayari sasa hivi ndege zipo. Zamani ilikuwa ni shida kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma, lakini kwa ahadi aliyoahidi, sasa hivi bombardier inaenda Kigoma, inaenda Tabora na maeneo mengine. Kwa maana hiyo, naamini hata tatizo la maji litakwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno hayo, naunga mkono hoja.