Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Julius Kalanga Laizer

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nitumie nafasi hii kukushukuru pia kwa kunipa nafasi ya kusema maneno machache kwa dakika hizi tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ni Wizara muhimu sana ni cross cutting Ministry kwa sababu Wizara zote zinaitegemea hii. Tuna matatizo makubwa ya upelekaji wa fedha ya miradi ya maendeleo katika Halmashauri zetu. Hili limekuwa ni tatizo sugu katika Halmashauri nyingi. Kwa mfano, katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli tumepelekewa milioni 200 tu kati ya shilingi bilioni 1.2 ambazo tulitengewa. Sasa katika mazingira ya sasa tunahangaika kupitisha bajeti, tunataka Waziri aje atueleze wana mikakati gani kuhakikisha kwamba fedha zote zilizobaki katika bajeti ya mwaka huu 2016/2017, zinapelekwa katika Halmashauri zetu kabla ya Juni mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama sitapata majibu ya kuridhisha basi nitashika shilingi ya Waziri, kwa sababu hakuna sababu ya kupitisha bajeti mpya kama bajeti tuliyoipitisha hatupeleki kwenye Halmashauri zetu. Haitakuwa na maana kwa sababu akinamama wajawazito watafia njiani na wakati wa mvua barabara zetu hazitapitika na hata sekta nyingine zote hazitakuwa na ustawi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nimeona katika kitabu tunashukuru kwamba barabara ya Loliondo – Monduli kwa maana ya Mto wa Mbu pamoja na Serengeti imeendelea kutengewa fedha. Barabara hii ni muhimu, tunaitengea fedha kidogo sana. Nataka Serikali ituambie mpango wa barabara hii itakamilika muda gani? Kwa maana mwaka huu itajengwa kilomita ngapi na mwaka unaofuata kilomita ngapi mpaka barabara itakapokamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri namwona Waziri wa Viwanda. kule Engaruka yamepatikana magadi yenye ujazo wa trilioni nne, mpaka sasa hakuna barabara itakayofika katika eneo lile na wananchi wetu wapo tayari kutoa ardhi yao kwa ajili ya viwanda vile. Kwa hiyo, kama Serikali haitakuwa na commitment ya kupeleka miundombinu kwa maana ya angalau barabara na baadaye reli, ardhi ile tutaendelea kuitumia lakini wananchi wetu wapo tayari kutoa hata bure kwa ajili ya kujenga kiwanda kile. Kama hakuna commitment ya Serikali ya kupeleka miundombinu kwenye maeneo yale mtuambie ili wananchi waendelee kutumia maeneo yale wakajenge mpaka mtakapokuwa tayari kuleta miundombinu na kiwanda kianze na wakati huo gharama za fidia zitakuwa kubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali ituhakikishie ni lini barabara hii itakamilika kutoka Mto wa Mbu kwenda Loliondo kwa sababu ya umuhimu wa magadi yaliyopo Engaruka ambao sisi tupo tayari kuwapa ardhi kwa ajili ya kuanzisha kiwanda hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni ahadi za Rais. Naomba Waziri atuambie Rais alivyopita katika Wilaya ya Monduli wakati anaomba kura aliahidi kutujengea barabara ya lami kutoka Monduli Mjini kwenda Monduli Juu kule kwa Sokoine. Pamoja na kwamba Waziri haandiki lakini nataka Serikali iniambie ni lini mchakato wa barabara hiyo utaanza kwa sababu Rais aliahidi au Serikali ituambie kwamba labda Rais alisema uwongo ili kujitafutia kura, kama ni kweli basi tuambiwe ni lini barabara ya Monduli kwenda Monduli Juu Serikali itaijenga kwa lami kama Rais alivyoahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la mwisho ambalo naiomba Serikali iangalie ni upelekaji wa fedha za miradi katika barabara za Mkoa. Sisi tuna barabara moja hii barabara ya Loksale tunaona imetengewa shilingi milioni mia tatu ambayo ina kilomita hamsini, haiwezi kusaidia chochote. Pamoja na kwamba kwa kweli tunampongeza Meneja wa Barabara wa Mkoa kwa sasa anafanya kazi nzuri na anasimamia miradi mingi ya Mkoa kuliko wakati mwingine wowote. Tunamshukuru na tunaendelea kumuunga mkono katika hili, fedha mnazompelekea ni fedha kidogo sana hazitoshi tunaiomba Serikali ione namna ya kuongeza fedha katika Mfuko wa Barabara ili barabara zetu nyingi ambazo bado ni vumbi ziweze kupitika kwa wakati wote, tusipofanya hivyo hata huduma zingine hazipatikana na huduma hizi tunazozitoa zitakuwa haziwafikii wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nikushukuru.