Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Pauline Philipo Gekul

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mimi nina mambo machache, naomba dakika zangu tano nimgawie Mheshimiwa Selasini, Mbunge wa Rombo, tembo wanamsumbua Jimboni kwake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni suala la chakula. Wakati Waziri wa Kilimo akieleza hali ya chakula nchini alisema kuna Wilaya zaidi ya 56 kama sikosei zina upungufu mkubwa, lakini Wilaya hizo hatujapewa list, ninaitake Serikali watupe majina ya Wilaya hizo tuzifahamu na ni lini sasa chakula kitaenda, kwa sababu wananchi wetu wana hali mbaya sana.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyoongea wananchi wangu wa Jimbo la Babati Mjini debe moja la mahindi wananunua kwa shilingi 20,000. Naomba nifahamu mnapeleka lini hicho chakula kwa wananchi wetu kwa sababu hali ni mbaya na mliwambia kwamba wauze ng’ombe hata watatu wanunue debe moja, hao ng’ombe watatu hata bei haifiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tumeenda Karatu tumeona ng’ombe wamedondoka barabarani wamekufa, sasa hata ng’ombe kumi hawatoshi kupata shilingi 20,000. Mtuambie mnapeleka chakula lini hasa kwa wananchi wangu wa Babati wana hali ngumu kweli na mvua hazijanyesha. Wakati mwingine viongozi wa juu tuangalie kauli zetu, huenda hata Mungu anatuadhibu kwa ajili ya kauli zetu, mlisema hamtoi chakula, mvua ikaacha kunyesha, saa hizi hali mbaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu Kamati iliyoundwa. Hii Kamati ya Migogoro ya Ardhi ya Wakulima na Wafugaji ni Kamati ambayo inahusisha Wizara zaidi ya tano, mpaka leo hamtuambii hiyo Kamati imefika Wilaya ipi? Hamtuhusishi Wabunge na Madiwani huko chini tufahamu hiyo Kamati, tuliuliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Maliasili, Ardhi na Mazingira, lakini huko kila tukizungumzia migogoro ya ardhi, wakulima na wafugaji mnatuambia Kamati iko site, mtuambie iko wapi? Imeanzia wapi? Imefikia wapi? Hiyo schedule mtupatie Wabunge ili tufuatilie, mkitujibu tu humu ndani mkatuambia Kamati iko site, watu wanauana haina maana yoyote Waheshimiwa Mawaziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtuambie iko wapi, mje na Babati huku, anzieni huko pia. Morogoro kule watu wanauana, Wabunge tushirikishwe hiyo Kamati tuipe ushirikiano mgogoro huo wa wananchi wetu kuuana uishe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni suala la kodi ya ardhi. Katika bajeti iliyopita Waheshimiwa Wabunge kodi ya ardhi tukasema TRA ikusanye, sasa hivi Halmashauri zetu hawakusanyi tena lakini TRA hawana manpower,haya maduhuli ya Serikali hayakusanywi tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri tu Wizara ya Ardhi, mlikuwa mnatuletea asilimia 30 retention ya premium, sasa hivi hizo pesa zingetusaidia hata kununua vifaa, Halmashauri zetu hatuna vifaa vya upimaji ndiyo maana ardhi kubwa ya Tanzania haijapimwa. Leo badala ya kuwezesha Halmashauri zetu wabaki na hizo retention za 30 percent mlipitisha kwenye bajeti mwaka jana, wakati mmetufukuza mkapitisha, mkasema TRA wakusanye. TRA hawakusanyi, hawana manpower. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Serikali kwamba rudisheni sasa kazi hiyo kwa Halmashauri zetu ili kazi ya upimaji ardhi katika Halmashauri zetu iende sambamba na suala zima la upatikanaji wa fedha. Kwa sababu ile 30 per cent ilikuwa inatusaidia. Kama TRA hawakusanyi mwaka mzima kwa nini msifanye maamuzi? Kazi kwenu, wakati wa bajeti kaeni chini mfikirie siyo kodi tu ya ardhi, lakini pia hata kodi ya majengo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni suala la fedha za maji, fedha za maji kuna mlango wa Wizara ya Maji, mna bajeti yenu huko haiko wazi sana, lakini kuna TAMISEMI na kuna Halmashauri zetu. Kwenye Halmashauri mnatupa ceiling ndogo sana Mheshimiwa Waziri. Kaeni chini muweze ku-reconcile pamoja vyanzo vyote vya fedha za maji ili Wabunge tujue kwamba miradi mikubwa tupitishie milango ipi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri ulikuja Babati katika Jimbo langu, pale Kata ya Sigino, uliona Kata nzima hawana maji kabisa vijiji vyote vine. Tukiwafuata mnasema kuna fedha upande wa Wizara ya Maji, kuna TAMISEMI, wakati huo huo ceiling hazitoki mapema saa hizi Mabaraza wameshaanza kukaa kwenye bajeti, ceiling hazijulikani. Toeni ceiling mapema, lakini onesheni mapema kwamba Wizara ya Maji tunaweza tuka-access fedha hizo kwa kiasi gani? Kama tutaendelea kutokuweka mambo haya wazi, tutaendelea kuimba wimbo wa kwamba hakuna maji katika Taifa letu kwa miaka zaidi ya 50 na akina mama wanaendelea kuchota katika makorongo na ndoo hazijashuka katika vichwa vyao.