Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii ya Afya.

Kwanza nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu tupo hapa kwa sababu ya afya na pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi ambavyo ameitendea haki Wizara hii ya Afya. Tumeona na tumeshuhudia ajira zikitolewa, tumeona jinsi ambavyo magodoro pamoja na vitanda vikipelekwa kwenye Halmashauri zote nchini, pia tumeona jinsi ujenzi wa chuo pamoja na hospitali ya Mloganzila kule Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zote hizi tunasema ahsante sana Mheshimiwa Rais pamoja na wasaidizi wake wakuu ambaye ni Mheshimiwa Waziri wa Afya Ummy Mwalimu pamoja na Mheshimiwa Dkt. Hamisi Kigwangalla, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija katika Jimbo langu la Busokelo kuna changamoto ambazo mara nyingi nimekuwa nikiongea nawe Mheshimiwa Waziri kwa bahati mbaya sana hazijaweza kutekelezeka. Tuliomba mashine ya usingizi na kwa bahati mbaya pia tuna kituo kimoja tu katika Jimbo zima la Busokelo na mashine hii haipo, maana yake inawalazimu wananchi wangu kusafiri umbali wa zaidi ya kilometa 60 kufuata huduma mjini. Kwa hiyo, nitashukuru sana kama ambavyo uliniahidi kwamba unaweza kufuatilia na kutupatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaomba sana katika hospitali hii ya Kandete tunasema kuna changamoto ya ultra sound na x-ray machine hatuna. Kwa hiyo, tunaomba kama mtaweza kutusaidia katika jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru sana kwa jinsi ambavyo mmejitahidi kupeleka dawa, lakini hizi dawa kwa bahati mbaya wakati mwingine ama yanachelewa kununuliwa katika Halmashauri zetu ama kunakuwa kuna technical delay hapo katikati. Kwa hiyo, tunaomba Wizara kama mtafuatilia vizuri na hii inakuwa ni nchi nzima. Wizara inatoa fedha lakini Halmashauri haziwajibiki ipasavyo. Kwa hiyo, katika hili nafikiri ingekuwa jambo jema kama tungefuatilia pia kama Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine niwashukuru kwa ajili ya Hospitali ya Rufaa ya Mbeya. Hospitali ya Rufaa ya Mbeya tumeona jinsi ambavyo mmeipa kipaumbele kwa maana ya majengo pamoja na vitanda. Bado haitoshi hospitali hii kuna specialist ambao wapo pale kwa zaidi ya miaka mine, categorization zao za mishahara bado ni zilezile za zamani. Kwa hiyo, tungeomba hata hospitali nyingine katika nchi hii ambapo wamepandishwa ngazi kwa kusoma ama kwa taaluma yao waweze kulipwa kufuatana na jinsi ambavyo wanafanya kazi pale kazini kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie suala hili la TEHAMA kwenye afya. TEHAMA kwenye afya ni muhimu sana katika ulimwengu wa sasa, ukizingatia kwamba kwa sasa bajeti iliyopita Wizara mlipendekeza kwamba mtaanza kutumia tele-medicine. Tele-medicine ni mfumo ambao unatumika kutibu wagonjwa ama kufanya consultation na wagonjwa kwa daktari alie mbali na eneo husika. Anaweza akawa Dar es Salaam akamtibu ama akampa ushauri mtu ambaye yupo nje kabisa na Dar es Salaam labda mikoani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba hii tele- medicine iweze kuwezeshwa zaidi ili daktari aweze kupata nafasi ya kuhudumia wagonjwa wengi zaidi kuliko hivi sasa mpaka mgonjwa ama client aende hospitalini kutibiwa. Ni muhimu sana hili lizingatiwe kama Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningefurahi zaidi kuona database ambazo zinatumika hospitalini hasa hizi za CTC II ambayo ni Care and Treatment Clinic pamoja na DHIS II ambayo ni District Health Information Systems kama zinakuwa developed au programmed na wazawa kuliko hivi sasa wazawa wanashiriki kwa sehemu ndogo, asilimia kubwa sana tunapewa misaada kutoka nje kwa maana kwamba hata wale specialist wa kusimamia hizi. Lengo lake ni kufanya sustainability yake iweze kuwepo kwa sababu hii misaada kuna wakati itakwisha na ikiisha hatutakuwa tena na support nyingine yoyote. Kwa hiyo, tukiwashirikisha wazawa itaturahisishia zaidi kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nikija katika suala la HIV (UKIMWI) tumeona mmetenga shilingi bilioni 251.5; ninaiomba Wizara na Waheshimiwa Wabunge ninyi ni mashahidi, hivi karibuni tulikuwa na semina ya kutoka National Council of People Living With HIV humu ndani. Tuliona kwamba kuna changamoto kubwa sana kwa dawa kwa ajili ya magonjwa nyemelezi. Kwa bahati mbaya sana hizi opportunistic infections wafadhili hawatoi wala Serikali hainunui. Maana yake inaishia kuwa gharama kwa wagonjwa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba niunge mkono hoja. Ahsante.