Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Neema William Mgaya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Afya. Nianze kwa kumpongeza Rais wangu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa jitihada kubwa ya kuimarisha upatikanaji wa dawa.

Ukiangalia kwenye bajeti ya mwaka 2015/2016 pesa zilizopelekwa kwenye huduma ya upatikanaji wa dawa ilikuwa shilingi bilioni 24, hivi sasa ndani ya miezi tisa chini ya Dkt. John Pombe Magufuli, pesa zilizopelekwa za dawa ni shilingi bilioni 112. Kwa Mkoa wa Njombe mpaka dakika hii hospitali, zahanati, vituo vya afya tumeshapokea karibia asilimia 80 mpaka 90 ya pesa za dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Mawaziri kwa usimamizi mzuri, Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla kwa kweli wanasimamia vizuri zoezi hili, pongezi sana kwao. Ombi langu moja kwa Serikali, Mheshimiwa Ummy ile hospitali yetu pale ya Makambako ni Hospitali ambayo ipo katikati inahudumia Mikoa ya karibu kama Iringa, wengine wanatoka Mbeya maeneo yale ya Mbarali kuja kupata huduma za matibabu pale Makambako. Hivyo basi, zile pesa mnazotupangia zinakuwa chache mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru tumepata pesa karibu asilimia 90 za dawa lakini mnazo tupangia ni ndogo tunaomba muongeze bajeti katika pesa za dawa katika Hospitali ile ya Makambako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee pia kuwapongeza tena Mheshimiwa Ummy na Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla kwa kusimamia kikamilifu huduma ya matibabu ya kibingwa. Kwa kweli katika hili mmefanya vizuri, tumeona katika hotuba yenu rufaa sasa hivi zimepungua za kwenda nje, hivyo naamini zile pesa ambazo zingetumika kwa ajili ya rufaa za wagonjwa kwenda nje zitatumika katika masuala mengine ya maendeleo kama maji, umeme, barabara na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitochoka kuendelea kupongeza, nawapongeza pia Mheshimiwa Rais, Waziri Ummy, Naibu Waziri Kigwangalla kwa kuweza kufanikisha upatikanaji wa vifaa vya hospitali kama magodoro, vitanda, mashuka, tumeona kwamba Wilaya zote ndani ya nchi yetu ya Tanzania tumeweza kupata vifaa hivyo. Hongera sana kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la vifo vya mama wajawazito, kila mwanamke aliyesimama hapa amezungumzia tatizo hili la vifo vya akina mama wajawazito. Takwimu zinaonesha na kwenye hotuba yake Mheshimiwa Waziri ameonesha kabisa kwamba vifo vya akina mama wajawazito vimeongezeka kutoka 430 mpaka 556 katika vizazi hai 100,000, hali ni mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ummy wewe ndiye Waziri mwenye dhamana katika Wizara hii ya Afya, wewe ni mwanamke, wewe ni mzazi, wewe ni mama wa watoto. Mheshimiwa Ummy unatusaidiaje wanawake wenzio katika tatizo hili? Hakikisha unapambania tatizo hili kutusaidia wanawake wenzio ili uweze kuacha alama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mheshimiwa Ummy katika Wizara hii unaye kaka yetu Naibu Waziri Dkt. Kigwangalla yeye ni daktari kwa taaluma na Balozi wa Wanawake, shirikianeni katika kuhakikisha kwamba tatizo hili la vifo vya wanawake linakwisha nchini kwetu Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala pia la huduma za afya kwa watoto wachanga. Nataka nijue ni lini Serikali itaweka utaratibu mzuri wa kuweza kusimamia afya ya mtoto mchanga kwa maana ya siku 30 mpaka siku moja. Nimesoma vijarida mbalimbali vya wataalam vinaonyesha kwamba tukiweza kudhibiti vifo vya watoto kuanzia siku 30 mpaka siku moja kwa maana ya kuboresha afya za watoto wao, tutaweza kupunguza vifo vya watoto wadogo chini ya miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ulaya