Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipatia nafasi hii na nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, aliyenijaalia kupata afya njema na kuwepo katika kuchangia hoja iliyokuwepo mezani.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mtanzania na napenda maendeleo ya Tanzania na napenda Watanzania iwe mweusi, iwe mweupe, mwenye rangi ya kijani, tuwe na maendeleo ambayo yanawiana. Nataka nitoe pongezi zangu za dhati kwa baadhi ya wawekezaji wa Kitanzania ambao wameonesha kuwa wana uwezo wa kuweza kufanya biashara na wana uwezo kuingia katika uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 20 Mwezi Aprili, kulifanyika mkutano mkubwa sana Nairobi wa African Urban Transport. Nataka kuwapeni taarifa Wabunge mwendo kasi UDAT imepata tuzo namba mbili. Yule ni Mtanzania kama ana mahali amekosea basi inabidi arekebishwe lakini ameonesha uwezo mkubwa na wameambiwa Wakenya, Waganda, Wazambia, Waethiopia na tumewaona wamekuja kujifunza Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya ndiyo maendeleo ambayo unayaona yakiwekezwa kwa ngozi nyeusi na Watanzania basi maendeleo haya yatakuwa yana uwiano, na pesa yetu badala ya kuipeleka nje, itabakia Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpongeze tena Reginald Abraham Mengi na yeye ameonesha uwekezaji wake unamsaidia na unamgusa mtu mwenye ngozi nyeusi na ajira kubwa zinakwenda kwa watu wenye ngozi nyeusi. Nampongeza Bakhresa, kazi yote na fedha zinazopatikana za Bakhresa zinabakia Tanzania na unaona hata nyumba zao na investment zao zinawagusa Watanzania na wengineo. Hii maana yake Nigeria waliwatengeneza watu weusi 150 mmojawapo akiwa Dangote ambaye anakuja kuwekeza Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaingia katika ulimwengu wa viwanda, tumewaandaa vipi Watanzania wenye ngozi nyeusi ambao ndio maskini zaidi ili waweze kuingia katika uwekezaji? Ni matumaini yangu, tusijibeze sisi wenyewe tunaweza. Mwanzo hatukuwa na elimu lakini sasa hivi tumepata elimu, watoto wetu hawa baadaye ndio wataokuwa akina Dangote wa Tanzania. Tusiwakatishe tamaa tuwape nguvu ili wazidi kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Lindi, Mtwara na Ruvuma tumeonesha mabadiliko makubwa sana. Mwaka jana nilimuuliza swali la papo kwa papo Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhusu tozo na kero ya korosho. Katika usimamizi bora unaofanyika tumepata korosho kilo moja kwa Sh.3,800, ilikuwa ni dhahabu ya kijani imewezesha kuiingizia Tanzania dola za Kimarekani 346,000,000 katika mnada wa kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pesa hizi ukizigawanya au ukazipigia hesabu kwa Tshs tumefanya mafanikio makubwa sana. Tumedhulumiwa kwa muda mrefu na wafanyabiashara wa mazao. Ningeomba speed hii iliyokwenda kwenye korosho iende kwenye kahawa, tumbaku, ufuta, mbaazi na alizeti ili Watanzania hawa ambao ni maskini waweze kufarijika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zao la korosho linastawi Pwani yote mpaka Zanzibar. Tuko kwenye Muungano, tusiiache Zanzibar nyuma katika kuondoa umaskini tukawa sisi peke yetu tunaendelea. Hii korosho inapatikana Madagascar, Comoro na Seychelles. Nilitegemea kwa upendo wetu tuliokuwa nao katika Muungano basi na korosho ipelekwe na kuhamasishwa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, korosho yetu imeingia dosari kubwa kwa wafanyabiashara ambao wana mazoea. Baada ya kuona tumepata soko la Vietnam wafanyabiashara wakubwa wa mazao wamezuia makontena wanaya-hold ili yule anayenunua korosho asizipeleke tena nje, hii ni dhuluma kwa Watanzania. Wamekuwa matajiri kwa kupitia Tanzania, leo wao wanakuwa matajiri hawataki waone uchumi wa Tanzania unaruka kwenda mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Waziri mwenye dhamana aliangalie hili na awaangalie wanaofanya mchezo huu, uishe. Hili ni tambazi, maana kama ni jipu limevilia limekuwa ni tambazi, nataka tuhame kutoka katika majipu tuyapasue matambazi ambayo yamezoea kutukamua na kutunyonya nchi hii ili tusiweze kutoka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda ambavyo vilibinafsishwa nataka aniambie Mheshimiwa Waziri, je, hivi viwanda vimebinafsishwa au vimeuzwa? Kama vimeuzwa nani amenunua na kama amenunua mbona havifanyi kazi zaidi ya miaka 20?

