Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema na mwingi wa Utukufu aliyenijalia kusimama hapa siku hii ya leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii nami kuchangia Wizara ya Miundombinu. Nianze na usafiri wa anga. Nachukua nafasi hii kumpongeza sana Rais wangu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri ya kusimamia kikamilifu utekelezaji wa ilani, lakini pia kuwezesha ndege hizi sasa kuweza kufanya usafiri ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa leo nikiwa nina furaha sana na niwashirikishe Wabunge wenzangu kwamba keshokutwa tarehe 30 ni siku maalum kabisa ambapo ndege aina ya bombardier itaanza safari zake kutoka Dar es Salaam kuelekea Songea. Naishukuru sana Serikali yangu, kitu kama hiki kilikuwa ni ndoto, lakini kwa kudra za Mwenyezi Mungu na kwa jitihada za Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli imewezekana kwa kipindi kifupi cha mwaka mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kwenye barabara. Kuna barabara ambayo ina changamoto kubwa sana. Barabara hii ni barabara yenye urefu wa kilometa 66 inayotoka Mbinga kwenda Mbamba Bay. Naomba barabara hii sasa ianze kutengenezwa kwa sababu ina muda mrefu, imekuwa katika mpango lakini pia tayari upembuzi yakinifu umeshafanyika, ianze kutengenezwa sasa kwa kipindi hiki cha mwaka 2017/2018 ili kuweza kuunganisha mkoa mzima na hata kufikia kule katika Ziwa letu la Nyasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapo sasa tutakuwa tumeshawezesha ile Mtwara Corridor kuwa tayari imeungwa kutoka Mtwara mpaka kufika Mbamba Bay ambapo sasa tunaweza tukasafirisha bidhaa mbalimbali kwa kutumia usafiri wa maji kutoka Mtwara na hata kupeleka mpaka Malawi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niende kwenye barabara ya Likuyufusi. Barabara ya Likuyufusi – Mkenda ni barabara yenye urefu wa kilometa 24 na ni barabara ambayo inaunganisha Mkoa wa Ruvuma na nchi yetu ya Msumbiji; kwa maana ya nchi ya Msumbiji na nchi yetu ya Tanzania. Ni barabara ambayo ikishajengwa kwa kiwango cha lami, itainua uchumi wetu wa Tanzania kwa kuunganisha mipaka hii miwili na kufanya biashara kama nchi marafiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende pia kwenye barabara ya Kitahi – Lituhi – Mbamba Bay. Hii barabara imekuwa ikipigiwa kelele sana, lakini kwa masikitiko makubwa, sijaona ikitengewa pesa kwa kipindi cha mwaka huu 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii inasikitisha sana na hii ni barabara muhimu ambayo kimsingi kama mnasikia makaa ya mawe yanayochimbwa katika Mkoa wa Ruvuma, basi barabara hii ni ile inayotoka Kitahi kwenda mpaka kwenye yale machimbo na kufikia Lituhi na hatimaye kwenda kuunganisha mpaka Mbamba Bay; inapita kwenye uwanda pembezoni mwa Ziwa Nyasa mpaka kufika Mbamba Bay. Mbamba Bay ni mahali ambapo tayari sasa hivi kumeshakuwa na uwekezaji mkubwa wa mambo ya utalii, lakini nashangaa hii barabara haiunganishwi hata kuweza kuwezesha watalii kuweza kufika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ina umuhimu mkubwa na ukizingatia kwamba magari makubwa yanayokwenda kuchukua makaa ya mawe kule katika eneo lile linalochimbwa makaa ya mawe; ni magari ambayo yanatimua vumbi kiasi ambacho wananchi wanaoishi pembezoni mwa zile barabara tayari asilimia kubwa wanaathirika kutokana na zile vumbi, wanapata maradhi ya aina mbalimbali, lakini pia inachelewesha hata namna ya kutoa makaa ya mawe na kupeleka labda Mtwara kule ambako huyu mwekezaji ambaye anazalisha cement kwa wingi anachukua makaa ya mawe kule. Siyo huko tu, viwanda vyetu vingi sasa hivi vinatumia makaa ya mawe. Kwa hiyo, barabara ile ni muhimu ili kuweza kurahisisha uchumi wetu tunaoutarajia; uchumi wa kati kufikia mwaka 2025. