Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

Hon. Maulid Said Abdallah Mtulia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

MHE. MAULID S.A. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kuwepo hapa na kuchangia jambo hili. Pili, nikushukuru kwa kunipa fursa hii.
Kwanza, nianze kusema naunga mkono taarifa zetu hizi nzuri kabisa zilizoandaliwa na Kamati zetu hizi kubwa mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuweka rekodi sawa lakini kubwa kuliko yote kuonesha kwamba sisi watu wa Kinondoni tuliwahi kuonja matunda ya UKAWA. Matunda yale tuliyaonja katika gogoro kubwa linaloonekana kwamba Manispaa na Halmashauri hazichangii 10% za vijana na wanawake. Chini ya aliyekuwa Meya wetu wa UKAWA, Ndugu Boniface Jacob, Manispaa yetu ya Kinondoni ambayo imeitwa manispaa sugu imefanikiwa kutoa pesa shilingi bilioni 2.4.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie wenzangu kama sisi Wabunge tukishirikiana na Madiwani wetu na Wenyeviti wetu wa Halmashauri au Mameya tukawa na nia ya dhati, hizi pesa zinatoka na sisi kwetu Kinondoni zimetoka. Niwaahidi wananchi wa Kinondoni vyovyote itakavyokuwa bila kujali mabadiliko yoyote yaliyotokea tutahakikisha mwaka huu wa fedha 2016/2017 tutatoa pesa shilingi bilioni 6.4 kwa sababu makusanyo yetu ya ndani ni takribani shilingi bilioni 64. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna masikitiko hapa, tulikuwa tumekadiria kukusanya property tax shilingi bilioni 10 kwa Manispaa yetu ya Kinondoni. Leo Mheshimiwa Waziri ameondoa kodi hii kutoka manispaa ameipeleka TRA na mpaka sasa ndiyo kwanza wamepeleka vibarua vya kuwataarifu watu kwamba wanadaiwa, tuna masikitiko makubwa sana. Kwa kuondoa hii shilingi bilioni 10 maana yake wananchi wa Kinondoni, vijana na wanawake mmewakosesha shilingi bilioni moja ambayo kama wangegaiwa shilingi milioni hamsini, hamsini, ni wananchi 20,000 mmewakosesha pesa hizi. Ni hasara kubwa sana kwetu sisi watu wa Kinondoni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri kama atashindwa kurejesha hii property tax kukusanywa katika Halmashauri basi walau arejeshe katika Manispaa. Kwa sababu kwenye Manispaa pesa nyingi zitapotea, kwa sababu Majiji yana majengo makubwa yenye thamani kubwa tofauti wakati mwingine na Halmashauri yenye majengo madogo. Kwa hiyo, tusije tukaipoteza hii fursa kwa kupoteza mapato mengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili napenda niishauri Serikali kama wajibu wetu wa msingi, imeelezwa hapa katika ripoti ya PAC tuna Shirika letu la NSSF. Katika mashirika yetu ya hifadhi hili ni shirika kubwa sana. Hili shirika lina utajiri wa shilingi trilioni 3.8. Shirika hili lina miradi 40 ambayo tayari iko kwenye utekelezaji. Shirika hili limepata mabadiliko, limepata Mkurugenzi mpya na ni mtu mwenye uwezo, Profesa, lakini kwa masikitiko makubwa Wakurugenzi nane ambao walikuwa wanafanya kazi na Mkurugenzi huyu wamesimamishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, yawezekana kuna mambo yamesemwa na nashukuru ripoti imeeleza vizuri, lakini imekuja kueleza vizuri suala la Dege Eco Village na imeeleza kwamba si kweli ardhi imenunuliwa kwa milioni 800 kama inavyoandikwa kwenye magazeti wakati mwingine, kilichotokea pale ni kwamba ardhi ile heka 300 imeingizwa kama capital na yule mwekezaji Azimio amepata 20% ya mradi kwa kutoa viwanja 300; siyo kapewa pesa milioni 800 kwa heka, siyo kweli. Kwa thamani ya mradi share atakayopata 20% wameigawanya kwa viwanja ikaonekana milioni 800 wakati siyo utaratibu. Utaratibu na huu sio mgeni, hata National Housing wamewahi kuingia mkataba na TPDC na wamepata 25% katika jengo lile kubwa pale la Mkapa Tower na kiwanja cha heka moja ni sawasawa na bilioni 4.5. Sasa huu ni utaratibu wa kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini masikitiko yangu au ushauri wangu naotaka kumpa dada yangu pale Mheshimiwa Waziri mhusika ni kwamba shirika kubwa kama hili akapewa Director mgeni, Wakurugenzi wake nane ambao walikuwa wanasaidiana na Mkurugenzi aliyeondoka, wanaojua uendeshaji wa shirika hili wakakaa pembeni akawa Mkurugenzi mpya anachukua na Wakurugenzi wake wengine wapya, tunapoteza pesa zetu, yaani shilingi trilioni 3.8 tunaziweka rehani. Hawa watu wanatakiwa wawepo wamsaidie, kuna kaka yangu Magoli, kaka yangu Kidula, Wakurugenzi wapo pale waende wakamsaidie.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine tunapata hasara kwenye mashirika yetu ni kwa sababu hatujali thamani ya kile kitu tulichonacho. Hii inatuletea matatizo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri afanye kila hali Wakurugenzi hawa wamsaidie Mkurugenzi wetu Mkuu ili uchumi wetu usiyumbe.