Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim M. Majaliwa, kuhusu hatuba ya Bajeti aliyoiwasilisha Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika kipindi cha mwaka mmoja wa Uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mengi yamefanyika. Nampongeza sana juhudi zinazofanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza juhudi zinazofanywa na Mheshimiwa Rais kuhakikisha Serikali inahamia Dodoma. Bado napenda kukumbusha sheria ya kuhamia Dodoma haijapitishwa katika Bunge lako Tukufu. Je nini kinasababisha ucheleweshaji wa utungaji wa Sheria
hii. Pamoja na nia nzuri ya Serikali kuhakikisha Dodoma inakuwa Makao Makuu, kumekuwa na malalamiko ya baadhi ya wananchi katika maeneo mbalimbali mfano Nkuhungu Centre, Kiwanja. P. 639 wanalalamika pamoja na kulipia viwanja vyao lakini wengine wamenyang’anywa kwa madai wameshindwa kuviendeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linaweza kuleta mgogoro mkubwa sana kati ya Serikali na wananchi, hata kama kuna baadhi ya wananchi wameshindwa kuendeleza maeneo ni vema wakapewa taarifa ili ithibitike mapema isiwe Serikali inapokea pesa ya kodi na baadhi ya wananchi
wanazo slip za Bank ambazo wamekuwa wanazilipia kodi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kuwa Serikali hii ni sikivu ni vema kufuatilia kwa ukaribu jambo hili ili kupata ukweli. Pia Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu hayo inatakiwa itende haki kwa wale wote waliovamia maeneo, hali kadhalika Kamati za Makazi nazo zifuatiliwe kwani kuna baadhi ya Wanakamati hao wanafanya udanganyifu wa kuuza maeneo bila kufuata utaratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza Serikali suala la ukusanyaji mapato unaofanywa na TRA, lakini mamlaka inabidi itumie mbinu mbadala ili ulipaji kodi uwe hiyari na wananchi waone ulipaji kodi ni wajibu wa kila Mtanzania. Kwani mtindo unaotumika wa kutumia maaskari na mabunduki mengi inaleta hofu. Ushauri wangu elimu ya mlipa kodi au ulipaji kodi ni kwa ajili ya maendeleo ya nchi katika masuala yote ya kijamii, elimu, afya, miundombinu, kilimo na ufugaji ni kwa maendeleo ya Watanzania wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kuweka dhamira ya dhati katika kuendeleza kilimo cha biashara, pamoja na kuzalisha mbegu za nafaka ni budi pia kilimo cha biashara cha mbogamboga ambacho kimeanza kuwa na tija na kikitiliwa mkazo kitasaidia kupunguza
umaskini kwani kilimo cha mbogamboga mfano matikiti maji, matango, carrots, hoho, vitunguu, nyanya na mboga zingine zinaweza kuongeza pato la Taifa, iwapo Taifa litaweka mkazo na kufanya tafiti zaidi na kuzalisha mbegu za mbogamboga. Ili zizalishwe kwa wingi, kwa bei nafuu ili ikiwezekana mazao ya mbogamboga yaweze kuzalishwa kwa wingi na hatimaye kusafirisha nchi mbalimbali duniani. Kwani uhitaji wa mazao ya mbogamboga ni mkubwa sana na una tija kwa wazalishaji mazao hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ukame na njaa, pamoja na wadudu waharibifu nalo ni jambo la kuliangalia kwa jicho tofauti. Kutegemea mvua katika kilimo bado kunasababisha njaa, kwani mvua hazitoshelezi kutokana na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi, hivyo ni budi Serikali ijikita katika kilimo cha umwagiliaji na pia uvunaji maji ya mvua ili yatumike kumwagilia kipindi cha kiangazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya maeneo ikiwemo kanda ya Kati, Mikoa ya Dodoma na Singida, pia baadhi ya mikoa inayolima mazao ya mtama, mfano Shinyanga kumekuwa na tatizo la ndege waharibifu ushauri wangu Serikali ifanye utaratibu wa kupata ndege yake ili inapotokea uharibifu wa ndege iwe rahisi kutekelezwa kwa haraka kuliko kusubiri ndege ya kutoka Nairobi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa vita dhidi ya rushwa na madawa ya kulevya. Bado mkazo utiliwe na Serikali kutoa elimu kwa jamii waone ubaya wa rushwa, pia kwa vijana kujihusisha na madawa ya kulevya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kujenga uchumi na viwanda na kuimarisha viwanda vyetu bado naendelea kushauri, wananchi wa Tanzania wahamasishwe kuzalisha malighafi kwa ajili ya kuhudumia viwanda. Kwani tukiwa na viwanda halafu malighafi ikaletwa kutoka nje haitakuwa na maana. Ni budi Serikali ikaweka mkakati wa makusudi ili kuhakikisha malighafi zaidi zinazalishwa nchini ili ziweze kukidhi mahitaji ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza ujenzi wa miundombinu vijijini unaotekelezwa na kampuni ya Viettel, je, ni ofisi ngapi za Wakuu wa Wilaya zimepatiwa miundombinu ya mitandao ya Internet nauliza jambo hili kwa sababu baadhi ya Ofisi za Wakuu wa Wilaya hazina huduma
za Internet. Nahitimisha kwa kumpongeza tena Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono.