Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Ahmed Juma Ngwali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ziwani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Mimi nianze na ripoti ya ukaguzi wa fedha ambayo TFF wenyewe waliwataka TAC wafanye na waliwakabidhi tarehe 19 Januari, 2016 ripoti namba A/1/2015/2016. Ripoti hii ukifungua ukurasa wa 28 kuna fedha ambazo zimetumiwa na TFF kupitia Rais wake Jamal Malinzi ambazo haziko kwenye document na fedha hizo wamelipana wao wenyewe na pia wakakopeshana wao wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha ambazo amelipwa Michael Richard Wambura bila kuwa na ushahidi wowote ni shilingi milioni sitini na saba mia tano na senti hamsini na nne. Fedha ambazo imelipwa kampuni ya Panchline Tanzania Ltd. ambazo hazina ushahidi wowote na hizi kampuni ni kampuni zao wenyewe tunajua, ni shilingi milioni mia moja na arobaini na saba laki moja hamsini na nne mia mbili ishirini na tisa. Fedha nyingine ambazo zimelipwa zikiwa hazina ushahidi ni fedha ambazo wamelipwa Atriums Dar Hotel Ltd. ambazo zilikuwa ni USD 28,000 sawasawa na shilingi milioni hamsini na tisa, ukifanya grand total pesa zote ambazo hazina mahesabu yoyote na zinaliwa ni shilingi milioni mia mbili sabini na nne na kitu kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni ripoti, ukitaka ushahidi Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe nitakukabidhi, ripoti ya ukaguzi ambayo Wizara kwa vyovyote mnajua, Baraza la Michezo linajua lakini pia TAKUKURU wanajua lakini Serikali imekaa kimya haijasema chochote. Kwa hiyo, naomba Wizara kwa jambo hili ilichukue ilifanyie utaratibu na wakati wa ku-wind- up nitataka majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti nyingine ya ukaguzi ni hii ya fedha za wadhamini, tarehe siioni vizuri lakini imefanywa na ma-auditor wa Breweries. Ukiipitia ripoti hii TFF wametafuna fedha za wadhamini zaidi ya shilingi bilioni 5.5 na hii ripoti nitakupa. Tena hii ni ripoti ya ukaguzi, haya maneno hayatoki kwenye kichwa tu kwa sababu ya mapenzi ama vipi. Tumalize jambo la TFF twende mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina masikitiko sana, mimi ni mpenzi mkubwa wa soka, lakini sidhani kwa mtindo huu inaweza kukua wala sifikirii, wala sina mawazo hayo mimi nina mawazo mengine ambayo nitapendekeza baadaye. Kwanza nionesha namna gani soka haiwezi kukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha ambazo wanakusanya TFF kwa ajili ya kukuza mpira wa miguu zinatoka FIFA ambazo ni fedha kidogo, ni dola 250,000 kwa mwaka. Fedha zinazopatikana Serikalini mnazijua hata kufika hazifiki lakini fedha zinazopatikana kutoka CAF ambazo sio nyingi ndiyo zinazotegewa lakini mpira hauwezi kuendeshwa na fedha hizo ni kidogo sana. Fedha nyingine ni za makusanyo za usajili wa kadi na fomu, wanasema players transfer fee, players contract registration fee, fedha kidogo sana hizo, league participation fee, fine as appeal maana yake hata ile fine ya timu ya Simba imo hapa, sponsorship deals na hizi ni mpaka zitokee na sales market right. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nipendekeze na kwa mtindo huu tusifikirie kimaskini kama anavyofikiria Mheshimiwa Mwamoto kwamba twende zetu huko vijijini tukatafute wachezaji, hapana, tuiunganishe Wizara yako na Wizara ya Viwanda ili ile dhana ya Rais Magufuli kwamba tuwe na tuwe na uchumi wa viwanda iweze kufanya kazi. Tufanye kitu ambacho nchi nyingi wamefanya wamefanikiwa wanaita sports industries ambapo inakusanya michezo yote, hockey imo humo, mwendesha baiskeli yumo humo kila kitu kimo humo. Leo unataka kukuza michezo, unaletewa jezi kutoka China, unakwenda kununua mpira Pakistan, huo mpira unakuwaje? (Makofi)


