Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Rev. Peter Simon Msigwa

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Iringa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nami naona nijaribu kushauri na kutoa mchango wangu kuhusiana na agenda iliyo mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali kadhaa ambayo napenda kumuuliza Waziri wa Fedha kwamba katika Mpango huu, ni kwa namna gani mambo haya ameyazingatia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa letu toka tumepata uhuru, ni Taifa ambalo limekuwa tegemezi. Tumekuwa tukiendesha bajeti yetu na masuala mbalimbali ya kimaendeleo kwa kutegemea Wahisani au Wafadhili. Takwimu nilizonazo mpaka sasa ni kwamba kwa kipindi cha miaka 40, Jumuiya ya Ulaya imetoa zaidi ya Euro bilioni tatu kusaidia shughuli za kimaendeleo ambazo zimekuja kwa mfumo wa Kiserikali. Ukiacha mashirika kama Maria Stops na mashirika mengine kwa mfano kutoka Uingereza, hivi vyote vimekuja kuchangia na vimesaidia sana kukuza maeneo ya elimu, miundombinu na afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye eneo la afya, Marekani na mashirika yake mengi sana yamesaidia sana Sekta ya Afya kusaidia wauguzi wetu namna ya kutatua kero mbalimbali za afya. Vile vile Kiserikali, mashirika kama DFID kutoka UK, USAID, UNFPA inayoshughulika na idadi ya watu duniani, haya yote yametoa michango kwa ajili ya kuisaidia nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunataka Taifa ambalo linajitegemea na tumekuwa tukijinasibu sana kwenye vyombo vya habari kwamba tunataka Taifa liwe la kujitegemea, kitu ambacho ni kizuri. Napenda Waziri wa Fedha aniambie, ni namna gani mpango wake una-reflect kuachana na huu utegemezi wa muda mrefu ambapo toka tumepata uhuru tumekuwa tukiwategemea hawa watu? Katika kipindi cha miaka kumi tumepoteza watoto zaidi ya 600,000 ambao wamekufa kwa utapiamlo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa letu sasa hivi kila saa moja mama mmoja mjamzito anakufa. Maana yake ni kwamba kwa mwaka tunapoteza akinamama wajawazito 9,000. Ni namna gani Mpango huu una-reflect kwamba tutahama kutoka kwenye hii hali ambapo tunapoteza watoto na akinamama wajawazito? Huduma ya afya kwa kiwango chote tunaitegemea kutoka nje!
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Taifa hili asilimia karibia 50 ya watoto wanaozaliwa ni stunts. Kuna mental retardation ya kutosha katika nchi; na wanasema pale anapokuwa mtu mmoja amedumaa, kuna watu wengine ambao wana mental retardation watano. Ni namna gani Mpango huu una-reflect kujaribu kuliokoa Taifa hili kwenye maeneo haya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa ambalo Kambi ya Upinzani imezungumza, ni jinsi ambavyo Mpango uliopita ulitekelezwa kwa asilimia 26 tu. Mheshimiwa Waziri, kabla hatujaenda mbele, you know speed is useless if you don’t know where you are going or if you lost. Kabla hatujaenda mbele unapotuletea huu Mpango, ni kwa nini Mpango uliopita tumeshindwa, ulitekelezwa kwa asilimia 26? Vitu gani vilisababisha tushindwe? Ni hatua gani zimechukuliwa? Kwa nini tulishindwa? Kwa nini hatutashindwa katika Mpango huu? Ni namna gani yale ambayo yalitushinda miaka iliyopita tutayarekebisha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya kabla hatujaenda mbele ni lazima tuwe na majibu ya kutosha. Kabla hatujaparamia huu Mpango tuanze kuupitisha, tuambiwe ni kwa nini tulishindwa na kwa nini hatutashindwa kwenye Mpango unaokuja?