Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba iliyoko mbele yetu. Niungane na Waheshimiwa Wabunge wote na Watanzania kuwapa pole wazazi wa watoto wetu ambao wametutoka kule Arusha, Mwenyezi Mungu awape faraja na awapumzishe watoto wetu kwa amani.

Mheshimiwa Naibu Spika, natamani sana akinamama tungeungana leo, ukiwepo na wewe Mheshimiwa Naibu Spika, kwa dakika moja angalau tuangue kilio kwenye Bunge hili kwa niaba ya akinamama wa Taifa hili wanaoteseka na kuhangaika kwa adha ya maji kwenye nchi nzima.

(Hapa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walitoa sauti ya kilio kwa niaba ya akinamama wanaohangaika kwa adha ya maji)

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania shida ya maji ni kubwa kupita maelezo. Ukiangalia hivi vitabu vya maji kwa miaka karibu mitatu, minne iliyopita unakuta mambo mengi yanayojirudia ni yale yale.

Kiukweli ni jambo la ajabu, Watanzania wanaongezeka kwa milioni moja kwa mwaka. Wakati watu wanaongezeka, mahitaji ya maji yanaongezeka, bajeti ya maji inashuka; haingii akilini kabisa. Kwa mwaka mmoja tunaongezeka watu milioni moja Tanzania na Mheshimiwa Waziri kasema, yaani hata ule uwezo wa ongezeko la watu, tofauti na namna ya kuweza kumudu gharama za huduma kwa wao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini mahitaji yanaongezeka wakati huo bajeti inapungua? Wale wanaoongezeka hawahitaji kunywa maji? Hakuna kitu muhimu kwa Mtanzania na mwananchi yeyote wa Tanzania na binadamu yeyote kama maji. Kwa hiyo, tunaomba sana suala la bajeti ya maji iongezwe, hakuna discussion, liongezwe kwa sababu watoto wa Tanzania wengi hawaendi shule kwa sababu ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, akinamama wanaamka saa 10.00 ya usiku kufuata maji visimani, wengine wanabakwa. Huwa tunasema, hatufichi, wanabakwa usiku wakifuata maji kwenye visima; watoto wanachelewa shule hawapati elimu wanayostahili. Suala la maji lazima Serikali ije na mkakati maalum wa namna ya kuhakikisha akinamama wa Tanzania wanapata maji ya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa Malagarasi. Nimewahi kusema Bungeni hapa mara nyingi, karibu miaka mitano sasa. Ardhi ya Kaliua na ardhi ya Mkoa wa Tabora haiwezi kuchimbwa maji kwenye ardhi yakapatikana, ndiyo maana kwa Kaliua nzima na hata Urambo hatukunufaika na mradi wa World Bank kwa sababu, visima vingi vilivyochimbwa havikutoa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haijasema njia pekee ya kutupatia maji Kaliua, Urambo na Nguruka ni kutupatia maji ya Malagarasi. Tangu miaka mitatu iliyopita, kuanzia 2014 tunaambiwa utafiti unafanyika, leo tunaambwa kwamba mpango unafanyika ili kumpata mshauri mwelekezi haweze kufanya environmental impact assessment, wakati huo akinamama Kaliua hawana namna.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nategemea angalau wangetuambia mwaka huu tumetenga angalau kuanza zile hatua za awali; lakini Mheshimiwa Waziri hata shilingi. Bahati nzuri hata nimeongea naye hata kabla ya bajeti hii; anasema wanategemea kutafuta fedha. Miradi inayotegemea sana fedha kutoka nje nyingi haitekelezeki. Kwa adha wanayopata akinamama wa Kauliua, Nguruka na Urambo ningetegemea Serikali itoe kipaumbele kwa fedha ya ndani ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwa Serikali imezindua miradi miwili ya Mkoa wa Tabora, Mradi wa Victoria na ule Mradi wa pale Mabama, Kaliua na Urambo hawamo, sisi hatumo kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa taarifa ripoti aliyoandikiwa Mheshimiwa Waziri, pengine ameandikiwa hakujua; kwamba mradi uliozinduliwa pale Mabama unalisha wilaya zote saba za Tabora si kweli, ni pale Uyui tu na ni baadhi ya vijiji, siyo vyote, lakini ripoti inasema Wilaya zote saba zitanufanika na mradi uliozinduliwa Mabama, kitu ambacho siyo kweli na kama ni kweli basi watuambie ndani ya Kaliua ni vijiji vingapi vimeingia kwenye mradi wa pale Mabama na pale Uyui?

