Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Zubeda Hassan Sakuru

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. ZUBEDA H. SAKURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuweza kunipa nafasi hii kujadili hotuba ya Waziri Mkuu katika kupitia mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka huu wa fedha wa 2017/2018. Pia nitoe pole kwa familia ya Mbunge mwenzetu Dkt. Elly Macha aliyefariki nchini Uingereza na naungana na wana CHADEMA wote kufikisha salamu hizi kwa familia yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuweka wazi kuwa naunga mkono kwa asilimia mia moja maoni ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe na naamini kwamba Serikali itaenda kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Baba wa Taifa alipata kusema maneno yafuatayo naomba niyanukuu: “tunataka kuona katika Taifa hili vijana jeuri na wenye kujiamini siyo vijana waoga akina ndiyo Bwana Mkubwa, vijana wenye ujasiri wa kuhoji na kupiga vita mfumo wa jamii isiyoshabihiana na matakwa na matarajio ya jamii ya Kitanzania na tunataka kuona vijana waasi dhidi ya mfumo kandamizi, ubwana na ufisadi katika Taifa”. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kijana nauliza swali ambalo vijana wenzangu wa Tanzania wanauliza where is Ben Saanane? Tunapozungumza leo hii kijana aliyezaliwa na mwanamke na Watanzania tunajua usemi wa Kiswahili unaosema “uchungu wa mwana aujuae mzazi” kijana wa watu Ben Saanane ana takribani miezi sita haonekani, hajulikani alipo, itakuwa ni kosa kubwa kama Bunge tukinyamaza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna taarifa mbalimbali zimeletwa mbele yetu, katika mijadala hii kunaonekana kwamba kulikuwa kuna namba 0768-797982 iliyosajiliwa kwa jina la Emmanuel Joseph, ndiyo iliyotuma ujumbe wa vitisho kwa Ben Saanane. Wasiwasi wangu kama kijana ambaye leo hii nipo katika siasa lakini siasa za upinzani na wasiwasi alionao Mama yangu Doris Harold Mboni alipo ni kwamba je, nini hatma yangu kesho?(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza mwezi Oktoba, 2016 kulitokea uvumi wa aliyekuwa Mkuu wa Majeshi Nchini Devis Mwamunyange kwamba amelishwa sumu. Uvumi huu ulianza tarehe 2 Oktoba, 2016 lakini ukaja kufupishwa kwa kumpata kijana aliyetuma na kuanzisha
ujumbe huu kupitia TCRA na Jeshi la Polisi, tunachouliza ni kitu gani kifanyike, ni aina gani ya hasira na maumivu ya wazazi wa Ben Saanane waliyonayo wayafanye ili TCRA na Jeshi la Polisi liseme huyo aliyetuma ujumbe ni nani? yuko wapi na wamechukua hatua gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu wana CCM pamoja na wana CHADEMA na wana CUF hakuna dhambi kubwa duniani kama dhambi ya uoga, uoga huanza kumtafuna mmoja baada ya mwingine. Tumeimbiwa juzi hapa na kijana mwenzangu Diamond anasema tupige kimya, mimi kama tunda la aliloliacha Baba wa Taifa sitokaa kimya nikiwa kijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini Waziri Mkuu kwa sababu tunapozungumzia hali ya kisiasa nchini ni lazima tuzungumzie tension iliyosambaa. Mimi kama Mbunge naweza nikajihakikishia usalama wangu lakini kwa wanaonipenda, familia yangu, jamaa zangu nawahakikishia nini? Tunapokaa hapa sasa hivi tunaongelea hali ya kisiasa kuwa nzuri nchini lakini kuna video zinatapakaa za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaama akivamia kituo cha Television (Clouds Media) Waziri Mkuu hajazungumzia kitu chochote. Pamoja na kwamba hawa ni wateule wa Rais lakini ipo haja Waziri Mkuu kuzungumza haya kama Msimamizi Mkuu wa shughuli za Serikali hapa Bungeni na tulitegemea kwamba hili litaonekana hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo linasikitisha sana ni kuhusu pension ya Wazee ambayo iko chini ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Mwaka 2010 hii Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na kwa kuwa ilikuwa katika ilani ya Chama cha Mapinduzi, wazee waliahidiwa pensheni, leo miaka 15 baadaye hakuna anayezungumzia pension ya wazee ambayo ilisemwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Mwaka 2005 na 2010 ni dhahiri kuwa, waliokuwa wapigaji kura wakubwa walikuwa ni wazee, sasa leo tunawaachaje? Itakuwa dhambi kubwa sana kuhitimisha mjadala huu bila kuhakikisha Serikali inatekeleza ahadi yake ya kuhakikisha wazee wote nchini wanapata pension. