Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na namshukuru Mheshimiwa Mwakajoka kwa kunipa dakika tano. Nami nianze kuchangia kwenye suala zima la mamlaka makubwa ambayo nafikiri RC na DC na DAS wanazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafurahi sana kuona leo kwa sababu mwaka jana hapa wakati sisi Wabunge wa Kambi ya Upinzani tunajaribu kuonesha matatizo na changamoto na udhaifu ambao baadhi ya RC na DC wanayo katika maeneo yetu, tulibezwa hapa, hatukusikilizwa lakini leo humu baadhi ya Wabunge wa CCM nao wameona hiyo shida na wameanza kusema. Nafikiri huu utakuwa ni mwanzo mzuri ili tuendelee kuelewana sawasawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema kwamba hawa RC na DC wamekuwa Miungu watu, wameona kwamba wana mamlaka makubwa kuliko mtu yeyote, hawatambui nafasi za Wabunge, wanaweza ku-revoke maamuzi ya Baraza na kuyaingilia, hata pale ambapo hayastahili. Ifike mahali hizo semina elekezi ambazo mlizisema zimefutwa nadhani iko haja ya kurudisha na kukaa na hao watu na kuwaambia. Siyo semina tu, hata akili nyingine tu ya kawaida ya busara ya RC au DC kujua mipaka yake, kujua namna ya kushirikisha hawa watu hawana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima muangalie mfumo mwingine, sijui wateuliwe wengine au wafanye nini hawa wameshindwa kazi, wamekuwa Miungu watu. RC anakaa kwenye kikao anaongea anasema, nadhani mnaelewa hapa kuna Waziri naweza kuwa na maamuzi makubwa kuliko Waziri hata Waziri mwenyewe anaelewa, anasema kwenye kikao na Waziri yupo, huyu ni RC. Sasa kama wanasema vitu kama hivi mbele ya Mawaziri unategemea nini kwa Wabunge?(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, RC anakuja kwenye eneo lako, Wabunge mnaomba kuonana nae hana muda na Wabunge. Haya ni masikitiko, lakini sasa angalau tunaanza kuelewana humu ndani na angalau haya machungu na ninyi Wabunge wa CCM mmeanza kuyapata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utawala wa sheria; sioni sasa kama kuna utawala wa sheria. Kuna Mbunge mmoja ameongelea kuhusu mlundikano wa kesi au mlundikano wa wafungwa Magerezani, lakini leo kama kuna kesi ya uchochezi ya mwana CHADEMA haichukui miezi mitatu hukumu tayari na inasikilizwa haraka sana, lakini kuna watu wamekaa gerezani kwa kesi ama za kusingiziwa au ambazo siyo za kisingiziwa miaka tisa, miaka 10, miaka mitano, miaka miwili wanasema upelelezi bado, lakini mwana-CHADEMA akisema jambo tena anaambiwa mchochezi na hii tafsiri ya uchochezi itabidi mtuambie uchochezi ni nini maana yake neno uchochezi linatumika vibaya, anaambiwa ni mchochezi, anapelekwa Mahakamani haraka hukumu miezi sita, miezi nane, miezi mitatu jela.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sidhani kama kuna utawala wa sheria, ni lazima mjitafakari upya, muangalie kama tuna Katiba, kama tuna sheria, kama kweli kuna kutenda haki kwa nini haki inatendeka kwa watu wachache na watu wengine wananyanyaswa kwa sababu ni washabiki wa upande fulani au wa Chama fulani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie suala la mwisho kuhusu Madiwani; Madiwani wamekuwa ni Wasaidizi wetu hata sisi Wabunge kwa maana kama tukiwa hapa Bungeni kwenye vipindi virefu vya Vikao vya Bunge, wao ndiyo wamekuwa wakikaa na wananchi na wakiwasikiliza kero zao, lakini Madiwani wamesahaulika. Madiwani leo wanapewa posho ya sh. 350,000 basi na hizo posho za vikao, tena wako Wakuu wa Wilaya wengine wanafuta posho za Madiwani ambazo zingine ziko kwa mujibu wa taratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Wakuu wa Wilaya wengine wanasema posho hii haitakiwi, hii haitakiwi, kweli kuna zile ambazo haziko kwa mujibu wa taratibu, lakini zile zilizoko kwa mujibu wa taratibu DC wanaingilia, wanazifuta. Tumewasahau Madiwani, hatufikirii kuwaongezea posho zao, tumewaacha Madiwani hawapewi mafunzo, capacity building haipo tena, angalau kwenye awamu zilizopita walikuwa wanapewa. Sasa unampeleka Diwani asimamie mradi wa mabilioni, yuko kwenye Kamati ya Fedha lakini hajajengewa uwezo.