Mheshimiwa Naibu Spika, inasikitisha, tutalia mpaka lini hapa Bungeni, ni kweli tulikuwa tunategemea mwaka huu uwe ni mwaka wa matumaini kidogo kwa wananchi wa Kaliua. Kweli naomba Mheshimiwa Waziri bajeti hii ikiisha twende na yeye Kaliua akawambie Wanakaliua wanapata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mifumo ya Maji Taka na Safi. Ni kweli kwamba kwa maeneo ambayo yameunganishwa na maji taka mifumo yake imechakaa na mingine imeoza. Nikianzia hapa Dodoma, wananchi wanalipa gharama kwa ajili ya maji taka kila bili inapokuja lakini mabomba yamepasuka yanavuja ovyo na bahati mbaya sana wakiitwa kuja kurekebisha wanachukua zaidi ya miezi miwili, miezi mitatu, wananchi wana adha kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujua zile fedha zinazolipwa kwenye kila bili kwa ajili ya maji taka nilijua ni kurekebisha mifumo iliyooza, kuondoa mabomba yaliyochakaa kuweka mabomba mengine lakini mabomba ya miaka thelathini yako pale pale tunalipa gharama tunapata usumbufu kila siku ni gharama.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri atakapo-wind up atuambie kwamba lini mifumo ile ya maji chafu kwenye maeneo ambayo kumeunganishwa system ya maji chafu itaondolewa na kuwekwa mingine kwa sababu ile iliyopo imechoka imeoza na inaleta shida kwa wananchi karibu kila siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, Upotevu wa Maji. Hotuba ya Mheshimiwa Waziri anasema upotevu sasa hivi ni asilimia 38 na hivyo imepungua. Upotevu wa maji ni mkubwa kweli kweli na kwa bahati mbaya bomba linaweza likapasuka katikati ya barabara Mawaziri wanapita pale, viongozi wanapita pale, inachukua almost miezi mitatu wakati maji yanatiririka, yanapotea Watanzania wengine wana-share maji na ng’ombe kwenye vijiji vya maeneo mbalimbali. Nikikutana na maji yanayomwagika mahali huwa naumia sana; kwa sababu nawaangalia wananchi wangu wanavyotesa nikikuta maji yanamwagika huko barabarani roho inauma sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo bado Serikali lazima inatakiwa iweke mifumo. Standard inayotakiwa kitaifa upotevu wa maji ni asilimia 14, kwa hiyo sisi asilimia 38 bado ni kubwa sana. Maji mengi tunayagharamia lakini yanapotea barabarani wakati huo huo kilio cha maji kinaongezeka kila kukicha; kitu ambacho ni hasara kwa Serikali na ni maumivu kwa Watanzania ambao hawana maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Gharama za Kuunganisha Maji. Gharama hizi zinazidi kuongezeka kila siku na zinakuwa kubwa kiasi kwamba mwananchi wa kawaida; kwa mfano hapa Dodoma gharama za kuunganisha zimezidi kuongezeka. Mwanzo utaratibu ilikuwa Mwananchi ananunua vifaa anakwenda kulipa gharama kule DUWASA anakuja kufungiwa maji.Leo unaambiwa ukalipe moja kwa moja kila kitu kule. Nimejaribu kwenda mimi mwenyewe, unajaribu kuangalia gharama ulizoandikiwa milioni moja na ushee wananchi wangapi wa hali ya chini wanaweza kuvuta maji? Ni wachache.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile ukiangalia vile vifaa bei ya madukani na bei ambayo umeandikiwa pale ni tofauti. Kwa hiyo, naomba suala la maji si biashara, maji ni huduma. Kila Mtanzania apate maji. Kwa hiyo tatizo la kuweka gharama kubwa wananchi wengi wanashindwa kugharamia ni maumivu kwa Watanzania lakini pia tunafanya huduma ya maji kuwa ni biashara na si huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho, Madawa ya Kutibu Maji. Tumekuwa tukilalamika hapa Bungeni miaka mingi gharama za madawa ya kutibu maji inakuwa ni kubwa kiasi kwamba kuna maeneo mengine kuna wakati inafika maji yatoka machafu, yanatoka yananuka, yanatoka yana udongo kwa sababu halmashauri na miji zinashindwa kumudu gharama, matokeo wanaweka dawa kidogo wananchi wanakunywa maji machafu. Kwa hiyo naiomba Serikali, kwa kutambua umuhimu waweze kupunguza gharama za kutibu maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, ahsante.