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia kuzungumzia kuhusu watu wenye ulemavu. Ni haki na wajibu wa walemavu kupata huduma zote za kijamii kama ambavyo tunapata sisi wengi lakini hali ikoje? Tukijiangalia na kufanya tathmini katika sekta mbalimbali za huduma za jamii, je, walemavu wamewekewa mazingira rafiki, kuwawezesha kupata haki zao za msingi kama tunavyopata wengine? Ukienda hospitalini, hakuna hata kitu kimoja kinachoonesha kwamba haya mazingira ni rafiki kwa walemavu, ukienda katika sekta ya elimu huwezi kukuta mazingira rafiki kwa ajili ya walemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna mikakati imewekwa ambayo Serikali inasema kwamba imejaribu kuyajibu haya lakini kwa kiwango kikubwa mtu mlemavu anayezaliwa katika familia ya kimaskini anakuwa ameachwa kama alivyo. Sasa ni wajibu wetu kama Wabunge kuendelea kuikumbusha Serikali kuhakikisha inajenga mazingira wezeshi kwa watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira rafiki au mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara; tarehe 2 Februari, 2017, Waziri Mkuu alitoa katazo la uuzaji wa viroba. Hakuna asiyepinga matumizi ya viroba nchini, lakini je, hili katazo lilikuja kwa wakati na je, lilikuwa rafiki kwa wafanyabiashara?
Mfanyabiashara wa Dodoma tulioneshwa hapa amejipiga risasi shambani kwake kwa sababu alichukua mkopo. Tunasemaje kwamba tunajenga mazingira wezeshi wakati Serikali inatoa matamko bila kufikiria athari zake mbadala zinazojengwa kwa wafanyabiashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kwa ubaya gani kwa Waziri Mkuu kuzuia uzalishaji wa viroba nchini halafu wawape muda au grace period hawa wafanyabiashara warudishe viroba viwandani vifanyiwe packaging inayotakiwa ili kuhakikisha kwamba hawa watu wanaweza kurejesha mikopo yao. Leo hii mtu amejiua kwa hasara ya karibu bilioni mbili, bilioni tatu, Waziri Mkuu anasemaje kuhusu hicho kitu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mtu ambaye anapenda matumizi ya viroba hapa, kwa sababu mwisho wa siku hivi viroba mnavyokataza vinaenda kutengenezwa upya katika ujazo mwingine na mnasema kwamba matumizi yake wanatumia vijana, hapana. Leo ukienda kwenye
maduka ya reja reja mtoto wa miaka saba, nane anatumwa kwenda kununua sigara, kuna mtu anayezungumzia hiki kitu au kwa sababu sigara imeandikwa ni hatari kwa maisha yako? Ni lazima tuhakikishe kwamba, tunawawezesha wawekezaji na wafanyabiashara nchini kwetu mazingira ya kubadilisha maisha kwa kupitia matamko yatakayowajenga na siyo kuwabomoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tumeona kwamba kuna baadhi ya makampuni nchini ambayo yanawafanyisha watu kazi bila ya kuwa na mikataba ya ajira. Je, Serikali inaliona hili? Kamati ya Miundombinu tulipita katika makampuni mengi ya simu na tukaona kwamba kuna
wafanyakazi ambao wanafanya kazi nchini lakini hawapewi mikataba ya ajira na hii mwisho wake inasababisha wao kushindwa kupata stahiki zao za kazi. Naamini kwamba Serikali inaweka mkakati wa kuhakikisha kwamba mikataba ya kazi katika sehemu za ajira inapewa kipaumbele na Watanzania hasa wazawa wanapata stahiki zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nije kwenye jambo moja la msingi; Tanzania ni yetu sote, Tanzania haitojengwa na CHADEMA peke yake, haitojengwa na CCM peke yake, ndiyo maana leo hii fedha za miradi ya maendeleo hazitoki Lumumba, mnakusanya kwa Watanzania waliowachagua na wasiowachagua, mnakusanya kutoka kwa wana CHADEMA na wasio wana CHADEMA, sasa tunapokuja tunajinasibu kwamba hii ni mikakati ya Serikali, hata TLP ingepewa dhamana ya Serikali, ingesimamia kwa sababu ni wajibu wa kila Chama kusimamia….
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Sakuru.