Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na mimi kwa kupata nafasi walau dakika tano hizi niseme machache ambayo nadhani yanaweza kutusaidia kuendelea mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kuungana na mapendekezo ya Kamati zote mbili nikiamini kwamba ni moja ya maeneo muhimu sana ambayo kama Serikali itayafanyia kazi tunaweza kupiga hatua ambayo tunaitarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ninavyofahamu mimi suala la ukaguzi, katika Halmashauri zetu, Taasisi zetu na maeneo mbalimbali ambayo kwa kweli CAG anapaswa kufanya kazi huko zinasaidia kuimarisha utendaji bora na matumizi bora ya fedha za Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa pamoja na uimarishaji huo, kama Kamati hizi mbili kama ambavyo zote zimesema haziwezi kupewa nguvu ya kufanya kazi ya kwenda field na kukagua kilichopo itakuwa bado ni sawa na kupiga mark time. Sababu moja kubwa ya msingi, kupata Hati Safi hakumaanishi yale yote yaliyofanyika yana ubora wa kiwango kinachostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana tunaamini kupata Hati Safi ni uandishi mzuri wa vitabu, lakini Kamati zinapokwenda field zinakutana na vitu tofauti; toka asubuhi Wabunge wameongea hapa. Sasa tunafikiri upo umuhimu, tunaamini kwamba, mambo haya yakifanyika vizuri sina shaka tutakuwa tumefikia malengo ambayo yametarajiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kubwa zaidi, limezungumzwa suala la miradi kutokamilika kwa wakati. Naamini katika Halmashauri zote nchini miradi mingi sana ilianza. Hapa imetajwa miradi ya maabara, ikaja ya miradi ya vituo vya afya, zahanati, madarasa na kadha wa kadha. Vyote hivi, kama haviwezi kupelekewa fedha kwa wakati ni lazima tutakuwa tunakutana na hoja za ukaguzi mara kwa mara na hatuwezi kufikia malengo kwa kweli ambayo wananchi wanatazamia kuyaona sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Fedha za Mfuko wa Vijana na Wanawake; liko tatizo na mimi sina shaka Mheshimiwa Simbachawene atakuwa analifanyia kazi suala hili vizuri akishirikiana na Mheshimiwa Jenista kwa sababu moja tu ya msingi kwamba, fedha hizi imekuwa ni tabia, fedha hizi imekuwa ni mazoea, hazitoki kadri sheria inavyosema na Wakurugenzi wamefanya kama fedha hizi ni za miradi ya kwao pekee yao, si fedha za Serikali kwa mujibu wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, ningeomba uwekwe utaratibu tena ikiwezekana kwa maandishi kuisisitiza sheria hii kwamba ikiwezekana kila mapato ya mwezi yanayopatikana hata kama vitakuwa vinapata vikundi vitano mpaka 10, lakini mwisho wa mwaka watakuwa wana kiasi kikubwa ambacho wameshakitoa na itakuwa inaonesha uhalisia wa kile tunachokizungumza.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijana hawa ambao sisi tunaotokana na Chama cha Mapinduzi tumetoa ahadi nyingi na ahadi hizi kwa vikundi mbalimbali ambavyo vimeshaundwa kama haziwezi kutekelezeka bado tutakuwa hatuna maneno mazuri ya kuwaridhisha wananchi hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye Kamati ya PAC yapo mambo mengi hapa yamezungumzwa na muda uliopita huko nyuma tulisema hapa, kwamba pamoja na CAG kupisha bajeti ambayo tumeipitisha kwenye Bunge hili, lakini ipo miradi, kwa mfano ipo mikataba mikubwa, mikataba ambayo kipato chake tunaamini ni mgawanyo wa Taifa hili. Kwa hiyo kama hatutaweza, kwa mfano, mikataba ya gesi, CAG asipoweza kwenda kukagua huko na haya tunayoyaona bado hatuwezi kuona kile ambacho tunakitarajia miaka 10, miaka mitano ijayo katika kuhakikisha tunamsaidia Mtanzania huyu ambaye ni maskini sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine ni juu ya Kamati kushindwa kufanya kazi. Kamati hizi haziwezi kufanikiwa, Kamati hizi haziwezi kuleta matunda chanya kwa sababu kama nilivyosema, upatikanaji wa Hati Safi ni uandishi bora wa vitabu. Wako wahasibu mabingwa wa kuandika vitabu vizuri. Tutaendelea kusifia Hati Safi lakini miradi kule nyuma ni hewa, miradi haitekelezeki, miradi imekufa. Ni lazima tuhakikishe Kamati hizi zinakwenda kukagua miradi ambayo tunadhani imetumia fedha nyingi za Serikali na kodi ya wananchi pia katika kuhakikisha tunamsaidia Mtanzania huyu ambaye ni maskini na mnyonge.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kwa sababu ya muda; suala la PSPF, fedha nyingi bado hazijalipwa, tunafahamu Serikali imejiwekea mkakati wa kulipa zaidi ya bilioni 150…
Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru na naunga hoja mkono.