Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Selemani Said Bungara

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Kilwa Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza natoa shukurani kwa kunipa nafasi hii ili nichangie. Pili, namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameumba mbingu na ardhi ili tuitumie sisi binadamu katika maendeleo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia habari ya maji na kila kiumbe ana asili ya maji, sisi binadamu tumepatikana kutoka na asili ya maji. Hata hivyo miaka 56 ya Serikali ya CCM tunazungumzia habari ya maji. Tunakwenda vijijini kuomba kura ajenda yetu kubwa ni kwamba mkinichagua kuwa Mbunge mtapata maji, miaka 56.

Mheshimiwa Naibu Spika, amesema Mheshimiwa wa Mtama hapa, Ilani ya CCM mliwaahidi Watanzania kwamba mtapata maji kutoka asilimia 67 mpaka 85. Mimi Jimbo langu au Wilaya yangu ya Kilwa maji vijijini ni asilimia 48.3. Tunaomba sana maji safi na salama. Tunaomba sana, bajeti ya maji lazima iongezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ikiwa 2016/2017 tulipangiwa au tulipitisha bajeti ya bilioni mia tisa hamsinitukapata asilimia 19, mwaka huu bilioni mia sita sasa ukipata asilimia 16 utajua mwenyewe itakuwa shilingi ngapi maana itapungua. Naomba sana bajeti hii ya maji irudi iende ikaongezwe fedha kama zilivyoongezwa mwaka jana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia Mradi wa Maji wa Mavuji. Katika bajeti ya 2016/2017, ukurasa wa 142 kulikuwa na mradi wa maji katika Mji wa Kilwa Masoko. Kazi zitakazofanyika ni ujenzi wa chanzo, mitambo ya kusafishia na kutibu maji, ulazaji wa mabomba, ujenzi wa matanki, ukarabati wa upanuzi wa mabomba ya kusambaza maji. Mahitaji ya fedha euro milioni 61.67. Maelezo, majadiliano ya Serikali na Ubeligiji kupitia kampuni ya Aspec international yanaendelea. Usanifu umekamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya! Nataka nijue toka kwa Mheshimiwa Waziri, mazungumzo kati ya Aspec na ninyi yameishia wapi? Mradi huu ungesaidia upatikanaji wa maji katika miji midogo miwili ya Kilwa Kivinje na Mji Mdogo wa Kilwa Masoko, lakini sasa hivi ni miaka mitano maneno tu, maneno tu, kesho, kesho kutwa, kucha maneno tu. Oh haa! Mheshimiwa Waziri leo nataka aniambie mchakato huu umefikia wapi ama sivyo kwa mara ya kwanza nataka nitoe shilingi;.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana. Serikali ya CCM kwa miaka 56 imeshindwa, tunataka kuiangalia Serikali ya Magufuli, maana Serikali CCM haipo, sasa hivi kuna Serikali ya Magufuli. Tunataka tuione Serikali ya Magufuli kwa miaka hii mitano itamaliza tatizo la maji? Kama haikumaliza tatizo la maji katika Tanzania, basi Magufuli bye bye (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana Serikali ya Magufuli ikishindwa kutatua tatizo la maji bye bye mwaka 2020, kwa herini. Waheshimiwa maji si mchezo, huwezi kuishi bila maji, huwezi kulala na mama bila maji. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana, bila maji hakuna kila kitu, watoto hawapatikani bila maji. Tunaomba hilo jambo la maji na hii bajeti lazima irekebishwe ili Watanzania tupate maji. Naunga mkono kabisa; utampata wapi mtoto bila maji? (Vicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kule Kilwa kuna mradi wa maji tangu mwaka 1992, Kilwa sehemu ya Mpala. Watu walitathminiwa lakini tangu 1992 mpaka leo hawajalipwa fidia, mpaka leo! Maji wameyachukua Mpala wameyapeleka Masoko lakini Mpala penyewe pale maji hakuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana katika majumuisho leo Mheshimiwa Waziri aniambie watu wa Mpala fidia yao watalipwa lini? Naomba sana na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji alikuja Mpala na akawaahidi watu wa Mpala kwamba lazima hela zao watapata, nataka nijue leo Serikali sikivu ya Mheshimiwa Magufuli mtoe kauli leo nisikie kama si hivyo sijapata jibu sawasawa nasema kweli Serikali ya Mheshimiwa Magufuli si Serikali sikivu. Kama sikivu kweli nijue kwamba watu wale fidia zao zimetoka au zitatoka lini. (Makofi)

Mheshimia Naibu Spika, naomba sana msimtie aibu Mheshimiwa Magufuli, Magufuli ni mzuri pengine wabaya ni ninyi hapo. Magufuli mzuri ana tatizo moja tu, anabinya demokrasia, hapo tatizo analo, lakini mengine hana matatizo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana; kuna matatizo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)