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara nyingine ya Lumecha – Londo. Barabara hii inaunganisha Mkoa wa Ruvuma na Morogoro. Barabara hii toka tumeanza kuiimba, ni muda mrefu na sijaona kama imetengewa pesa. Namwomba Mheshimiwa Waziri, tafadhali sana naomba atenge pesa kwa ajili ya kuunganisha hii barabara inayotoka Lumecha hatimaye kwenda Londo, Mkoa wa Morogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ambayo inatoka Mtwara Pachani kuelekea Narasi. Barabara hii kwa kweli wanasema hivi, mtu naweza akasahau kwake, akapata sungura wa kugawa, akagawia maeneo mengine akasahau kwake. Namwona kabisa kaka yangu Mheshimiwa Ngonyani Naibu Waziri wa Miundombinu amesahau; na leo nimeona nisimame hapa niisemee. Barabara hii iko katika Jimbo lake lakini naona kama ameisahau. Naomba Mheshimiwa Waziri tafadhali juu ya tafadhali, naomba utusaidie hii barabara ili iweze kutengenezwa kwa kiwango cha lami iweze kusaidia wananchi wa Namtumbo lakini pia na wananchi wa Tunduru. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii imeweka changamoto nyingi sana kiasi ambacho akinamama wengi wanaopata shida za namna ya kujifungua kwa kweli siku ya uwasilishi hapa wa Wizara ya Afya, jamani nitawaletea na picha ili mwone wanawake wa Namtumbo wanavyopata shida hasa maeneo ya kule pembezoni kuelekea Namtumbo na kuunganisha na Tunduru. Wanapata shida kubwa sana kiasi ambacho wanabebwa mpaka kwenye matenga, barabara ni shida, magari hayawezi kwenda huko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri barabara hii. Naomba sana Mheshimiwa Waziri amsaidie ndugu yake huyo Naibu Waziri aliyeko hapo ili aweze kupata hii barabara. Barabara hii ina changamoto kubwa sana; akina mama wanapoteza maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hebu siku moja hawa wanaume na wenyewe wangeonjeshwa wakaona uchungu wa kuzaa, ndiyo pale wangeweza kujali na kuthamini hata wakaona umuhimu kwa barabara ambazo tunaziomba kwa machungu waweze kutuunganishia. Akinamama wanapoteza maisha! Nasikia uchungu sana, natamani kulia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ambayo inatoka Lingusenguse kuelekea Tunduru, nayo ni ya Mheshimiwa Naibu Waziri katika Jimbo lake. Anashindwa kusema, mimi naona nimsemee hapa kwa sababu yeye yuko hapo. Naomba umsaidie hii barabara pia ina changamoto kubwa. Tafadhali juu ya tafadhali, tusaidieni, wanawake wa Namtumbo wanapoteza maisha, wanawake wa Tunduru wanapoteza maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niende kwenye barabara ya Nangombo – Chiwindi yenye urefu wa kilometa
19. Barabara hii ni barabara ambayo iko kwa dada yangu Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya, anafuatilia pole pole, lakini mimi leo nimesimama hapa kindakindaki nimsaidie kumsemea mwanamke mwenzangu. Barabara hii nayo ina changamoto kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba barabara hizi nilizozitaja hapa zilizopo ndani ya Mkoa wa Ruvuma, endapo zitatengewa fedha, katu hutaniona nikisimama hapa nikiongelea barabara tena katika Mkoa wa Ruvuma. Kwa maana moja ama nyingine, tutakuwa tumemaliza matatizo ya barabara katika Mkoa wa Ruvuma. Naomba tafadhali sana mwaka huu wa fedha muweze kutenga fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia barabara hii niliyosema ya Kitahi – Lituhi, Mheshimiwa Waziri kama hataitengea fedha atakapokuja ku-wind up hapa, haki ya Mungu nitashika shilingi. Nimhakikishie kabisa nitashika shilingi kwa sababu ni barabara ambayo ni muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kwamba nakushukuru sana na naunga mkono hoja.