Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Selemani Jumanne Zedi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukene

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuwa na afya njema ili na mimi kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Bukene niweze kuchangia hoja muhimu sana ya Wizara ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekti, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu kwa uwasilishaji mzuri sana na hotuba nzuri sana ambayo imewasilishwa kwa weledi wa hali ya juu, hongera sana Mheshimiwa Ummy. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kabisa kwa kusema kwamba naunga mkono hoja hii asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Bukene, kwa dhati kabisa ya moyo wangu niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuhakikisha kwamba Jimbo langu la Bukene kwa mara ya kwanza linapata huduma ya upasuaji kwa vituo viwili vya afya. Huduma ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na nichukue fursa hii nimpongeze Naibu Waziri ya Afya Mheshimiwa Dkt. Hamisi Kigwangalla ambaye alifunga safari baada ya kufanya ufuatiliaji wa muda mrefu na kuja hadi kituo cha afya cha Itobo kufanya uzinduzi kwa niaba pia ya kituo cha afya cha Bukene, hongera sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kazi nzuri hiyo uliyoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vituo hivi vya upasuaji ni azma ya Serikali ya Awamu ya Tano kupunguza vifo visivyo vya lazima vya akina mama na watoto. Kabla ya vituo hivi akina mama waliokuwa wakihitaji huduma za upasuaji katika Jimbo la Bukene walikuwa wakilazimika kusafiri zaidi ya kilometa 80 kutoka maeneo mengine hadi hospitali ya Wilaya ili kupata huduma hii. Lakini sasa huduma hii imesogezwa karibu sana na niseme tu kwamba katika muda wa hii miezi miwili ambayo upasuaji umeanza muitikio ni mzuri sana na tumeweza kufanya operesheni za kutosha na kuokoa maisha ya akina mama na watoto wa ndani ya Jimbo la Bukene.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu ni moja tu, pamoja na kwamba huduma hii imeanza, lakini kuna upungufu mkubwa sana wa watumishi. Katika kituo cha afya cha Bukene mganga anayeweza kufanya upasuaji yuko mmoja tu na huyu anaifanya shughuli hiyo kwa muda wa saa 24. Kwa hiyo, inapotokea kwamba anakuwa kwenye majukumu yasiyoweza kuzuilika mgonjwa akifika pale kama anahitaji upasuaji anakosa hiyo huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hivyo hivyo kwenye kituo cha afya cha Itobo, mganga anayeweza kufanya upasuaji kwa sasa tunaye mmoja tu na kwa Itobo ni mbaya zaidi kwa sababu mganga huyu bado ana miezi michache tu ili astaafu. Kwa hiyo, kama hakutakuwa na jitihada za ziada ili kupata mganga basi huenda kituo hiki kikashindwa kutoa huduma ya upasuaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Halmashauri ya Nzega tumejaribu kufanya re-allocation ya kuwatoa waganga kutoka Hospitali ya Wilaya kuwapeleka kwenye hivi vituo vya afya lakini re-allocation hii sasa imefika mwisho kwa sababu hata Hospitali ya Wilaya nao wana upungufu. Hata hao wawili huyu aliyeko Bukene na aliyeko Itobo tumewatoa pale Hospitali ya Wilaya ya Nzega. Kwa hiyo, re-allocation ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Nzega imefika mwisho haiwezekani tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe kwa niaba ya wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega Wizara itufikirie kama ombi maalum ili tuweze kupata madaktari wanaoweza kupasua wapangwe katika Halmashauri ya Wilaya ya Nzega na mmoja hususan apelekwe kituo cha afya cha Itobo na mmoja hususan apelekwe kwenye kituo cha afya cha Bukene ili huduma hizi muhimu na nzuri za upasuaji ziendelee kupatikana ili wananchi wetu, na hasa akina mama na watoto waweze kuepukana na vifo ambavyo kimsingi vinaweza kuzuilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kuzungumzia ni huduma za x-ray katika Hospitali ya Wilaya ya Nzega. Leo hii tunapozungumza hapa ni miezi mitano sasa x-ray ya Hospitali ya Wilaya ya Nzega imekufa haifanyi, kazi. Hoja yangu hapa ni kwamba tatizo sio kufa kwa x-ray; x-ray ni kifaa ambacho kinafanya kazi kwa hiyo kinaweza kufa. Lakini hoja yangu hapa ni uharaka wa namna ambavyo x-ray iliyokufa inaweza kushughulikiwa ikapona na ikaendelea kutoa huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, x-ray ya Hospitali ya Wilaya ya Nzega imekufa tangu tarehe 13 Desemba, 2016 na baada ya kufa tu Mkurugenzi wa Halmasauri ya Nzega aliandika barua kwa Katibu Mkuu wa Wizara ili Wizara wai-engage kampuni ambayo ina mkataba wa kutengeneza hizi x-ray za Phillips ili iweze kuja Nzega na kutengeneza. Lakini speed imekuwa ndogo mno, mpaka leo tunaongelea mwezi wa tano ni danadana tu. Hao mafundi walikuja mara moja wakaangalia vifaa, wakatoweka mpaka sasa hawajaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho tutataka tujue utaratibu au mkataba uliopo kati ya Wizara na hawa watoa huduma wa ku -service hizi x-ray aina ya Phillips ukoje na umekaa vipi kwasababu kama utaratibu ni mbaya basi tupendekeza kwamba Hospitali za Wilaya zenyewe zitafute mafundi au service provider wenye uwezo ili waweze kutengeneza x-ray. Kwa sababu ni jambo ambalo halikubaliki x-ray kukaa miezi mitano imekufa na wagonjwa wanakwenda pale wanakosa huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linaleta usumbufu mkubwa sana kwa wagonjwa wanaofika Hospitali ya Wilaya ya Nzega na ambao matatizo yao yanahitaji huduma za x- ray wanapata taabu sana. Kwa hiyo, niombe kabisa kwamba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kutoa majumuisho atoe ufumbuzi, kwamba x-ray ya Hospitali ya Wilaya ya Nzega ambayo miezi mitano sasa imekufa ni lini itaweza kushughulikiwa ili wananchi waweze kupata huduma hiyo muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nizungumzie upatikanaji wa dawa katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD). Kwanza niipongeze Serikali kwa dhati kabisa kwa kutenga hela nyingi za kutosha kununua dawa. Hili kwa kweli ni jambo la kupongezwa, haijawahi kutokea kiwango cha bajeti kilichokwenda kwenye dawa mwaka huu ukilinganisha na miaka ya nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hoja hapa ni sasa madawa yapatikane, kwa sababu kupatikana kwa fedha za kununua dawa ni jambo moja lakini kupatikana kwa dawa pia ni jambo linguine. Kwa sababu utaona kwamba fedha za dawa ambazo zinapelekwa kwenye akaunti za vituo vya afya au zahanati kule MSD kwa hiyo, unakuta vituo vya afya au zahanati vikiomba dawa MSD kunakuwa na out of stock nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega. Taarifa za tarehe 28 mwezi uliopita, ukijumlisha vituo vya afya na zahanati zote tuliomba dawa za shilingi milioni 126 lakini tukapata dawa za shilingi milioni 24 tu, ambayo ni kama asilimia 20 tu. Kwa hiyo, utakuta kwamba sasa hivi tuna balance ya fedha za dawa ambazo ziko MSD, karibu shilingi 503,000,000. Hata hivyo ukiomba dawa sasa upatikanaji wa dawa unakuwa mdogo. Kwa hiyo upatikanaji wa fedha uendane sambamba na upatikanaji wa dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia 100 na Wizara ya Afya wanafanya kazi nzuri sana. Ahsante sana.