wenzetu watoto ambao wanazaliwa kwa gramu 500 mpaka gramu 600 wanaishi tofauti na hapa kwetu. Naiomba Serikali sasa ione umuhimu wa kuweza kuanzisha huduma ya afya za watoto hawa wachanga wa siku 30 mpaka siku moja, waanzishe wodi kwenye kila Wilaya ndani ya Tanzania kama ilivyopeleka vifaa vile kila Wilaya na hizi wodi za watoto wachanga zifunguliwe kila Wilaya ili kina mama wa Wilaya ya Wanging’ombe waweze kupata huduma hiyo, Ludewa, Makete, Njombe na Wilaya zingine ndani ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma ya matibabu ya saratani, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri amezungumza kwamba sasa hivi wanakwenda kununua mitambo ya kutoa huduma ya tiba kwa ajili ya saratani. Mheshimiwa Waziri na dada yangu Ummy, kwa nini Serikali msiwekeze zaidi kwenye kinga, ukizingatia kwamba saratani ambayo inaua Watanzania wengi ni saratani ya shingo ya uzazi. Wanawake wengi wanakufa, hebu wekezeni zaidi kwenye kinga, kwenye Wilaya zetu kule tunakotoka ili mwanamke wa Ludewa kule aweze kupata huduma hiyo na kugundua hilo tatizo mapema. Kwa sababu inaonekana kwamba wagonjwa wa saratani wanakuja kugundulika wana matatizo hayo wakati imeshafika stage ya hali mbaya, matokeo yake Serikali inatumia gharama kubwa kuwatibia, kuwafanyia huduma na matibabu ya mionzi, chemotherapy wakati tungezigundua mapema tungeweza kuokoa maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina experience Mama yangu amekufa kwa pancreatic cancer, na tumekuja kugundua muda umeshapita, kama kungekuwa na huduma hizi mapema hata akina mama wanapokwenda tu hospitali anaweza aka-check, akagundua mapema, mtu anaweza akakaa kwa muda mrefu zaidi ya miaka 15 mpaka 20, lakini wagonjwa wengi wa kansa wanagundulika wakati hali imeshakuwa mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali ijikite zaidi kwenye kinga na kushusha kule kwenye Wilaya zetu ili kila Wilaya tuweze kupata huduma hii ya kinga ili tuweze kuokoa wanawake wengi, Kwa sababu kansa ya shingo ya uzazi ndiyo ambayo inaua wanawake wengi. Wengi wanaokufa na kansa ni wanawake ukiangalia katika takwimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la uwezeshwaji wa wanawake kiuchumi. Mheshimiwa Waziri, Dada Ummy kwenye hotuba yako umejinasibu kwamba kule Dar es Salaam mmefungua Benki ya Wanawake, Pwani wamefaidika, Dar es Salaam wamefaidika na mikopo wamepatiwa viwanja. Mimi naomba kwenye majumuisho yako ukija kujumuisha hapa uniambie ni lini Benki ya Wanawake itafunguliwa Mkoa wa Njombe ili sisi wa kina mama wa Njombe tuweze kufaidika na sisi na mikopo hiyo, lakini vilevile tuweze kufaidika tupate viwanja kama walivyopata akina mama wa Dar es Salaam, kama walivyopata akina mama wa Pwani. Hivyo, katika majumuisho yako nitapenda unijibu kwamba ni lini benki hiyo itafunguliwa ndani ya Mkoa wa Njombe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimalizie kwa kuzungumza suala la haki za watoto hasa watoto wa kike. Akina mama wenzangu Mheshimiwa Faida Bakar mpaka ametoa machozi hapa kuhusiana na suala la watoto, nakubali kabisa sisi kama walezi, wazazi tunajitahidi sana kuwasaidia watoto wetu wasiingie kwenye ndoa za utotoni, lakini Sheria ya Ndoa ni kichocheo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajua kabisa kuwa suala hili ni la Katiba na Sheria, lakini Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dada Ummy wewe ndiye unayesimamia haki ya mtoto wa kike. Nakuomba sasa kushirikiana na Waziri wa Katiba na Sheria, mlilete suala hili mapema ndani ya Bunge ili tuweze kulifanyia maboresho na tusibaki tu tunalalamika hapa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.