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Upinzani imezungumza kwamba tunapopanga mipango lazima iwe inaendana na mazingira, kuna mipango mingine ni kweli huwa inakuwa imposed, haiendani na uhalisia wetu. Huu Mpango wako unasema nini kuhusu kuendeleza Sekta ya Utalii ambayo inachangia asilimia 25 ya fedha za kigeni? Vile vile asilimia 17 zisizo na kodi, yaani GDP Mpango wako unasemaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu gani? Kumekuwa na uvamizi na nashukuru sasa hivi Waziri wa Ardhi amekuja; kumekuwa na uvamizi wa mifugo, wafugaji wamevamia maeneo mengi ambayo ndiyo yanakuza Sekta ya Utalii ambayo kimsingi ndiyo yanatuletea pesa nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tena na Waziri wa Mifugo yupo hapa! Nchi yetu ina asilimia 10 kwa ajili ya ufugaji. Kwa bahati mbaya haya mashamba makubwa mengi ambayo tulitenga asilimia kumi kwa ajili ya ufugaji yamehodhiwa na watu wachache ambao kimsingi hayatumiki. Sasa maeneo haya yamesababisha hawa wafugaji waanze kuondoka sehemu ambazo tumezipima. Sasa zinaathiri kwenye hunting industry, zinaathiri kwenye National Parks wakati hii ardhi ipo, haijapangwa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshangaa juzi Waziri wa Maliasili anahangaika na tumbili wale waliokamatwa KIA. Ni kweli sikubaliani wanyama wasafirishwe ovyo ovyo, lakini ukiangalia tumbili na athari zinazopatikana kwa wavamizi wafugaji wanaopeleka kwenye maeneo ya uhifadhi, ni athari kubwa sana kuliko tumbili ambao tunahangaika nao pale KIA. Ni sawa na nyumba inaungua moto, watu badala ya kuokoa vyombo, vinateketea, wewe unamshangaa binti aliyevaa sketi fupi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ndiyo Serikali yenu! Hatuna priorities! Hii Sekta ya Utalii ndiyo inaiingizia Taifa asilimia 25 ya fedha za kigeni. Wafugaji najua wanapiga kelele sana, sio kwamba siwapendi, najua wengine watainuka hapa! Ufugaji katika nchi hii unachangia one point seven ya GDP, halafu mnaleta mchezo na inayochangia asilimia 17, hapa balance iko wapi? Naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha anipe majibu, mmejipangaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Iringa Mjini kwenye Sekta ya Utalii, hii Southern Circuit mlituambia katika Bunge hili kwamba tunataka na Southern Circuit kuwe na utalii, lakini Iringa Mjini pale ni mahali ambapo pamekaa kimkakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumelalamika sana miaka mitano hapa kwamba ule uwanja wa ndege uharakishwe, ujengwe vizuri na barabara ya lami ijengwe mapema iwezekanavyo kwenda kwenye Mbuga ya Ruaha ya National Park ambayo kimkakati ni hii Sekta ya Utalii. Sasa kumekuwa na maneno mengi, mara mnawapiga mkwala hawa wafadhili ambao wanatusaidia; Mheshimiwa Mpango umesema tunaweza kujitegemea, mmekejeli hata zile fedha za MCC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekwambia hii ni nchi ambayo watoto wanakufa kwa utapiamlo. Tuambieni hii mikakati yote kwa miaka 40 tumetegemea fedha za kutoka Ulaya, mmejipangaje kujiondoa kwenye eneo hili? Naunga mkono tujitegemee, lakini tuwe realistic, tunaachanaje na kujitegemea? Tunatoa elimu ambayo ni spoon feeding! Ni elimu ya watu ambao wanamaliza shule lakini hawana mchango! Tunasomesha wachumi ambao hawana uchumi, wanataka wafundishe uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kwenda kujifunza uchumi, bora niende kwa Mangi kwenye kaduka kake atanifundisha uchumi kuliko nimpate mchumi mwenye degree kwa sababu hana uchumi yeye mwenyewe, hawezi kuleta chakula mezani. What kind of economics is that? Huo Mpango wako ni lazima tuwe na majibu haya, ni namna gani tutapunguza vifo vya akinamama wajawazito? Huu Mpango tunataka utupe majibu ni kwa kiwango gani tumeshidwa miaka mitano iliyopita?
Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 26 ni ndogo sana. Utupe majibu ya kutosha! Nami najua, tulikwambia mapema kabisa, wewe sio mwanasiasa, lakini sasa hivi naona siasa imeanza kuingia, unatoa majibu ya kisiasa. Tunataka utupe majibu ya uhalisia! Kama kweli tunajifunga mkanda, tujue tunajifunga mkanda kwa kiwango kinachotosha. Tuambiane ukweli! Zama za kudanyanyana hazipo, tuambiane ukweli kwamba hela hii walikuwa wanatusaidia Wamarekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema ukifuatilia hizi hela, afya ya nchi hii tumeikabidhi kwa Wamarekani, hatuna uwezo huo! Nimetaja haya mashirika yote ya Kiserikali, achilia mbali hizi NGOs ambazo zote zinaleta pesa kusaidia akinamama. Haya ndiyo mambo ambayo Bunge tunatakiwa tujadiliane na tuambiane ukweli hapa! Kinachonishangaza kikubwa, ni kwa kiwango gani tunacheza na Sekta ya Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutengeneze Mpango in our context. Utalii ndiyo unaotuletea pesa nyingi katika nchi yetu, lakini matokeo yake, tunacheza na mifugo. Bahati mbaya wenzetu wa Kanda ya Ziwa, they speak a lot, wana influence. Akina Musukuma hawa wanaongea sana, wangependa hata hifadhi zile zote waingie wanyama tu. Nakubaliana kwamba mifugo ni ya muhimu katika Taifa letu, lakini hatuwezi! Hii inachangia one point seven GDP, tukaua inayochangia seventeen. Yaani tunaua uhifadhi kwa kiwango kidogo kwa sababu ya kufurahisha watu kisiasa. Naomba Mpango huu u-reflect ni namna gani tuta-boost uchumi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tunataka tuwe na uchumi wa kati, lakini ukiangalia idadi zote mlizotupa, wasomi tunaowaandaa katika sekta mbalimbali, kwa mfano, utalii una-boom katika nchi yetu. Sioni wale wanaohusika na industry hii tumewaandaa kwa kiwango gani; wale wanaohusiana na gesi tumechukua sababu za makusudi kiasi gani kuwaandaa kwa ajili ya uchumi wa baadaye badala ya kuleta siasa?
Mheshimiwa Waziri naomba haya maswali yangu niliyokuuliza kwenye Mpango wako, ina-reflect kiasi gani ili tuwe wahalisia, tusifanye vitu vya kubahatisha na siasa? Sasa hivi tumemaliza uchaguzi, hebu tuingie kwenye uhalisia, tusiende kwenye siasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ninavyozungumza, bandari kwa taarifa zenu wenyewe, imeshuka kufanya kazi kwa kiwango cha asilimia 50. Wateja wengine kutoka Kongo wameondoka, wanakimbilia Beira. Haya mambo tutawezaje kuyafikisha kwenye uhalisia kama hatuambizani ukweli? Nasi kwenye Ilani yetu ya Uchaguzi tulisema angalau one third ya bandari ndiyo yangekuwa mapato ya Taifa. Sasa hivi tumeshashusha asilimia 50.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba uchumi pamoja na siasa mnazozifanya, hebu tu-balance kuwe na uwiano kati ya business na politics. Naona mizania ya siasa inapanda zaidi kuliko uchumi. Hebu tu-balance, kwa sababu mwisho wa siku, huu ni mtumbwi, tumepanda wote. Kama mwenzetu umeanza kutoboa, tutazama wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba haya majibu yasawazishwe ili kwa pamoja turidhiane, tuishauri Serikali. Waziri wa Ardhi unanisikia, Waziri wa Mifugo unanisikia, bahati mbaya Waziri wa Maliasili hayupo, naomba m-balance haya mambo; kwa sababu siku moja nimemsikia Waziri wa Maliasili na Waziri wa Mifugo, kulikuwa na sintofahamu kidogo katika eneo hili. Mimi wale tumbili hata mngeacha waende, hakuna shida. Ingekuwa tembo au faru, hiyo sawasawa. Wale Tumbili si sawa na Kweleakwelea! Wapo wengi tu, tungeuza tupate hela; lakini mnaacha uhifadhi, ng‟ombe wanakwenda kule, wanaharibu uhifadhi! Hii ni kwa ajili ya vizazi vyetu vya baadaye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hayo tu machache, nimejaribu kusaidiana kidogo katika hilo. Ahsante sana.