Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Julius Kalanga Laizer

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninakushukuru kwa kunipa nafasi, naomba Waziri atakapokuja kuhitimisha hapa aniambie ni lini wananchi wa Lokisale, Mswakini na Lemoti, ambao mazao yao yaliharibiwa na tembo takribani kwa mfululizo miaka kumi sasa mpaka siku ya leo Serikali haijawalipa, ni lini Serikali watalipwa fidia zao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeendelea kuwa wahifadhi wazuri na ndiyo maana sisi hatuli nyamapori, lakini kama wanyama wenyewe wanakuja kula mazao yetu na Serikali haioneshi kujali tutapata ukakasi katika kuwalinda wanyama hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimesikia mtu mmoja akichangia akisema watu wa Ngorongoro wametoka 8,000 wamekuwa 90,000. Kabla hatujahoji idadi ya Watanzania walioko Ngorongoro ambao ni haki yao na wala siyo hisani kwa sababu ni Watanzania wenzetu, ni muhimu pia tuhoji miaka hiyo na leo wanyama walioko Ngorongoro ni wangapi na wameongezeka kwa kiasi gani na ni lini jamii yetu imehusika? Tuambiwe hata Mmasai mmoja aliyehusika kufanya ujangili katika Hifadhi ya Ngorongoro?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hamuwezi kutuhukumu kwa kuwaangalia majangili ambao ninyi mnawafahamu na Serikali imeshindwa kuwashughulikia. Tunataka mtuambie ni lini jamii hiyo imehusika katika kufanya ujangili kwa wale wanyama, kama kweli hoja yenu ni ya ujangili? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nashukuru kwamba leo watu wa Kaliua wameguswa, kwa sababu mara zote tunasema wananchi wa Ngorongoro wanaokaa kule wana haki kwa sababu ni ardhi ya vijiji. Leo wananchi wa Kaliua nao wameguswa, nashukuru sana Mheshimiwa Mbunge mwenzangu nae anakubaliana kwamba vijiji vilivyosajiliwa wapate haki kwa sababu vimesajiliwa na viko kihalali. Ni vizuri kwa sababu wameguswa, tutaendelea kuwa wengi tunaotetea maslahi ya Watanzania wenzetu.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niihoji Wizara, hivi lengo la Wizara ni uhifadhi peke yake au lengo la Wizara ni kuhakikisha kwamba uhifadhi na maisha ya Watanzania yanaendelea kuongezeka? Maana leo ardhi haiongezeki, lakini hatuwezi pia, kubadilisha nchi hii ikawa ni nchi ya uhifadhi peke yake. Haiwezekani tukawa na uhifadhi bila watu, hata haya mapato tunayopata kutokana na wanyama, kama hakuna Watanzania watakaohudumiwa na fedha hizo, hakuna sababu ya kuwa na uhifadhi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninadhani ili jambo hili liende vizuri ni lazima tujue kwamba, katika maeneo ya uhifadhi kuna watu pia na kuna wanyama. Tujenge mazingira mazuri ya kupanga matumizi bora ya ardhi ili wote tuweze kunufaika na ardhi hiyo. Tatizo hapa ambalo ninaliona Wizara haipo tayari kushirikiana na wananchi kutatua migogoro iliyoko katika maeneo ya uhifadhi. Inaonekana Wizara inatumia nguvu kubwa, inatumia Jeshi, inatumia Polisi, katika kuumiza na kuua wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali leo ituambie, hivi ni Serikali imebariki maumivu na mateso ya wananchi katika maeneo ya uhifadhi? Kama Serikali haikubaliani na uonevu na maumivu wanayopata wananchi wetu, hao askari wanaotesa watu na kuua watu, wanapata wapi mamlaka ya kufanya hivyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali haikemei, na mimi nadiriki kusema kama Serikali haikemei uonevu na mauaji yanayofanyika kwa raia, maana yake Serikali imebariki uonevu na mauaji ya raia walioko katika maeneo ya hifadhi. Haiwezekani watu wauawe tu halafu Wizara imekaa kimya, Serikali imekaa kimya! Wabunge tunapiga kelele hapa, halafu tuseme Serikali haijabariki! Mimi naamini kama Serikali haitoi kauli maana yake Serikali imeagiza polisi na Askari wa Wanyamapori waue raia katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie katika suala la uporaji wa mifugo katika maeneo ya uhifadhi. Kama walivyosema Wabunge wenzangu, hivi nani anayeharibu misitu kati ya ng’ombe na wakata mikaa? Hivi nani anayeharibu misitu kati ya wafugaji wanaofuga ng’ombe tu na wale wanaochoma mikaa na mikaa mmetoa kibali inauzwa kila mahali kwenye nchi hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu Serikali i-admit leo, kama Serikali ina chuki na uadui na wafugaji, tujue kwamba Serikali haitaki ng’ombe kwenye nchi hii. Jana tulikuwa tunajadili bajeti ya Wizara ya Mifugo, tunaambiwa thamani ya bidhaa inayotokana na mifugo ni zaidi ya trilioni 17 ya nchi hii, leo tunadiriki kuona kwamba wafugaji hawana haki katika Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatukatai uhifadhi, lakini uhifadhi leo hii umefika hapa kwa sababu ya ukarimu wa wafugaji katika nchi hii. Kama ingekuwa ni watu wengine wameishi katika hifadhi wale wanyama wasingekuwepo leo, wafugaji tumekuwa tukiishi na wanyama bila madhara yoyote. Kwa nini leo ninyi, kwa sababu, mna nguvu, mna dola, mna jeshi, mna polisi, mnaona hatuna haki kuishi katika maeneo hayo ambayo ninyi mlitukuta katika maeneo hayo?
Mimi naomba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.