Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Naibu Spika, leo sikupanga kuzungumza lakini nimeomba kuzungumza kutokana na hali halisi ya bajeti ya Wizara ya Maji.

Kwanza kabisa kwa mara nyingine binafsi kama Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, napenda kumshukuru sana Mheshimwa Rais kwa uteuzi wa Profesa Kitila Mkumbo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji. Ninaamini kabisa kwamba kutokana na uwezo wake, umahiri wake na weledi wake ataweza kuisaidia nchi na ujumbe utakwenda duniani kwamba ndani ya Vyama vya Upinzani kuna watu wazalendo na uwezo wa kufanya kazi, ninamtakia kila la heri Profesa Kitila. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo kubwa ambalo tunaliona na naomba Waheshimiwa Wabunge tuelewane katika hili, Mheshimiwa Rais alikuja hapa Bungeni, katika moja ya jambo ambalo lilikuwa ni very emotional kwa Watanzania ni pale Rais alipoahidi kuwatua akina mama ndoo kichwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona Makamu wa Rais akizunguka kila kona ya nchi hii kufanya kazi hiyo, hata bajeti ya mwaka jana picha iliyokuwa mbele ya kwenye bajeti ilikuwa ni picha ya Makamu wa Rais anamtua mama ndoo kichwani, lakini kwa masikitiko makubwa sana bajeti ya Wizara ambayo ndiyo inawahusu Watanzania moja kwa moja imeshuka kutoka bilioni 915 za maendeleo mpaka bilioni 623 za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unatafsiri vipi uwekezaji wa rasilimali fedha namna hii kwenye ajenda ya kuwashusha na kuwaondolea kina mama ndoo kichwani. Waheshimiwa Wabunge nilikuwa nawaomba kwa siku tatu hizi za bajeti hii, najua tuna kero zetu kwenye majimbo, najua tuna matatizo kwenye mikoa yetu na kila mtu ataanza kuongelea mradi wake, iwapo hatutaungana pamoja na kutaka bajeti ya Wizara hii irudishwe angalau kwa mpango ule wa mwaka jana, hayo malalamiko yote mtakayoyatoa kwenye majimbo yenu hayatakuwa na maana yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Bunge tunayo hayo mamlaka, Kanuni za Bunge zinaturuhusu kuitaka Serikali ikapange upya bajeti hii, kama unaguswa na kero ya maji kwenye eneo lako, kama unaguswa na kero ya maji kwenye mkoa wako au jimbo lako au kijiji chako una njia moja tu ya kufanya ya kumsaidia Waziri bajeti hii iende ikaandikwe upya, tupate bajeti angalau ile ya mwaka jana iweze kurudi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo siyo la Vyama, wanaoumia na maji ni watu wa vyama vyote na watu wasio na vyama vilevile. Nimeomba dakika hizi tano kwa ajili ya kui-set hiyo trend na tuweze kuiambia Serikali, kuna mapendekezo mengi Kamati ya Maji imetoa maependekezo kuhusiana na Rural Water Agency, imetoa mapendekezo kuongeza fedha kwenye mafuta kwa ajili ya kuweza kuelekeza maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hiyo bajeti ya mwaka jana ya bilioni 915 ni asilimia 19.8 tu ya miradi ya maendeleo ndiyo imepelekwa kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ambayo imetueleza hapa. Hata Waziri mwenyewe kwenye hotuba yake ukurasa wa 120 ameeleza, tuchague, tupige kelele humu ndani, tulalamike, halafu tuonekane tumesemea watu wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, au tuchukue hatua ya kuhakikisha kwamba bajeti ya Wizara ya Maji inakwenda kurudishwa angalau kwenye kiwango cha mwaka jana. Naomba Waheshimiwa Wabunge huo ndio uwe mjadala wetu na huko ndiko ambako twende, tuweze kuwatua akina mama ndoo kichwani. Ahsante sana.