Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. BAL. ADADI M. RAJABU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kupata muda huu kuweza kuchangia hii hoja muhimu sana ya viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais na Awamu yake ya Tano, kwa kuweka msisitizo mkubwa sana kwenye viwanda. Viwanda ni kitu muhimu sana kwenye nchi yoyote na ndiyo vinavyokuza pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na shukurani hizo lakini mtakumbuka kwamba viwanda vingi kwenye hii nchi vilikuwa Tanga. Tanga ilikuwa ni kitovu cha viwanda, lakini viwanda sasa hivi Mkoa wa Tanga vimekufa kabisa. Sasa nilitegemea Mheshimiwa Waziri alipoingia madarakani kitu cha kwanza kingekuwa ni kufufua vile viwanda vya Tanga ambavyo vilikuwa zaidi ya 1000. Kwa hiyo, tulitegemea kuna mikakati madhubuti ya kufufua vile viwanda. Kulikuwa na viwanda vingi tu vya chuma, sabuni, mbolea na vitu vingi tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa hivi sijaona juhudi zozote za kufufua vile viwanda, lakini namshukuru kwa kutuletea kiwanda kikubwa sana ambacho kitaweza kutoa tani milioni saba kwa mwaka, Kiwanda cha Hengya na nimeambiwa kufuatana na taarifa yake kwamba wawekezaji wenyewe wako hapa Bungeni. Nawashukuru sana na nawahakikishia kwamba, wawekezaji hao waje Tanga na hawatapata matatizo yoyote na najua kabisa Mkuu wetu wa Mkoa wa Tanga yuko China kwa ajili ya ku-facilitate kiwanda hicho kiweze kuja Tanga. Karibuni sana Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Muheza sasa hivi sisi tumeshajitayarisha, tuna ardhi kubwa sana. Tuna ardhi ambayo sasa hivi tunasubiri mtuletee viwanda, tunafanya juhudi kubwa sana za kutafuta viwanda vya matunda; kutafuta wawekezaji wa viwanda vya mihogo pamoja na viwanda vya kuwekeza mipira, hizi pilipili manga pamoja na karafuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ardhi tunayo na nilishamwambia Mheshimiwa Waziri na tujitahidi kwa uwezo tuweze kupata wawekezaji wa kuweza kusaidia kupata hivi viwanda hasa vya matunda pamoja na mihogo. Juhudi bado zinaendelea na mazungumzo bado yanaendelea na insha Allah pengine tunaweza kufanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamefunguliwa viwanda vingi hapa karibuni, viwanda vya matunda, lakini ningependa kumshauri Mheshimiwa Waziri kwamba, wawekezaji wanapokuja asiwaelekeze kwenye sehemu moja tu, ajaribu kuwaelekeza kwenye sehemu zile ambazo zao linatoka. Zao la matunda linatoka Tanga (Muheza). Kwa hiyo, ningeshukuru sana alete wawekezaji au wa mihogo Muheza, tunayo ardhi kubwa sana kwa ajili ya viwanda na kulima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, TIC au EPZA. Vituo hivi ni muhimu sana kwenye nchi yoyote ile. Vituo vya TIC, EPZA, panapotokea ukorofi, ucheleweshaji wowote kwenye vituo hivyo, wawekezaji hapa ndipo wanapoweza kutoroka na kuondoka kwa kuwa vituo hivi ndivyo vinavyopokea wawekezaji. Sasa, niliwahi kuzungumza mwaka jana hapa kwamba, Kituo cha TIC lazima pawe na Land Bank, mwekezaji anapokuja hataki usumbufu, yeye anataka kuambiwa maeneo ni haya, ni haya, ni haya, wekeza hapo. Sasa utaratibu wa kusema watu binafsi ndio wawekeze pale, una land yako unakwenda kuingiza kwenye TIC inaleta usumbufu. Ni lazima Serikali sasa hivi kuptia Wizara ya Ardhi itoe ardhi TIC, ni lazima itoe ardhi EPZA ili mwekezaji akija aende moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mara ya mwisho mimi kwenda TIC baada ya kupeleka wawekezaji pale, kulikuwa na vibali zaidi ya kumi na tano. Sasa sijui sasa hivi hivyo vibali vimepunguzwa kwa kiasi gani, lakini unaposema One Stop Centre ni lazima iwe One Stop Centre kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nenda Mauritius Enterprise, wao wana-time frame; mwekezaji anapokwenda pale ilikuwa 2400Hrs lakini wamepunguza mpaka 0600Hrs; kwamba kila kitu Residence Permit, Working Permit, viwanda, sijui leseni vyote vinafanyika katika siku moja. Sasa mwekezaji anataka kitu kama hiki na ndiyo maana kwenye ripoti za transparent international dhidi ya good governance na corruption, Mauritius na Botswana wamekuwa wanaongoza kwa miaka mingi na ni kwa sababu ya TIC yao, Mauritius Enterprise, ukienda Botswana TIC yao, hakuna usumbufu watu wanapata vibali mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ningeshauri kwamba, Mheshimiwa Waziri aangalie vibali gani pale vinaleta usumbufu, atoe vile vibali weka vibali vichache. Mwekezaji hapendi usumbufu atoke hapa aende sijui biashara, atoke hapo aende sijui immigration, atoke hapo aende wapi! Anataka kila kitu akikute pale pale na hapo ndipo tutakapoweza kupata wawekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kuna taarifa wawekezaji wanaondoka, ni kweli? Ningependa hiyo taarifa labda Mheshimiwa Waziri aje ui-clarify wakati atakapokuja ku-wind up kama kweli wawekezaji wetu wanaondoka kwa sababu ya huu usumbufu ambao ni unnecessary ambao upo sehemu mbalimbali? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana nilimwomba Mheshimiwa Waziri kwamba Kiwanda cha Kamba, Tanga kina mashine nzuri na kinatoa mali ambazo zinanunuliwa hata nchi jirani. Nikaomba kwamba, Serikali sasa hivi basi iwape zabuni wale Kiwanda cha Kamba, wanatengeneza mazulia mazuri sana, ili mazulia yote ambayo yanatengenezwa, basi wapewe zabuni Tanga ili waweze kuzalisha na kuweza kuinua kile kiwanda. Sasa hivi kinatoa vizuri na kinataka kuleta mashine nyingine ambazo ni nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ningependa kushauri tu kwamba, ili kuleta wawekezaji, najua kwamba wanatumia Mabalozi nje, lakini ni vizuri wakaweka ma-trade attachee kwenye sehemu zile chache ambazo wanaona kwamba, kuna wawekezaji wengi ambao wanakuja. Wapeleke hawa ma-trade attachee watakaa kwenye Ofisi za Ubalozi na watakuwa specifically kazi yao iwe ni hiyo na wawape assignment kubwa, tutakuwa hatupati hasara, lakini nina hakika kabisa kwamba kuwepo kwa ma-trade attachee kwenye Balozi zetu kutasaidia sana badala ya kuwaachia hilo jukumu Mabalozi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga hoja na nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)