Mheshimiwa Mwenyekiti, nina masikitiko makubwa sana, tunafanya vibaya sana katika Olympic, vibaya tena vibaya sana. Mheshimiwa nikuulize kitu kimoja, kuna Wanyamwezi wengi sana, samahani Wanyamwezi, pamoja na Wasukuma basi tunashindwa hata kupata mtu wa kurusha tufe? Mheshimiwa Waziri unashindwa hata mtu wa kurusha mkuki, vifua vyote vile, nguvu zote? Mheshimiwa Waziri tukienda kwenye ngumi kila siku tunapigwa, basi nguvu zote tulizonazo tupigwe siye tu kila siku? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ni kwamba hatujaandaa watu wetu, hatujaandaa sekta ya michezo. Kwa hiyo, mimi nipendekeze tena tunapokuwa na hiyo sport industry tunakuwa na michezo mingi ndani, tusifikiri kimaskini, lazima tupate fund kubwa, tutumie PPP, tupate ma-expert, tuwashawishi watu, Serikali iingilie kati pamoja na sekta binafsi ili tuwekeze tuwe na Olympic Park, tuweze kukuza hiyo michezo vinginevyo tutakuja kusema Jamal Malinzi kapiga hela, tutasema maneno ambayo hayawezi kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo cha msingi tupate hiyo sport industry inaweza kutusaidia sana. Maana yake ni kwamba tutajenga viwanda ambapo mipira ya michezo yote tutaweza kuzalisha sisi wenyewe, tutaweza kuzalisha jezi sisi wenyewe, viatu tutaweza kutoa sisi wenyewe, ngozi za ng’ombe tunazo tunaweza kufanya kila kitu sisi wenyewe, hapo hiyo soka inayozungumziwa ndiyo inaweza kukua, tusifikiria kimaskini. Tukishakuwa na hiyo sport industry ndiyo tunaweza kufanya kitu, lakini ukisema leo tukatafute watu sijui Shinyanga, sijui wapi tuunde timu ya Taifa, sio rahisi kabisa. Kwa hiyo, mimi napendekeza hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni muhimu sana, nirudi tena pale TFF. TFF ni Tanzania Footbal Fedaration maana yake ni kwamba Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tulitakiwa sisi tupate Makamu Mwenyekiti ama mbadilishe jina liwe jina lingine lakini mkisema ni chombo cha Tanzania halafu Zanzibar hawana ushiriki katika jambo hili inakuwa haliko sawa. Nafikiri tukae tuangalie upya namna gani tutawashirikisha Zanzibar katika hiyo TFF pamoja na kwamba Mheshimiwa Ally Saleh anasema siyo vizuri, lakini tutakaa pamoja tutalizungumza jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho nizungumzie sanaa, sanaa imezidi imevuta mipaka sasa. Maana nyimbo sasa zinazoimbwa zilivyokuwa na matusi kama ninyi wenyewe Serikali hampo, sijui BASATA wanao-control wanafanya kazi gani? Michezo ya kuigiza (bongo movie) hizi, watu wanakaa wamevua mashati, wanabusiana, wanafanya mambo ya ajabu ajabu, huwezi kukaa na familia yako ukatizama, huwezi kukaa na mtu yeyote ukatizama na nyie mpo na nyie mnatizima, tatizo lenyewe na ninyi mnatizama. Hiyo ndiyo shida, utafikiri kama hatuna control. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, japo dakika zangu hazijaisha lakini baada ya kusema hayo niseme kwamba siungi mkono hoja mpaka Mheshimiwa Waziri atakapojibu hoja zangu, ahsante.