Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii adimu. Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu na kuwapongeza kwa kazi nzuri ambayo mmefanya, mimi sikuwepo nilipata changamoto za kiafya lakini Alhamdulillah sasa nimerejea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasimama hapa mimi kama Mbunge wa Muleba Kusini iliyopo katika Mkoa wa Kagera. Kama mnavyojua mapori ya hifadhi na sehemu ambazo zina mvua za kutosha ziko katika Mikoa ya Kagera na Geita, kwa kweli tuko katika hali ngumu. Mheshimiwa Waziri na timu yake nawapongeza lakini kwa sababu ni mwanafunzi mwenzangu, research methodology tuliisoma wote, leo naomba aniruhusu niende kiutafiti. Nina nyaraka 10 (annexes) ambazo nitaomba Mheshimiwa Waziri azifanyie kazi asije akaniweka katika hali ngumu ya mimi kuondoa shilingi hapo kesho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii tuna migogoro ya wakulima na wafugaji, asilimia 28 ya nchi hii sasa hivi ni hifadhi. Mheshimiwa Profesa ambaye anafanya kazi nzuri, anatambua kabisa kwamba neno la Kiingereza la kutumia hapa ni untenable, kwamba hali hii haiwezekani kuendelea kama ilivyo business as usual, asilimia 28 ya Tanzania inaendelea kuwa hifadhi wakati watu hawana mahali pa kulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani kinadharia, haiwezekani Wabunge wengi wamechangia hapa na wote tunaelekea huko haiwezekani, something has to give way. Haiwezekani kwa sababu watu wameongezeka, sasa naomba nichukue nafasi hii kusema kwamba Mheshimiwa Waziri Nchemba tarehe 22 Desemba, 2015 mara baada ya kupewa jukumu la kuongoza Wizara ya Mifugo alikuja Ngara akakaa na wananchi, akaingia makubaliano, akaleta faraja, akatupa matumaini naomba nyaraka ya kwanza appendix no.1 Waziri airejee, sina muda wa kwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nyaraka hii, kilichotokea ni nini, Mheshimiwa Makamu wa Rais ambaye tunajivunia sana sisi akinamama, Samia Suluhu akaandika barua ambayo naomba niikabidhi kama appendix no. 2 akiagiza kwamba mifugo iendelee kuwa pale ilipo mpaka hapo Serikali inajipanga. Sisi tukawaambia wananchi kwamba Serikali yetu sikivu inayoongozwa na Jemedari Dkt. Magufuli haiwezi kuwaacha wafugaji hoi, kwa hiyo barua ya Mheshimiwa Makamu wa Rais ipo hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka telegraphically, tarehe 11 Oktoba, 2016 Mheshimiwa Waziri huyu Profesa ndugu yangu, akatoa tamko hapa akawaambia kwamba kulingana na maelekezo ngazi za juu basi wafugaji wabaki pale walipo, wakati anajipanga, naomba niikabidhi iko hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naogopa maana dakika kumi siyo nyingi lazima niende telegraphically. Sasa kilichotokea na kinachoendelea sasa hivi from nowhere ile Kamati ya Serikali iliyoundwa ya kutafuta maeneo mbadala kwa ufugaji, mara wakaibuka kuwafukuza wafugaji kutoka kwenye mapori ya akiba. Hii ni contradiction kabisa na kwa kuokoa muda natoa nyaraka hapa kumsaidia Ndugu yangu Profesa Maghembe aangalie mambo yaliyojiri. Kwa sababu yeye ni mwenzangu na jirani ya jirani yangu hapa Mama Kilango wanatoka Upareni. Nimeleta hapa picha za ng’ombe wa Ankole wanavyofanana wanapopita kwenye shamba, hakuna linalobaki. Huwezi kusema una- support kilimo kama mifugo itatolewa kwenye akiba kiholela huwezi, it is not possible.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake mkulima miezi sita amehangaika, lakini kundi la ng’ombe likipita in five minutes shamba limekwisha, kwa hiyo ndiyo hali halisi. Kwa hiyo, tatizo hili siyo tu la wafugaji ni tatizo la wakulima, kwa sababu wakulima wale ng’ombe watamaliza hayo mazao yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuokoa muda kinachofuata sasa, mapendekezo ya wafugaji wamekaa na Serikali, Mheshimiwa Waziri anajua hilo. Serikali kwa ujumla Serikali inayofanya kazi ya matumaini sasa inakuwaje hiki kitu kinatushinda wakati tunakwenda kujenga standard gauge na vitu vingine vikubwa. Kwa hiyo, nataka kuweka hapa mapendekezo ya wafugaji wenyewe, let us take it from the horse’s mouth, wafugaji wenyewe wanasemaje, wafugaji hawa wanatii Serikali, hawakaidi Serikali lakini hawawezi bila ardhi, kama huna ardhi huwezi kufuga.

