Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Livingstone Joseph Lusinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba nikushukuru sana kwa kunipa fursa hii ili na mimi nichangie kuhusu hizi Wizara mbili. Wabunge wengi wamepongeza na mimi nawaunga mkono kwa pongezi walizotoa kwa Waheshimiwa Mawaziri kwa uchapakazi na hata zile tahadhari zilizotolewa kuhusu namna gani wanatakiwa kukaza buti kwa ajili ya kuhakikisha Taifa linasonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hizi ni Wizara nyeti sana na zimepewa watu barabara kabisa ambao wanafanya kazi kwa ufanisi na weledi mkubwa. Kazi yetu siis kama Wabunge ni kujaribu kuonesha ni maeneo gani Serikali iyatilie mkazo na ni maeneo gani yanahitaji uangalifu mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mbunge kutoka jimbo la Mtera na ni jimbo la vijijini, naiomba Serikali itazame kwa jicho la huruma sana majimbo ya vijijini. Hata hili ongezeko la watu mijini tunalolisema linatokana na vijijini kukosa huduma nyingi za msingi, huduma nyingi za msingi zikipatikana vijijini, nataka niwahakikishie mlundikano wa watu mijini utapungua kwa kiwango kikubwa. Tukizungumzia maji safi tunazungumzia mjini, tukizungumzia umeme wa uhakika, tunazungumzia mjini na tukizungumzia matibabu ya uhakika tunazungumzia mjini. Vijijini watu hawatakaa, watakimbilia mijini ili waje wapate huduma hizo muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namuomba sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, suala la kuhakikisha kila kata, hata ikiwezekana kila tarafa ipate kituo cha afya cha uhakika, gari la kubeba wagonjwa la uhakika, hii itasababisha watu wabaki vijijini na wasukume mbele gurudumu la maendeleo. Tukiweka bajeti kubwa za maji mijini, tukaweka bajeti kubwa za afya mijini, watu wa vijijini hakuna namna yoyote ya kuwaacha wao wakae vijijini wasije huko mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie barabara. Barabara za vijijini Halmashauri nyingi hazina uwezo wa kuzitengeneza. Uharibifu wa barabara ni mkubwa! Kuna majimbo ni makubwa mno. Kwa mfano, Jimbo langu mimi, ukitoka hapa ilipodondoka treni wakati ule, ukatoka Igandu mpaka mwisho Ilanga kuna kilometa zaidi ya 220; haiwezekani ambulance ziwe mbili au moja, inachakaa haraka kabla ya muda, kwa sababu inapita kwenye barabara mbovu halafu hazitoshi ambulance zenyewe. Kwa hiyo, naiomba Wizara ya TAMISEMI ihakikishe inatoa msukumo mkubwa kwenye bajeti za kutengeneza barabara za ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumza na Waheshimiwa Wabunge hapa, wamesema sana kuhusu Halmashauri zetu, kwa Waheshimiwa Madiwani. Tunawapozungumzia Waheshimiwa Madiwani kuna baadhi ya Halmashauri Madiwani wana hali mbaya, hata posho zao zile stahili zao hawapati, sembuse hiyo ya kuongeza! Hawapati hata zile za ndani za kwao. Wanakopwa kuendesha vikao, kwa sababu ya ugumu wa Halmashauri; katika vyanzo vya mapato wengine wanategemea kilimo; ukame umekuja, hawawezi kukusanya mapato ya ndani. Kwa hiyo, hata hiyo asilimia 10 tunazosema wapewe akina mama na vijana haziwezi kupatikana kwa sababu Halmashauri hazina makusanyo ya kutosha. Zile kodi za kero zilizofutwa, hakikisheni Serikali mnazifidia kuzilipa Halmashauri ili zipate uwezo wa kujiendesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumza sana kuhusu mapato ya Madiwani, tukiyaboresha Diwani ndio anayezika, anauguza, anasomesha. Akibaki na mapato yake madogo Diwani anakimbilia kwa Mbunge, anamkuta vilevile naye yupo taabani, inakuwa shida kubwa sana kuendesha majimbo. Kwa hiyo, naomba sana Waheshimiwa Madiwani wapewe uangalizi mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia maji. Miradi ya maji inasuasua sana. Ukienda unakuta hela ipo. Nauzungumzia mradi wa Kata ya Manzase, umechukua muda mrefu sana. Tumempeleka Katibu Mkuu wa CCM, tumempeleka Waziri Mkuu, Mzee Pinda na ndio alikuwa aufungue, imeshindikana. Leo ukienda anakwambia BOQ imefanyaje; ukienda wanakwambia mkandarasi sijui amefanyaje, wananchi hawataki kusikia maneno, wanataka kuona wanapata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imefika wakati mpaka wananchi wanakata tama. Mheshimiwa Jafo kaenda pale kasukuma akaweka na tarehe, lakini bado. Wanakwambia sijui tutangaze tenda upya, tubadili kutoka mfumo wa diesel kwenda solar, maneno hayatusaidii, tunataka maji katika katika Kata ya Manzase, hatutaki maneno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumze kwa utulivu sana kwenye suala la ulinzi na usalama; nadhani juzi sikupata muda wa kutosha. Nashauri Serikali iunde dawati kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani au Wizara yoyote, ambalo wananchi watakwenda kuripoti pale juu ya ndugu zao waliopotea. Tusizungumze pale anapopotea mtu maarufu tu, Watanzania wengi sana wamepotea katika mazingira ambayo watu wengi hawajui wako wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tengenezeni dawati halafu mruhusu wananchi waje watoe taarifa za upotevu wa ndugu zao, mtashangaa idadi ya watu waliopotea bila taarifa.

