Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Wizara hii muhimu sana, ambazo ni Wizara tatu kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda niwashukuru sana Mamlaka ya Bandari kwa kazi ambayo wanaifanya Kigoma, nimeona zabuni ya bandari ya Kibirizi, ninaamini kabisa bandari ya Ujiji zabuni yake itakuwa ama imetoka leo au Jumatatu na pili bandari ya Kagunga imekamilika, kwa hiyo, napenda niwashukuru sana, nataraji kwamba hatua zitakazofata bandari ya Mwamgongo na bandari ya Mtanga zitaweza kufanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili nimeona ukurasa wa 102 wa hotuba ya Waziri kuhusiana na uwanja wa ndege wa Kigoma, nashukuru sana kwamba sasa zabuni itatangazwa tena na kuhakikisha kwamba tunapata mkandarasi kwa ajili ya kujenga jengo la abiria na njia zinazoenda pale. Hii ni ishara kwamba naungana mkono na juhudi za Mkoa wa Kigoma na Wabunge na wananchi wa Mkoa wa Kigoma kutaka kuubadilisha Mkoa wetu ule uweze kuwa na maendeleo ya kasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ambalo nataka kuzungumzia ni reli, wenzangu wamezunguka hapa kuhusu reli na ukitazama hotuba ya Waziri wameendelea toka mwaka jana tumelalamika kuhusu jambo hili, kwamba wametoa tafsiri mpya ya reli ya kati. Reli ya kati tafsiri yake ni Kigoma - Dar es Salaam au Dar es Salaam - Kigoma, maeneo mengine yote ni matawi ya reli ya kati. Ukitoka Ruvu kwenda Tanga ni tawi, kutoka Tabora kwenda Mwanza ni tawi, kutoka Manyoni kwenda Singida ni tawi, ukitoka Kaliua kwenda Mpanda ni tawi, mengine yote hayo ni matawi. Reli ya kati ni Dar es Salaam – Kigoma na Kigoma - Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa standard gauge kwa hatua hizi wanazoziita hatua za awali unatoka Dar es Salaam kwenda Mwanza. Nilikuwa namuomba Waziri atafute andiko ambalo Mbunge wa zamani Mheshimiwa Ali Karavina aliandika, alikuwa Transport Economist Shirika la Reli wakati ule TRC, angalia takwimu ni wapi ambapo utapeleka reli upate fedha za kujenga maeneo mengine. Kwa sasabu lango la mashariki la nchi yetu ni Dar es Salaam, lango la magharibi la nchi yetu ni Kigoma.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu zinaonyesha kwamba mizigo ambayo Tanzania inahudumia kwa nchi za Maziwa Makuu, nchi ambazo zinaizunguka Tanzania ni tani milioni tano kwa mwaka, kwa taarifa ya hali ya uchumi ya mwaka 2015/2016. Katika hizo asilimia 34 ni Zambia, asilimia 34 Congo, asilimia 12 Rwanda, asilimia sita Burundi, asilimia 2.6 Uganda. Unapoanza na standard gauge matrilioni ya fedha, ukaipeleka Isaka na Mwanza maana yake ni kwamba unaenda kuhudumia mizigo asilimia 15 ya mizigo yote ambayo tunaipitisha unaacha kwenda kuhudumia mizigo asilimia 40, kwa maana ya Congo na Burundi ambayo yote inapita Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, economics gani ambazo mmezitumia katika kuhakikisha kwamba reli inaelekea mahala ambapo hakuna mzigo, economics gani ambazo mmezitumia? Sipendi kusema kwamba Kigoma inatengwa siyo lugha ambayo mimi kama kiongozi napenda kuzungumza. Suala hili takwimu zote za kiuchumi zinaonesha reli inapaswa kwenda kule ambapo kuna faida. Hampeleki kule ambapo kuna faida hii maana yake nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu Waziri, kuna fedha za Benki ya Dunia ukurasa wa 187 wa hotuba yako kwa ajili ya ukarabati wa reli, hata hizi bilioni 200 za ukarabati wa reli ambao upo sasa, hivi na zenyewe mmepeleka kule ambako mnapeleka standard gauge, mnashindwa hata kutudanganya kwa pipi? Hata kutudanganya Diamond aliimba nidanganye nidanganye nidanganye tu, mnashindwa! Angalau mngetupa hizi bilioni 200 mkakarabati reli ikafanya kazi mkapata fedha za kujenga huko ambako mnataka kupeleka standard gauge. Hili jambo naomba mlitazame vizuri, mliangalie kwa sababu haliendani kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata ukiangalia Waziri bandari zako, angalia takwimu za mwaka jana, bandari zipi ambazo zinakua, bandari ya Kigoma growth rate yake mwaka jana twelve percent, bandari zingine zote ni negative growth. Bandari ya Mwanza mwaka jana negative 41 percent mnapeleka reli huko, mnaacha kupeleka reli mahali ambapo mtapata fedha ili mpeleke reli sehemu nyingine. Hebu mtueleze hizi ni siasa, huu ni ukanda au ni uchumi katika maamuzi ambayo mmeyafanya kwa sababu hamueleweki.

