Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Savelina Slivanus Mwijage

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi za maendeleo zinakuwa nyingi, pamoja na hayo Wizara inaomba bajeti ya kukidhi miradi hiyo na bado fedha hazitoki kwa wakati na kinachotoka ni kidogo mno kukidhi mahitaji. Ni kwa nini Wizara isipange au kuona sasa ni wakati wa kumaliza viporo kuliko kuendelea na miradi mipya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Uwanja wa Ndege Kajunguti umekuwa kwenye bajeti kwa muda mrefu sana lakini katika bajeti hii sikuona sehemu ilipotengewa fedha ya kujenga uwanja huu. Serikali ingekuwa inatenga angalau kila mwaka kwa ajili ya kufidia wananchi watakaoathirika na suala hilo. Kipindi uwanja wa Taifa wa Mwalimu Nyerere unaanza kujengwa vile vile uwanja wa Kajunguti ulikuwa kwenye malengo ya kutengenezwa, ila sijaona wala kusikia sehemu yoyote kuwa uwanja huu utafanyiwa marekebisho yoyote. Suala hili la uwanja wa Kajunguti limekaliwa kimya sana. Huo uwanja ni tegemeo kubwa sana kwa Wanakagera. Kama tunavyotegemea uwanja wa nchi jirani ya Uganda Entebbe sasa uwanja wetu wa Kajunguti uboreshwe ili Wanakagera wasitegemee nchi jirani kama Uganda, Burundi na Kenya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba majibu sahihi ya maswali haya:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara zinazojengwa hazijengwi kwa viwango stahiki, ni kwa nini Wizara wakati inatengeneza tenda isijiridhishe kwanza kazi anazopewa huyo mwombaji wa tenda ana uzoefu nazo wa kutosha? Nimeona barabara ya Ushirombo – Lunziwe – Nyakanazi – Rushounga hadi Benako, barabara hii ni mbovu kupitia kiasi, kilomita ulizotaja zilizokarabatiwa kweli ni aibu, ukizingatia kwamba barabara hii ni rasilimali kubwa sana kwa kuwa inapitisha magari makubwa yanayokwenda mikoani na nchi jirani zinazotuzunguka. Hivi kwa makusanyo yetu Serikali inashindwa nini kutengeneza barabara kwa viwango stahiki? Kutengeneza barabara vipande vipande ni aibu kubwa kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, njia za majini (katika Ziwa Victoria) kwa Mkoa wetu limekuwa ni tatizo kubwa, tulikuwa na meli za usafirishaji mizigo zilizokuwa zinawasaidia wafanyabiashara kusafirisha bidhaa zao mbalimbali, tulikuwa na meli aina ya Nyangumi, Umoja, MV Butiama na MV Victoria lakini kwa sasa meli hizo zote zimekuwa chakavu na nyingine mpaka kusimama kabisa. Je, ni lini Serikali itajielekeza katika kuzitengeneza meli hizo? Kwa sababu wafanyabiashara kutoka sehemu jirani kama vile Uganda, Kenya na Burundi wanashindwa kufanya shughuli za kiuchumi kutokana na tatizo la usafirishaji wa majini. Ni lini Serikali yetu italeta wawekezaji kama ilivyo Dar es Salaam ambako wana mwekezaji ambaye ni Azam? Wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu na Nne kulitokea mwekezaji ambaye alileta Speed boat ambazo zilikuwa zinafanya safari yake Bukoba kwenda Mwanza lakini zilizuiliwa. Kwa hiyo, ni lini Serikali itamruhusu mwekezaji huyo kuendelea na usafirishaji huo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nimekuwa nikipiga kelele mara kwa mara kuhusu kivuko cha Kyenyabasi kinachounganisha vijiji vitatu vya Bujugo, Kanazi na Kasharu. Wananchi wa vijiji hivyo vya Bukoba Vijijini wanateseka kwa kuwa kivuko hicho kimekuwa kikikarabatiwa na TEMESA kila wakati lakini bado tatizo lipo pale pale. Je, ni lini Serikali italeta kivuko kingine kusaidia wananchi wangu wa Mkoa wa Kagera?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wananchi wangu wa Bukoba Vijijini wanateseka sana na barabara za vumbi kama vile barabara za Kanazi, Karebe, Ibwera, Katunjo, Nyakibimbili, Katoro hadi Kyaka. Je, ni lini Serikali itaweka mikakati na mipango ya kutengeneza barabara hizo tajwa zinazounganisha vijiji mbalimbali ikiwemo na Hospitali ya Izimbya ambayo iko kwenye barabara ya vumbi ili kuwasaidia wananchi? Naomba majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya ukanda wa Ziwa Victoria imekuwa matatani sana maana ziwa linazidi kusogea mpaka kwenye makazi ya watu na maeneo ya mashule. Kwa mfano, Lake View Secondary School, sehemu za vivutio vya watalii kama vile Space Hotel, Kloyera tours, Bukoba Club Yasila Hotel na Shule ya Nyashenye vyote viko hatarini kukumbwa na maji. Je, ni lini Serikali itajenga ukuta kuzuia maji ya ziwa yanayowasogelea wananchi wa Bukoba hususan waishio Kando kando ya ziwa? Naomba majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na malalamiko kwa wananchi juu ya kuweka minara katikati ya nyumba. Migogoro hii imekuwa mikubwa na haitafutiwi ufumbuzi mwaka hadi mwaka kiasi kwamba imekuwa kero kubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera. Minara hiyo kwa nini isiwekwe juu ya milima ili wananchi wakae kwa amani hususani ni wananchi wa Kata ya Kashi Manispaa ya Bukoba? Vile vile naomba nijue hii migogoro ya wananchi ni lini itakwisha? Kwa sababu imekuwa ni kero kubwa kwa wananchi wa Kagera. Kuweka minara kuna madhara makubwa kwa wananchi kutokana na miungurumo yake pamoja na mionzi ya minara hiyo kukaa karibu na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba suala la minara nipate majibu. Naomba kuwasilisha.