Kwa hiyo, nashauri Serikali badala ya kulaumiana sisi wenyewe sijui kuna kikundi kinafanya nini, nilisema juzi mimi mwenyewe ni muhanga, nina mjomba wangu anaitwa Nikanoli, aliondoka mwaka 1980 mpaka leo hatujui yuko wapi. Wala siyo maarufu, wala hakuwa Balozi wa Nyumba Kumi useme ametekwa; aliondoka akapotea. Yupo mwingine alikuwa anaitwa Yoel, ameondoka tangu miaka ya 1970, hata kumjua watu hawamjui. Kwa hiyo, ukienda kwa kila Mbunge inawezekana ukakutana na taarifa za upotevu wa watu kwenye majimbo mengi sana, kama siyo yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali, badala ya kuanza kushutumiana sijui nani anafanya nini, tutengeneze dawati watu wapeleke habari za upotevu wa ndugu zao, za upotevu wa jamaa zao ili waweze kutafutwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge hapa tunazungumzia juu ya heshima na Daktari tena kazungumza vizuri sana. Daktari akasema tubadilishe fikra na huu ni mchango wake karibu wa pili anatushauri tubadilishe fikra kwamba tuwe na mtazamo mpya. Sina hakika kama yeye anao, lakini anasema katika huo mtazamo mpya, tuache kushughulika na watu wadogo wanaomtukana Mheshimiwa Rais. Ila Daktari huyo huyo anayetaka tubadilishe fikra, anasema Kiongozi wa Upinzani aheshimiwe ni mtu mkubwa. Mheshimiwa Rais atukanwe, Mheshimiwa Mbowe aheshimiwe, hatuwezi kwenda hivyo! (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunataka heshima, turudi kwenye Katiba inayosema kila mtu anastahili heshima, bila kuangalia cheo chake. Watanzania wanastahili heshima, Mheshimiwa Rais anastahili heshima, Kiongozi wa Upinzani anastahili heshima, Mbunge anastahili heshima, Diwani anastahili heshima. Tutaheshimiana na tutaona kuendesha nchi ni kazi rahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukibadili fikra zetu tukaacha eti watu wadogo wadogo wanamtukana Mheshimiwa Rais kwenye simu, hao tusishuhulike nao, ila tushughulike na viongozi waliotengeneza, aaah, sidhani kama ni sawa sawa!

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nalishauri Bunge hili, kama tunataka kutoka hapa tulipo, kwanza kuna baadhi ya mazoea tuyaache. Pale tunaposema tunahitaji mabadiliko kwenye nyanja fulani, nina hakika kabisa Mheshimiwa Rais anafanya kazi nzuri kabisa ya kubadilisha mfumo wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi yetu kubwa badala ya kumrudisha nyuma tumpe moyo, tumtie nguvu, Mawaziri tuwape moyo, tuwatie nguvu wasukume gurudumu mbele. Nani asiyejua maeneo mengi yaliyokuwa yamesimama? Wizara kama ya Ardhi ilikuwa na matatizo chungu nzima! Tulikuwa na kesi chungu nzima, lakini sasa hivi zinatatuliwa kwa speed kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe sana, tunapozungumzia heshima tuzungumze pande zote mbili. Nataka niseme kwamba, jana ilitolewa hoja hapa, watu wameidharau na wengine wakaona kama inachomekwa. Nasikia ninyi mna vyombo hapa mnaweza kutuambia, kuna Mbunge amekamatwa na konyagi anaingia nayo Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi juzi hapa Serikali imemwajibisha Kitwanga kwa kudhaniwa tu amelewa, akawajibishwa. Leo Mbunge anaingia na konyagi ndani ya Ukumbi wa Bunge, huko amekamatwa. Tunataka tuone na ninyi meno yenu yako wapi katika kumwajibisha huyo Mbunge, kama mtaweza! Maana kazi yenu ni kusema tu, siyo kutenda. Bahati nzuri Mbunge mwenyewe anatoka upande huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka tuone mtakuwa wakali kwa kiwango gani kwa Mbunge anayeingia amelewa, halafu ana chupa ya konyagi ndani ya eneo la uzio wa Bunge! Sisi tumeshaonyesha njia, Mheshimiwa Waziri amekuja anatikisika, hana chupa, hana nini, mkasema ooh, amelewa sijui nini na Uwaziri kaupoteza. Ninyi sasa tuone sasa mtachukua hatua gani ili...(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na ahsante sana.