Mheshimiwa Naibu Spika, amezungumza ndugu yangu Mwambe, huyu Mwambe ana uchungu na korosho. Kiwanda cha Lindi kimefungwa, Kiwanda cha Mtwara kimefungwa, Kiwanda cha Masasi kimefungwa, Kiwanda cha Newala kimefungwa, Kiwanda cha Kibaha kimefungwa, wao wanachukua zile korosho wanakwenda kupeleka ajira kwao, kwa nini? Hamwoni kama Mkoa wa Lindi hakuna kiwanda hata kimoja? Tutapataje utajiri katika hali ngumu ya kimaskini kama hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, tumefikia mahali tunajiuliza hivi Lindi kweli mkoa wenye majimbo nane hatuna kiwanda hata kimoja. Kama Waziri ananibishia, aniambie Lindi kuna kiwanda fulani, hakuna, vyote havifanyi kazi, ina maana tunatengeneza umaskini Mkoa wa Lindi na Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mjumbe katika Kamati ya Uwekezaji. Nimeangalia katika makosa ambayo tumeyafanya nchi hii ni kwamba hatuna sera. Kama hatuna sera tumeingiaje katika uwekezaji wa viwanda? Tunakwendaje na maendeleo ya viwanda wakati hakuna sera? Sera ni usukani, utatoa sheria, taratibu na kanuni, hatuna. Sasa hivyo viwanda 200 vinavyokuja sheria gani itasimamia? Utaratibu gani utasimamia? Kanuni gani itasimamia? Tutarudi kule kule. Hivyo naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuleta majibu aniambie kwa nini sera ya viwanda haijakamilika mpaka leo. Tunakwenda katika ulimwengu wa viwanda, tunaendaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikwenda mpaka kwenye madini. Tulienda katika Idara na Maendeleo ya Madini bila kuwa na sera. Tulitembelea Buzwagi hakukuwepo na sera, wamechimba mahandaki, watu wengine wameshamaliza kuchimba madini, tumeachiwa malaria katika Mikoa ya Geita, Simiyu na Mara. Ndicho tunachokataa hiki, tunataka sera ije iweze kuwakamatia wale ambapo katika upande wa environmental impact assessment.

Mheshimiwa Naibu Spika, ifikie mahali tujiulize tumelogwa na nani? Wanatuambia wenyewe, nilikaa na mtu mmoja akaniambia Tanzania is a sleeping giant na tunajitambua kabisa kama tuko sleeping giant. Kama tungekuwa si sleeping giant tungekuwa na sera sasa hivi, lakini mpaka leo tunakimbizana na viwanda lakini hakuna sera. Leo unaposema mimi mtaalam unakuja kunielimisha nini wakati huniambii nitafanya nini? Nenda TPDC, walikuja kwenye Kamati wakiwa hawana sera, strategic plan, wala action plan, kutakuwa na commitment hapo?

T A A R I F A . . .

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa ya Mheshimiwa Ally Saleh, namwambia kitu kimoja, bahati nzuri nilikwenda Lima Peru, nimetembelea mpaka Mexico walifanya makosa haya sasa hivi zile nchi ziko polluted kwa vile hawaku-update hizi sera zao, wakajiingiza katika mikataba na sheria mbovu na kuiweka nchi katika umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia madini. Leo tunaletewa na STAMICO kuwa kuna baadhi ya mashirika ambayo yameingia ubia na madini, kwa vile hakuna sera, amefanya feasibility study na…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru, sina lingine. Ahsante sana.