Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuunga mkono hoja iliyo mbele yetu. Aidha, baada ya kuunga mkono hoja, naomba nichangie baadhi ya maeneo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii pamoja na Naibu Waziri na watendaji wote ukianzia na Katibu Mkuu (Ujenzi) na Katibu Mkuu (Uchukuzi na Mawasiliano) pamoja na wataalam wote wa Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizi, naomba nichangie kwa kuanza na Jimboni kwangu. Niombe Serikali ihakikishe inajenga barabara ya kutoka Sumbawanga – Matai - Kasanga Port kwa kiwango cha lami. Ujenzi huu umechukua muda mrefu sana kutokana na upatikanaji wa fedha kutoka Wizara ya Ujenzi kwenda kwa mkandarasi na hivyo mradi kuwa na gharama kubwa kutokana na Serikali kulazimika kulipa fedha nyingi kutokana na mkataba. Kiasi cha fedha kilichotengwa ni cha kutosha, niiombe Serikali ihakikishe fedha zinatolewa ili mradi huu wa barabara uweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ninalopenda kuchangia ni juu ya ujenzi wa barabara ya kutoka Matai - Kasesya border, ambayo Mheshimiwa Waziri alipata nafasi ya kuitembelea na kuahidi kwamba mara mkandarasi atakapopatikana ujenzi utaanza. Katika mwaka huu wa fedha wa 2016/2017, Serikali iliweza kutenga kwenye bajeti

kiasi cha shilingi bilioni 11 na ukisoma taarifa ya Mheshimiwa Waziri imeonesha kwamba taratibu za kumpata mkandarasi zinaendelea. Ni imani yangu kubwa kwamba kiasi cha fedha kitaweza kutolewa kabla ya mwaka huu wa fedha haujamalizika. Katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2017/ 2018 barabara hii imeweza kutengewa kiasi cha shilingi bilioni 4.9 kutoka shilingi bilioni 11 kwa mwaka wa fedha 2016/2017, sitarajii gharama za ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami kupungua kwa zaidi ya nusu. Naiomba Serikali iharakishe utaratibu wa kumpata mkandarasi ili aanze ujenzi wa barabara hii muhimu sana kwani siamini kwamba nchi hii ina tatizo la upatikanaji wa wakandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kuchangia ni kuhusu ujenzi wa Daraja la Mto Kalambo, ahadi ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa akiwa Waziri wa Ujenzi na akasisitiza siku alipokuja kuomba kura Kalambo akimtaka Mkurugenzi atangaze mara moja kazi ya ujenzi wa daraja hilo. Naomba niishukuru Serikali kwa kutenga kiasi cha shilingi milioni 100 japo kiasi hiki sidhani kama kinatosha kwa kuzingatia ukubwa wa daraja hili. Naiomba Serikali ihakikishe kwamba ujenzi wa daraja hili unaanza mapema na hasa kipindi cha kiangazi kwani mvua zikishaanza kunyesha siyo rahisi ujenzi kufanyika kwani mto hufurika kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ifike mahali Serikali itimize ahadi zake kwa vitendo kuhusu ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga kwani ahadi hii ni ya muda mrefu sana. Umuhimu wa uwanja huu baada kukamilika kwa Uwanja wa Kimataifa wa Songwe na ule wa Mpanda Mkoani Katavi unajulikana na hakuna hata chembe ya ubishi. Naomba Serikali sasa itende haki kwani fedha za kutoka nje ni miaka zaidi ya mitatu zimekuwa zikioneshwa tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ngazi ya kitaifa naomba kuchangia kuhusiana na mradi wa usafirishaji wa DART. Ukienda kwenye mataifa ya nje miongoni mwa miradi inayopigiwa mfano Kusini mwa Jangwa la Sahara basi utakuta miradi miwili kama one success stories nayo ni treni ya umeme ya Lagos na Mradi wa Mabasi ya Mwendo Kasi ya Dar es Salaam. Ni jambo la busara kwa kuwa mradi huu kama moja ya miradi ya kitaifa na wenye mafanikio makubwa na hivyo kutouchukua kama mradi wa watu wa Dar es Salaam. Hivyo sote tuna jukumu la kuhakikisha kwamba mradi huu unapewa upendeleo wa pekee kwa maslahi ya Watanzania wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile uwekezaji mkubwa unafanywa na Serikali kwa maana ya ujenzi wa miundombinu kwa awamu ya kwanza, ya pili, ya tatu na hata ya nne iko haja kubwa kwa Serikali kuhakikisha uwekezaji mkubwa unafanywa kwa Serikali kuuza baadhi ya hisa zake kwa Watanzania wengi na pia kuwa na maongezi ili mbia wa Serikali naye auze hisa zake kwa kuzipeleka DSE (Dar es Salaam Stock Exchange) ili umiliki uwe wa wananchi wengi na ili mtaji mkubwa uweze kupatikana utakaowezesha uwekezaji mkubwa ikiwa ni pamoja na kiwanda cha kuunganisha mabasi hapa nchini pamoja na uzalishaji wa matairi, hili litawezesha kauli ya Serikali yetu ya CCM ya Tanzania ya viwanda kutekelezeka kwa vitendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mataifa ya wenzetu kama Ethiopia, Japan, Korea na kwingine wameweza kufanikiwa kwa kuweka mikakati maalum ya kuhakikisha kwamba kunakuwepo na upendeleo maalum kwa wazawa na makampuni ya wazawa wazalendo. Wakati umefika sasa kama Taifa tukafanya uamuzi huo bila ya kuchelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna msemo wa Waswahili unaosema ukiona vinaelea vimeundwa. Hayo makampuni yanayotamba duniani kama vile Samsung, Dangote, Hutchison Whampoa, DSM Port Operator - TICTS na kadhalika yametokana na maamuzi yaliyofanywa na Serikali zao mahususi kuyafanya yakue kabla ya kuyataka yaanze kushindana na nguvu za soko.