Ninaomba jambo hili muweze kulitazama vizuri kwa sababu jambo hili linaleta hisia ya kwamba hamuendeshi nchi kwa mujibu wa Katiba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Katiba Ibara ya 9(d) Serikali ihakikishe kwamba maendeleo ya uchumi ya Taifa yanakuzwa na kupangwa kwa ulinganifu na kwa pamoja. Hizi sentiments mnazisikia za watu wa Kusini, sentiments mnazisikia za watu wa Magharibi hazijengi umoja wa Taifa, hili jambo naomba mlitazame vizuri ili liweze kufanyiwa kazi inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili katika reli ambalo nataka kulizungumzia leo nataka kuongea na reli tu. Pili, what are offsets agreements katika uchumi huu wa reli? Tunatenga fedha nyingi sana kwa ajili ya ujenzi wa reli. Tunawezaje ku- link ujenzi huu, kipindi hiki cha ujenzi na ukuaji wa sekta ya viwanda. Forwards na backwards linkages kwenye mikataba mmezitazama namna gani? Waziri nakuomba google tu kwenye Ipad yako hapo kitabu cha Transport and Developing Countries kimeandikwa na Dr. David Hilling. Kinaeleza namna ambavyo in 18th century ujenzi tu wa reli ulivyoweza ku- transform uchumi wa Italy.

Nheshimiwa Naibu Spika, tunaweza kabisa juhudi zetu za ujenzi wa viwanda tukazi-link na ujenzi wa reli, tusifanye makosa tuliyoyafanya kwenye bomba la gesi la Mtwara, ambapo kila kitu kilichofunga lile bomba kilitoka China. Leo bomba linatumika only six percent hamna maendeleo yoyote ambayo tumekuja kuyapata kama nchi mpaka sasa. Kwa hiyo, naomba hili jambo mliangalie forward and backward linkages, iangalieni hiyo mikataba upya. Offsets agreements ni muhimu sana kwenye mikataba mikubwa namna hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho katika hili la reli ni suala la kwa nini wenzetu Ethiopia walikosa fedha kama sisi tunahangaika kutafuta fedha, wakatoa bond ya wananchi, sovereign bond ya wananchi, especially diaspora wakanunua kujenga The Millennium Dam ambayo inatengeneza ten thousand megawatts za umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Hussein Bashe ameongea asubuhi hapa, ili tufaidike vizuri badala ya reli kuishia Morogoro, kipande hiki na kipindi hiki cha miezi hii reli ingefika Makurupora na mkaweka dry port pale Makutupora, kwa sababu mnakuwa na long haulage, unakuwa na economies of scale kwenye reli, lakini tunajua hatuna fedha, shirikisheni wananchi tupate fedha ya kufanya kipande hiki kwa kutoa bond, fifteen years. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leteni sheria hapa kwenye Bunge, tutunge sheria ambayo kila mwaka tuta-allocate a certain amount of budget kwa ajili ya kulipia hizo percent ambazo tutaliwapa hao watu, ambao ni bond holders, after fifteen years tutakuwa tumefanya hiyo kazi, tumejenga reli na hamtakuwa mnahangaika. (Makofi)

Mheshimia Naibu Spika, ninyi mnajifungia ndani wenyewe, hamtaki kusikia mawazo ya watu wengine, watu wengine wakizungumza mnaona kama wanapinga, hakuna mtu ambaye anaweza kupinga maendeleo ya nchi kwa sababu ni maendeleo yetu wote. Kwa hiyo, nilikuwa nawaomba mtazame jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, angalieni uwezekano wa kuwa na railways bond angalau kipande ambacho mnataka kiishie Morogoro, kiishie Makutupora ili tuweze kupata fedha za kujenga maeneo mengine, vinginevyo hatutaweza kwenda huko tunakotaka kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maelezo yangu mengine nimeyaandika kwa maandishi, nadhani nimeshaleta, mtaweza kuangalia namna gani mtakavyoweza kujibu. Nawashukuru sana.