Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Kiteto Zawadi Koshuma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano


MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kutoa mchango wangu kwa maandishi katika Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwepo wa meli mpya katika Ziwa Victoria, kutafungua fursa za biashara katika Mikoa ya Mwanza na Kagera kwani mazao mengi kutoka mikoa hiyo hutegemea usafiri wa maji. Vile vile meli hiyo itasaidia usafirishaji wa abiria na mizigo. Hivyo niiombe Serikali kutenga fedha katika mwaka huu wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya ununuzi wa meli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa upanuzi wa barabara ya Furahisha hadi Pasiansi Airport, hii imesaidia kupunguza foleni na msongamano wa magari. Naiomba Serikali ianze kufanya tathmini ya kuendelea kupunguza msongamano katika Jiji la Mwanza kwa kufungua barabara zitakazoondoa msongamano katikati ya Jiji. Barabara hizo ni za:- Buhongwa
– Rwanhima – Kishiri – Igoma na barabara ya Mkuyuni – Mahina – Nyakato – Buzuruga na barabara ya Butimba – Fisheries – SAUT – Mkolani. Kwa kufungua barabara hizi kutaondoa msongamano katikati ya Jiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Wizara hii lakini sijaona fedha zilizotengwa kwa ajili ya ununuzi wa kivuko cha base Wilaya ya Ilemela kwenye Jimbo la Mheshimiwa Angelina Mabula ambapo pia Mheshimiwa Rais aliahidi wakati wa kampeni za uchaguzi 2015. Katika vikao vya RCC tulikubaliana kununua kivuko hicho. Niiombe Serikali itenge fedha za kununua kivuko hicho ambacho kitawasaidia wakazi wa kisiwa hicho cha base wapatao 600 na zaidi hususan akinamama ambao wanahitaji kuvuka kuja mjini kwa ajili ya kujifungua hasa wanapopata rufaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nashukuru na naunga mkono hoja.