Mheshimiwa Mwneyekiti, kwa hiyo suala la kuwapatia wafugaji ardhi, appendix zinaendelea ninayo ya nane hapa ambayo na yenyewe Waziri ataifanyika kazi. Apppendix hii inaonyesha kabisa mapendekezo na wafugaji wanavyohangaika, wana vijana makini, tunahangaika nao sisi, sasa inaonekana Mheshimiwa Waziri anakuwa mbali hawamfikii kwa urahisi. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, kama yote haya hayakutosha, tunavyozungumza sasa hivi wafugaji wameporwa ng’ombe wao kwenye mapori. Kwa kumsaidia Waziri katika kuja kujibu kesho, mimi msimamo wangu unatoka kesho baada ya kusikia majibu na nyaraka zote hizi za Kiprofesa nilizoweka mezani hapa. Huyu siyo kwamba ni Profesa pia ni my classmate, he knows what I am talking about. Suala hili ni nyeti, suala hili ni la Usalama wa Taifa naomba lifanyiwe lifanyiwe kazi. Ng’ombe 2000 wameporwa maporini, mtu msanii mmoja anasema anaendesha eti mnada maporini. Sasa mnada nani ananunua ng’ombe porini? Wanauziana wao kwa wao, It is totally unacceptable (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli haya mambo anataka tuseme ukweli, nami ninasimama hapa kwa imani kabisa kwamba Serikali haiwezi kushindwa kitu hiki. Mitandao ya Ma-game wapo kule kwenye mapori wanaendesha minada ya kisanii wanauziana wao, naomba Serikali, Mheshimiwa Waziri Serikali watuletee taarifa hawa ng’ombe wamewauza wamemuuzia nani na sasa hivi hao ng’ombe wapo wapi, maana yake itabidi wawapeleke, siyo wapo kwenye misitu hiyo hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema hivi sitaki sensation nimeleta facts hapa kwa imani kabisa kwamba Serikali itazifanyia kazi. Kwa sababu, bila kufanya hivyo you forget kuzungumza mambo ya wakulima na wafugaji, viwanda vitatoka wapi, viwanda vya ngozi kwa mfano, kama huna mifugo huwezi kuwa na viwanda vya ngozi! kwa hiyo lazima tuwawezeshe wafugaji wetu, wakulima wamewasukuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza hapa katika Jimbo langu watu wengi hata mifugo hawana, lakini jirani zangu kutoka Geita, kutoka Simiyu wako kule na ni Watanzania wana haki ya kuwa kule. Sasa wanaendesha propaganda ooh, unajua yule Mama Tibaijuka ni Munyamulenge na yeye ana mifugo, maneno ya rejareja kutukatisha tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wenzetu Rwanda kule kwa Kagame ni ng’ombe 10 hakuna mchezo. Kule kwa Mseveni anauza maziwa Dubai, wenyewe wameshapiga hatua kwa nini, because of land tenure, wametoa maeneo ya kudumu kwa hiyo wana Small Ranching Associations. Hicho ndicho kilio chetu naomba Serikali itusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndio msimamo wangu, Waheshimiwa Wabunge wenzangu twende conceptually tui- support Serikali hii kwa kuleta facts, wale ambao wanalinda maslahi yao kwenye ma-game na kuniita majina, mimi hayo majina hayanitishi, yaani wanasema ukijaribu kutetea hoja wanasema huyu ana maslahi binafsi. Kwa hiyo, inakuwa characterization watu wengi wanaogopa. Watu wengi wanaogopa kusimamia jambo hili kwa kuogopa kwamba watasema hawa ndiyo wana mifugo, lakini nataka kusema kwamba tafadhali sana hali ni tete, na ni suala la Usalama wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi za ufugaji tuondokane na migogoro; nimezungumzia Mkoa wa Kagera lakini the same applied to sehemu nyingi Tanzania nzima. Naomba kuwasilisha nashukuru sana, kesho ndiyo nitajua baada ya kumsikiliza Profesa mwenzangu kama naunga mkono hoja au naondoka na shilingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.